Mashirika ya ndege ya Air France na KLM yamekabiliwa na adhabu ya jumla ya dola za Marekani 425,000 (takriban bilioni 1.2 kwa fedha za kitabzania) baada ya safari zaidi ya 130 za ndege kuingia katika anga inayodhibitiwa na Iraq zikiwa chini ya kimo cha futi 32,000, kinyume na masharti ya usalama wa anga yaliyowekwa na Marekani.
Kwa mujibu wa Idara ya Uchukuzi ya Marekani (USDOT), Air France ilihusika katika safari zaidi ya 30, huku KLM ikihusika katika zaidi ya safari 100 zilizofanyika kati ya Januari 2022 na Mei 2025.
Safari hizo zilikiuka vizuizi vilivyolenga kupunguza hatari kwa ndege za kiraia zinazopita katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro ya kikanda.
Kutokana na ukiukaji huo, Air France ilitozwa faini ya dola 105,000, huku KLM ikitozwa dola 320,000. Kati ya jumla ya faini hizo, dola 265,000 zinapaswa kulipwa, wakati dola 160,000 zilizobaki zinategemea kutotokea kwa ukiukaji mwingine ndani ya kipindi kilichowekwa.
Hata hivyo, mashirika hayo yalipinga kuwajibika moja kwa moja kwa mabadiliko ya kimo cha ndege, yakieleza kuwa marubani wao walikuwa wakifuata maelekezo ya watawala wa usafiri wa anga.
CODESHARE ILIVYOYAFANYA MASHARTI YA MAREKANI KUHUSIKA
Ukiukaji huo ulihusisha safari za ndege zilizokuwa na namba za utambulisho wa Delta Air Lines, licha ya ndege hizo kuendeshwa na Air France na KLM.
Hali hiyo inahusiana na utaratibu unaojulikana kama codeshare, ambapo shirika moja la ndege huruhusu shirika mshirika kutumia namba yake ya safari kwenye huduma inayotekelezwa na shirika jingine.
Katika tukio hili, safari hizo zilibeba namba za Delta Air Lines, Amercan Airlines, na hivyo kuhusishwa na masharti ya usalama wa anga ya Marekani yaliyokuwa yanatumika kwa huduma hizo.
View attachment 3697886