Tupatieni Katiba Yetu
Kelvin Kachingwe
LUSAKA, Okt 28 (IPS) - Shinikizo linazidi kupanda kwa ajili ya katiba mpya inayoainisha maoni ya wananchi wakati ucheleweshaji wa kuandaa rasimu hiyo bado unaendelea.
Pamoja na kwamba Kongamano la Taifa la Katiba (NCC) liliongezewa muda wa miezi minne kutoka ombi la kwanza la miezi 12, shinikizo inazidi kupanda kwa chombo hicho kukamilisha katika muda uliowekwa ili nchi ipate fursa ya kuendesha uchaguzi mwaka 2011 chini ya katiba mpya.
Zoezi la kuandika rasimu ya katiba mpya ambalo liliwashirikisha wananchi katika mijadala, lilianzishwa na rais aliyefariki Levy Mwanawasa. Lengo lilikuwa kuizuia serikali pekee kupitisha Katiba ya Jamhuri kinyume na demokrasi.
Chombo cha NCC, ambacho kilianzishwa mwaka 2007, kilitakiwa kuandika rasimu ya katiba ambayo ingesubiri maoni ya wananchi katika kipindi cha mwaka mzima.
Lakini ilipofika katikati ya mwaka 2009, NCC iliomba mwaka mmoja zaidi ili kufanikisha zoezi. Rais Rupiah Banda, ambae ana mamlaka ya kukubali ametoa miezi minne tu badala ya 12 iliyoombwa.
Akitangaza kuhusu kuiongezea muda dhamana ya NCC wakati wa uzinduzi rasmi wa bunge mwezi uliopita, Rais Banda amesema anasikitishwa na jinsi mambo yanavyoenda polepole.
Tilyenji Kaunda, mtoto wa rais wa kwanza, Dr Kenneth Kaunda na kiongozi wa chama cha upinzani cha United National Independence, anasema NCC haina budi kumaliza kwa haraka kazi yake katika muda uliowekwa ili uchaguzi mkuu ujao ufanyike chini ya katiba mpya.
"Katika vikao vyake vijavyo, NCC hazima ihakikishe inamaliza kazi kwa sababu wananchi wengi wa Zambia wana shauku kuona katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu ujao," amesema katika mkutano na vyombo vya habari mapema mwezi huu.
Chama cha upinzani cha United Party for National Development (UPND) kinasema kwamba kina wasiwasi kwamba muda ulioongezwa wa mchakato wa katiba mpya ni ishara kwamba nchi haitakuwa na katiba mpya wakati wa uchaguzi mwaka 2011.
"Iwapo tutaendelea kuongeza muda wa NCC, kuna uwezekano wa kutokuwa na katiba mpya mwaka 2011 kwa sababu bado kuna mazoezi mengine kadha ambayo yanatakiwa kufanyika hususan kuendesha kura ya maoni, ndio maana kuongezwa kwa muda sio dalili nzuri kwa taifa," Charles Kakoma, mwenyekiti wa habari na uhamasishaji wa UPND anasema.
Hata hivyo, msemaji wa NCC, Mwangala Zaloumis anasema kuongeza muda ni muhimu kwa sababu mbalimbali ambazo zimeifanya NCC kushindwa kufikiria ripoti za kamati sita kati ya 11 ambazo chombo kilistahili kuzipitia wakati wa kipindi cha mwaka mmoja wa mamlaka hayo.
"Kuongeza muda kulisababishwa na mambo mengi, baadhi ya hayo ni kifo cha Rais Mwanawasa mwaka uliopita, kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa rais na vile vile mabadiliko ya hivi karibuni katika mzunguko wa bajeti. Wakati Bunge linaendesha kikao chake, NCC hairuhusiwi kufanya kazi," Zaloumis amesema.
Profesa Patrick Mvunga, mwanasheria wa katiba, anasema kwamba kuharakisha mchakato wa kutayarisha katiba mpya kwa sababu ya uchaguzi mkuu mwaka 2011 hakutaweza kuleta matokeo mazuri yaliyokusudiwa.
"Ni vizuri kila wakati kufanya kazi nzuri, na kazi nzuri lazima iende na wakati. Iwapo sababu kubwa ya kuwa na katiba ni kwa ajili ya uchaguzi, wale wote wanaotaka katiba ikamilishwe badala yake waiambie NCC wamalize kuzishughulikia sheria zote zinahohusu uchaguzi," Profesa Mvunga anasema.
" Kama ni muhimu hivyo, ingebidi vipitie vifungu vinavyohusiana na uchaguzi na ndio maana sielewi pale watu wanaposema kwamba lazima tuwe na katiba kabla ya uchaguzi mwaka 2011 kwa sababu sio vifungu vyote katika katiba vinahusu uchaguzi, sio mambo yote katika katiba ni uchaguzi."
George Kunda, makamu wa rais nchini alisema mwaka uliopita kwamba NCC itamaliza kazi yake ifikapo Desemba 2009 ili taifa liwe na katiba mpya kabla ya uchaguzi mwaka 2011 lakini aliongeza kwamba mchakato lazima uwe wenye uhalisi na sio wa kuharakisha.
"Hatuwezi kuhujumu mchakato kwa kupendekeza muda usio halisia. Tutamaliza kati kabla ya 2011, lakini tusipendekeze muda ambao hauendani na kazi yenyewe," amesema.
Mwezi Julai 2008, kikundi cha vyama vya vyama hiari, katika barua walioiandikia sekretarieti ya NCC na kunakili kwa Rais, Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu, ilidai kwamba kongamano limalize kazi yake ifikapo mwishoni mwa mwezi Julai 2009 na kutoa ripoti ya fedha ya kina kuhusu matumizi ya fedha za umma tangu ilipoanzishwa.
Mashirika yamesema kwamba NCC ilibidi kumaliza kazi yake mara moja ili kutoa fursa kwa zoezi jingine linalohusu ya kupitishwa kwa katiba, hususan Kura za Maoni, liweze kufanyika kabla ya uchaguzi mwaka 2011.
"Zoezi kubwa kama hilo haliwezi kuachiwa lifanye kazi bila kuwa na ratiba maalum…na ili kuonyesha uwajibikaji na uwazi, tunataka ripoti ya fedha kutoka NCC na matumizi yake," ilisomeka sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa na baadhi ya wawakilishi kutoka Transparency International Zambia, Citizens Forum, Women in Law Southern Africa na Southern African Centre for Constructive Resolution of Disputes.
Kujibu hoja hiyo, mwenyekiti wa NCC Chifumu Banda alisema kwamba kongamano ni taasisi ya serikali ambayo hukaguliwa na Mkaguzi Mkuu.
"Katibu wa NCC ndie afisa mdhibiti pamoja na mafungu yote yanashughulikiwa na watumishi wa serikali. Matumizi yetu yatawekwa wazi kwa wananchi," amesema.
Lakini Michael Sata, kiongozi mkorofi wa upinzani kutoka chama cha Patriotic Front anapinga kuongezewa muda NCC na anatoa changamoto kwa chombo hicho kuonyesha maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa.
"Kila mtu NCC, hawako pale kutayarisha katiba, wako pale kugawana dola milioni 80 zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Watatumia kila sababu kuhakikisha kwamba ‘wanazimaliza' dola milioni 80 kwa ajili ya vikao," Sata amesema.
Situmbeko Musokotwane, waziri wa fedha, katika hotuba yake ya bajeti mwezi uliopita, ametenga fungu jingine la dola milioni 1 kwa ajili ya NCC baada ya rais kuongeza muda wa mamlaka hiyo kwa miezi mingine minne.
Mapema mwaka uliopita, katibu wa NCC Russell Mulele alisema kwamba ingawaje rais ana mamlaka ya kuongeza mamlaka baada ya muda wa miezi 12 kumalizika, watahakikisha kwamba wanakamilisha kazi hiyo katika muda uliowekwa ili uchaguzi mkuu mwaka 2011 ufanyike chini ya katiba mpya.
Banda anasema ana imani kubwa kwamba katiba mpya itakuwa tayari kabla ya uchaguzi mkuu.
"Hatutarudi nyuma kwa sababu tumetoka mbali na tunakaribia ukingoni kukamilisha zoezi la katiba," Banda anasema.
"NCC ina muda maalum ukiondoa siku ambazo Bunge linafanya kikao, siku za mapumziko na siku za mwisho wa wiki, isingekuwa hivyo na maombolezo ya Rais Levy Mwanawasa, tungefika mbali."
Kupitishwa kwa Sheria ya NCC kunatokana na mapendekezo ya wananchi kwa Kamati ya Kupitia Katiba ya Wila Mung'omba kwamba katiba ipitishwe na Bunge, Kongamano la Katiba au chombo kingine chochote kinachoaminika ambacho kitawakilisha mawazo ya wananchi. (END/2009)
Someni kwa Wazambia jamani Wapo juu kutuzidi sisi kwanini tubaki nyuma jamani?