SoC04 Mageuzi ya kimfumo na kiteknolojia yanahitajika katika Wizara ya Ardhi ili kukabiliana na kero za ardhi

SoC04 Mageuzi ya kimfumo na kiteknolojia yanahitajika katika Wizara ya Ardhi ili kukabiliana na kero za ardhi

Tanzania Tuitakayo competition threads

Jobstata

New Member
Joined
May 29, 2024
Posts
2
Reaction score
1
Wizara ya ardhi ni miongoni mwa sekta nyeti sana ambayo mtu yeyote anayepewa nafasi ya kuiongoza wizara hii hapaswi kucheza nayo hata kidogo mathalani viongozi wa vijiji na watendaji wote katika mipaka yao wanapaswa kutambua madhara ambayo yanaweza kujitokeza endapo hawatatilia mkazo juu ya umakini hasa linapokuja suala la nani anapaswa kumiliki ardhi, kwa taratibu gani na kwa muda gani.

Ukosefu wa umakini, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka vimegharimu maisha ya wengi kutokana na migogoro ya ardhi, mbali na madhara ya kibinadamu pia inaathiri uchumi wa taifa letu.

Mara kadhaa tumesikia wawekezaji wanaondoka na mitaji yao kisa urasimu wanaokutana nao pindi wanapotaka ardhi ya kuwekeza biashara mbalimbali.

Kwa mfano, jiji la Dodoma ni jiji linalokua kwa kasi sana hasa baada ya serikali kuhamishia shughuli zake katika makao makuu ya nchi Dodoma, mahitaji ya ardhi yameongeza huku gharama pia iongezeka maradufu.

Lakini uwepo wa fursa hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la migogoro ya ardhi kutokana na uporaji wa ardhi wa baadhi ya maafisa ardhi wasio na waadilifu, mfano Novemba 27, 2023 Waziri wa ardhi yumba na maendeleo ya makazi Mhe. Jerry Silaa aliwasimamisha wapima ardhi wawili kwa kosa la kupora ardhi ya inayomilikiwa na kanisa la Moraviani mtaa wa Itega jijini Dodoma. Chanzo ITV digital.

Changamoto hiyo haipo katika jiji la Dodoma pekee bali katika maeneo mengine ya Tanzania kama ambavyo tumeshuhudia waziri Silaa akitokwa jasho katika kukabiliana na wanyang’anyi wa ardhi. Ili kukabiliana na changamoto hizo serikali kupitia wizara ya ardhi inaweza kufanya yafuatayo.

Matumizi ya Tehama.
Serikali iboresha miundombinu ya teknolojia kwa kuhakikisha kunakuwa na mifumo ya kisasa ya kidijitali inayorahisisha taratibu za upimaji na umilikishaji kwa ufanisi zaidi.

Aidha ianzishe matumizi ya GPS kwa ajili ya kupima na kufuatilia mipaka ya ardhi, kuweka vituo vya data ambavyo vitapatikana kwa urahisi kwa wadau wa ardhi, kuwe na programu za usimamizi wa mali za ardhi ili kuongeza ufanisi wa shughuli za umiliki wa ardhi.

Kuongeza uwazi katika mchakato wa utoaji hati.
Wizara ya ardhi inaweza kuongeza uwazi katika mchakato ya utoaji hati kwa kuwashirikisha wadau wafuatao, serikali ya eneo husika, Maafisa wa ardhi, wamiliki wa ardhi, Wanasheria wa ardhi na Wanajamii wa eneo husika. Kwa kufanya hivyo hatuwezi kusikia kiwanja au shamba limeporwa au kuuzwa kwa mununuzi zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja.

Pia wizara ya ardhi inaweza kuongeza uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa utoaji wa hati za umiliki wa ardhi kwa kutekeleza kwa kuweka mfumo wa kidijitali wa usajili wa ardhi ili kupunguza ucheleweshaji na urasimu, kuwezesha upatikanaji wa taarifa za umiliki wa ardhi kwa umma kwa njia ya mtandao kadhalika kuwapa mafunzo watumishi wa ardhi ili kuhakikisha wanazingatia maadili na uwazi katika kazi zao pia kutumia vyema miundombinu ya teknolojia.

Kupunguza gharama za upatikanaji wa hati.
Serikali inaweza kupitia upya vipengele ambavyo vinakwamisha upatikanaji wa hati miliki ya ardhi kwa wote, Watanzania wengi ili kumudu gharama za upimaji pamoja na upatikanaji wa hati ni lazima awe na mali nyingine au auze sehemu ya ardhi hiyo , waliowengi kutokana na hali ya kipato duni wanaishi au wanamiliki maeneo ambayo hayajarasimishwa na hivyo kuwa rahisi kuporwa.

Aidha Serikali inaweza kupunguza gharama za hati kwa kuboresha mifumo ya usajili na kutoza ada za usajili ambazo ni nafuu kwa wananchi. Pia, inaweza kuhakikisha taratibu za kupata hati zinakuwa rahisi na kuepuka rushwa au urasimu usio wa lazima. Hatua hizi zitasaidia kuhakikisha kuwa gharama za hati zinakuwa za nafuu na zinapatikana kwa urahisi kwa wananchi wote.

Kutatua migogoro ya ardhi kwa haki na kwa haraka zaidi.
Migogoro ya ardhi suala la kulipa kipaumbele sana katika jamii ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza endapo haitatatuliwa kwa wakati na kwa haki. Ni muhimu kuhakikisha kwamba migogoro hiyo inatatuliwa kwa njia ya haki na kwa haraka ili kuzuia migogoro zaidi na kudumisha amani na ustawi wa jamii.

Serikali na wadau wote waliotajwa katika kipendele ‘B’ hapo juu wanaweza kutumia njia mbalimbali za kutatua migogoro ya ardhi ikiwa ni pamoja na mazungumzo, upatanishi kwa kutumia mabaraza ya ardhi na mahakama. Ni muhimu kwa serikali na jamii kwa ujumla kuhakikisha kwamba mifumo ya kutatua migogoro ya ardhi inaboreshwa ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote na migogoro inatatuliwa kwa haraka zaidi.

Mwisho.
Mbali na kutumia taknolojia na kuboresha mifumo yote ya utoaji hati na utatuzi wa migogoro, jamii pia ipewe elimu namna bora ya kupata ardhi bila kuzalisha migogoro, maafisa ardhi kuongeza uwajibikaji na uwazi, taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa iwe macho kubaini yanayoendelea kwenye sekta ya ardhi na kuchukua hatua madhubuti ili kukomesha tatizo la rushwa.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom