========
Vifungu hivyo ni kinyume na Katiba, vinakiuka Ibara ya 21(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi mbele ya jopo la majaji watatu, Jaji John Mgetta, Jaji Dk. Benhaji Masoud na Jaji Edwin Kakolaki baada ya kupitia maombi ya kupinga vifungu hivyo vya Sheria ya Uchaguzi na majibu ya wajibu maombi.
Naibu Katibu Mkuu wa ACT - Wazalendo, Joram Bashange, aliwasilisha maombi dhidi ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika maombi yake Bashange aliambatanisha hati ya kiapo aliyoapa na mjibu maombi alijibu akiambatanisha na hati ya kiapo kinzani kilichoapwa na Fausta Mahenga.
Katika maombi yake Bashange anapinga uhalali wa kikatiba wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura. 343 na kifungu cha 45(5) na 13(7) cha Sheria ya Uchaguzi Serikali za Mitaa sura ya 292.
Inadaiwa kuwa vifungu vilivyopingwa vinaruhusu kupita bila kupingwa mgombea ubunge na udiwani kuwakilisha jimbo na kata huku mgombea pekee wa urais huchaguliwa kwa kura ya siri na sio kama aliyetangazwa kuwa amechaguliwa bila kupingwa.
Katika hoja zake Bashange anadai kwa kuruhusu wagombea wasio na upinzani kama ilivyosemwa hapo awali, vifungu vinavyopingwa vinakiuka haki za raia kupiga kura kuwachagua wawakilishi na kushiriki katika masuala ya umma kupitia kuchaguliwa wawakilishi wa bunge na mamlaka za serikali za mitaa.
Inadaiwa masharti hayo yanakiuka ibara ya 21(1) na (2) na Ibara ya 26(1) ya Katiba.
Kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 21(1) bila kuathiri masharti ya Ibara ya 39, 47 na 67 ya Katiba ya Sheria za nchi kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa au kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, kila raia wa Jamhuri anayo haki ya kushiriki ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria.
Ibara ya 21(2) inasema kila raia anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi wa mambo yanayomuhusu yeye, maisha yake au yanayolihusu taifa.
Ibara ya 26(1) inasema kila mtu ana wajibu wa kufuata na kuitii Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano.
Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili iliangalia vile vile katika Ibara 76 na 77(1) ya Katiba kuhusu matakwa ya kufanya uchaguzi katika kila jimbo na wananchi kushiriki katika uchaguzi huo kwa kina.
Ibara ya 76 inasema kila baada ya Bunge kuvunjwa kutakuwa na uchaguzi wa wabunge katika majimbo yote ya uchaguzi.
Ibara ya 77(1) ya Katiba inasema wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi watachaguliwa na wananchi kwa kufuata masharti ya Katiba hiyo na vile vile masharti ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba kuhusu wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi.
"Kwa athari hiyo mbunge jimbo lolote lazima achaguliwe kwa uhuru na wananchi isipokuwa kama kuna kizuizi kinachoruhusiwa na Katiba kumzuia raia kutumia haki ya kupiga kura.
"Kifungu cha 77(1) kinahusika, kinaonyesha wabunge wanaowakilisha maeneo ya majimbo lazima wachaguliwe na wananchi kwa mujibu wa Katiba na sheria iliyotungwa na Bunge, kwa mujibu wa Katiba ya kusimamia uchaguzi wa wajumbe wa Bunge linalowakilisha majimbo ya uchaguzi.
"Tunakubaliana na mwombaji kwamba sheria iliyotungwa kudhibiti uchaguzi wa wabunge wanaowakilisha maeneo inapaswa kuzingatia maagizo ya Katiba ambayo kwa lazima kutoa haki ya kupiga kura kama njia ya kupata wabunge wa Bunge linalowakilisha majimbo ya uchaguzi," lilisema jopo.
Jopo lilisema katika kupitia Katiba hawakuweza kupata chochote kinachoruhusu utaratibu unaohitaji wagombea ambao hawajapingwa au wasiogombea kuchukuliwa na kutangazwa.
Mahakama inasema kutokana na hoja zilizotangulia mwombaji anayo hoja ya kutosha kuonyesha kuwa masharti yaliyopingwa yanakiuka ya kifungu cha 21 cha Katiba inapoanzisha mambo mapya au hali zinazowabana watu kutumia haki ya kupiga kura kumchagua mgombea aliyependekezwa na chama katika jimbo au kata ambayo kuna mgombea pekee.
"Sisi tunakubaliana na mwombaji kwamba masharti yaliyopingwa ni kinyume na dhamana ya kikatiba ya haki ya kupiga kura iliyowekwa chini ya kifungu cha 21," lilisema jopo.
Mahakama ilisema katika hoja za wajibu maombi haijaonyeshwa jinsi masharti yanayopingwa yanavyofaa ndani ya madhumuni yoyote ya utoaji haki, haikuonyeshwa jinsi uokoaji wa gharama za serikali kwa kutojihusisha na uchaguzi na mgombea aliyependekezwa hapigiwi kura kuwa iko ndani ya vipengele vyovyote vya ibara ya 30(2) ya Katiba kama wanavyodai.
Jopo lilisema hata kama imeonyeshwa hivyo, bado Mahakama haijashawishika kwa kuwa mwombaji anachotafuta katika maombi yake ni kuhusu anayelalamikiwa, mfumo huo unaathiri maslahi ya umma.
Pia hawaoni kitu chochote halali ambacho kilikuwa kinakusudiwa kuafikiwa katika sheria hiyo zaidi ya kuanzisha kundi la wabunge na madiwani waliotangazwa kuchaguliwa bila kupingwa kitu ambacho hakijakusudiwa kwenye Katiba.
"Kwa kuzingatia upungufu katika hoja za wajibu maombi kuhusu utumikaji wa masharti ya kuokoa gharama, tunakubali kuwa masharti yaliyopingwa hayapo katika ibara ya 30(1) na (2) ya Katiba kama inavyodaiwa na walalamikiwa.
"Tunakubali kuwa vifungu vilivyopingwa vinakiuka Katiba na wajibu maombi hawakuweza kutoa uthibitisho wa
kuonyesha kwamba masharti yaliyotajwa ni muhimu na yamo katika kifungu cha 30(2) cha Katiba.
"Katika suala hili, hatuna chaguo lingine isipokuwa kuzingatia ibara ya 64(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kuhusu masharti yaliyopingwa.
"Mahakama inaona hoja zilizowasilishwa zinatosha kuondoa vifungu vinavyopingwa kwa manufaa ya mwombaji.
"Kwa sababu zilizotajwa hapo juu, maombi yanakubaliwa, tunatangaza kwamba masharti ya kifungu cha 44 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura 343 na vifungu 45(2) na 13(7) vya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali ya Mitaa, sura ya 292 ni kinyume cha Katiba hivyo basi ni batili kwa kukiuka masharti ya ibara ya 21(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama ilivyorekebishwa mara kwa mara," lilisema jopo.
Chanzo: Nipashe