Ndugu zangu naomba nianze kwa kunukuu kiapo cha Rais John Pombe Magufuli siku ile ya tarehe 05/11/2015 mbele ya Jaji Kiongozi Mh. Mohamed Chande Othman katika uwanja wa Uhuru baada ya kutangazwa mshindi wa Urais na Tume ya Uchaguzi chini ya Jaji mstaafu Damian Lubuva.
1. Mimi John Pombe Joseph Magufuli naapa kwamba nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
nitalinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyowekwa kisheria. Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie.
2. Mimi John Pombe Joseph Magufuli naapa nitatenda kazi zangu za Urais wa Jamhuri ya Tanzania kwa uaminifu kwa kutimiza wajibu wa kazi hizo kwa bidii na moyo mkunjufu na kwamba
nitawatendea haki watu wote kwa mujibu wa sheria, mila na desturi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila woga, bila upendeleo, huba wala chuki. Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie.
3. Mimi John Pombe Joseph Magufuli naapa katika
kutekeleza madaraka niliyopewa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie.
Sasa...
Pamoja na Rais John Pombe Magufuli katika awamu yake ya kwanza kushindwa kuilinda, kuitetea na kuiheshimu Katiba ya Jamhuri ya Tanzania kama alivyoapa, anapata wapi ujasiri wa kuwaangalia Watanzania kwa ujumla wao usoni na kuwaomba wamuongezee awamu nyingine? Ili iweje?
Ili azidi kuisigina Katiba kwa kutotenda haki kwa Watanzania wote kwa mujibu wa sheria, mila na desturi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila woga, bila upendeleo, huba wala chuki? Huu uthubutu anautoa wapi?
Pamoja na Rais John Pombe Magufuli katika awamu yake ya kwanza kuruhusu uwepo wa kikundi kinachodaiwa cha wasiojulikana kuwateka, kuwatesa na kuwapoteza raia wema wa taifa hili, anapata wapi ujasiri wa kuwaomba raia wenye hofu na usalama wao wamuongeze miaka mingine mitano? Ili iweje?
Ili wasiojulikana waendelee na vitendo vyao viovu dhidi ya raia wema wa nchi hii kwa kuwadhulumu haki yao ya msingi ya kuishi kwa uhuru, amani na usalama wao na mali zao bila hofu na woga? Huu uthubutu anautoa wapi?
Pamoja na kijana mwana harakati Ben Saanane kupotea na hadi leo haijulikani aliko katika awamu yake ya miaka mitano, Rais Magufuli anapata ujasiri wapi wa kuwatazama usoni familia yake, wazazi wake, ndugu zake, rafiki zake na Watanzania wenzake na kuwaomba wampe kipindi kingine? Ili iweje?
Ili azidi kuwatisha vijana kama Ben Saanane kwamba kwa kutumia uhuru wao wa maoni kikatiba katika kuikosoa serikali na kiongozi wake mkuu wanahatarisha maisha yao hivyo wawe tayari kupotezwa? Huu uthubutu anautoa wapi?
Pamoja na mwandishi wa habari Azory Gwanda kupotea katika mazingira tatanishi na juhudi kushindikana za kumpata, Rais Magufuli anapata wapi ujasiri wa kuwatazama usoni familia yake, jamaa zake, waandishi wenzake na Watanzania wenzake na kuwaomba wampe kura zao? Ili iweje?
Ili ujumbe uwafikie Watanzania na waandishi wa habari popote walipo kwamba kuandika habari zisizoipendeza serikali hii na kionozi wake mkuu ni kuhatarisha maisha ya huyo mwandishi? Huu uthubutu anautoa wapi?
Pamoja na kituo cha utangazaji cha ClousFM kuvamiwa usiku wa manane na kiongozi wa mkoa akifuatana na askari wenye bunduki na kutaka kituo kiandike habari anazotaka yeye, Rais Magufuli anapata wapi ujasiri wa kuomba muhula mwingine wa vitendo vya aina hiyo kuendelea? Ili iweje?
Ili vituo vya habari popote vilipo, visitumike kwa namna yoyote kuwapasha wananchi habari ambazo serikali hii na kiongozi wake mkuu hawataki katakata wananchi wazipate kwa namna yoyote ile? Huu uthubutu anautoa wapi?
Pamoja na Mbunge Mh. Tundu Antiphas Lissu kumiminiwa risasi mchana kweupe na kunyimwa stahiki na haki yake ya kutibiwa kama Mbunge, Rais Magufuli anapata wapi ujasiri wa kuwaangalia wapiga kura jimboni kwa Lissu na bila kupepesa macho kuwaomba kura azidi kuwa Rais wao? Ili iweje?
Ili wakae wakijua kuwa yaliyompata Mh. Tundu Antiphas Lissu yataendelea kama wapiga kura wa jimbo hilo wataendelea kuwa wakaidi na kumchagua mwakilishi wanayempenda na si wanayeletewa? Huu uthubutu anautoa wapi?
- Pamoja na mateso waliyopata wasanii kama Roma Mkatoliki wa kutekwa kuteswa na kudhalilishwa kote huko, bado Rais Magufuli ana ujasiri wa kipekee wa kuambatana na wasanii na wao kulazimika kumpigia kameni katika juhudi zake za kuomba kura aongezewe awamu nyingine, ili iweje? Hata sijui!
- Pamoja na mateso waliyopata wakulima wa korosho mkoani Mtwara, Rais Magufuli anategemewa kufika huko na kwa ujasiri usio wa kawaida, ngeni na usioambatana na Utanzania wetu, na kuwataka wana Mtwara kumpa kura aweze kuwaongoza tena kwa muda wa miaka mitano, ili iweje? Hata sijui
- Pamoja na mateso waliyopata wana Dar es Salaam kwa kuvunjiwa nyumba zao bila fidia na kulazimika kulala nje pamoja na watoto wao, Rais Magufuli anategemewa kuzuru eneo husika na kwa ujasiri usio wa kawaida kuwaomba wampigie kura katika uchaguzi ujao aendelee kuwa Rais wao, ili iweje? Hata sijui
- Pamoja na dhulma uliombatana na unyang'anyi wa wazi waliofanyiwa wafanya biashara nchini hadi kufilisiwa katika awamu hii ya miaka mitano, Rais Magufuli anategemewa kuzunguka Mtwara hadi Kagera, Unguja hadi Kigoma na kwa ujasiri uso kifani, kuwaomba kura zao waendelee kukamuliwa! Ili iweje? Hata sijui
- Pamoja na...ningeweza kujaza kitabu kizima.
Pamoja na pamoja yote hadi leo hatma ya Ben Saanane haijulikani, hatma ya Azory Gwanda haijulikani na hatma ya waliopotea haijulikani.
Pamoja na pamoja yote hadi leo waliomteka Roma hawajulikani, waliomteka MoDewji hawajulikani na waliommiminia Lissu risasi hawajulikani.
Pamoja na pamoja yote hatma ya wafanya biashara haijulikani, hatma ya wakulima (wa korosho) haijulikani na hatma ya wafanya kazi haijulikani
Pamoja na pamoja yote CCM ni ile ile, mgombea wa Urais kutoka CCM ni yule yule, Katiba ni ile ile na wasiojulikana bado hawajulikani.
Pamoja na pamoja yote Rais Magufuli anaomba kura na akichaguliwa ataapa tena kiapo kile kile. ...je Watanzania wenzangu tutapona?
Hakika uthubutu wa Rais John Pombe Magufuli si tu hauna mfano, ni ngeni na nakataa si wa Kitanzania.