Ni kweli dunia ina nguvu zake katika mfumo wa maisha yetu hapa duniani. Kuna watu wenye roho mbaya wasiopenda maendeleo ya watu wengine, hufanya jitihada za kuwakwamisha wenzao, lakini inafika muda nguvu za ulimwengu huwazidi na mtu wanayemkwamisha huibuka kwa kwa njia za ajabu mpaka wao wanashangaa!
Wakati mwingine Mungu huwatumia haohao wabaya wako kama daraja la mafanikio yako pasipo wao kujua. Adui tusiwachukie, kwani huenda huyo ndio njia yako. Siri za Mungu binadamu hatuzijui, hivyo tusifanye mambo kwa kiburi; kwamba yote tunatajua wenyewe kumbe kwenye mfumo haiko hivyo.
Tusiwe na ghadhabu juu ya wenzetu, kwani huwezi kujua wakati (siku gani) utakuwa wapi na utakabiliwa na nini na utahitaji msaada toka kwa nani. Huenda huyo unayemchukia leo ndio atakuwa msaada pekee siku utakapobananishwa, na utamumuona mfalme siku hiyo!
Samsoni alipokuwa anasafiri nyikani kwenda kwa ndugu zake, alivamiwa na simba, alipambana na simba na kufanikiwa kumuua, akamtupa pembeni ya njia na kuendelea na safari.
Siku ya pili akiwa anarudi nyumbani kwake, akiwa njiani, alishikwa na njaa kali sana, kiasi cha kuishiwa nguvu. Huku akiwa hana tumaini la kupata chakula (maana alikuwa nyikani), alipofika mahali alipomuua simba, akakumbuka na kumtazama pale pembeni ya njia alipomtupa.
Akaona kama kuna nyuki wanaruka pale, akaamua kusogea karibu na ule mzoga wa simba aliyemuua jana yake. Lahaula! Akakuta masega ya asali yaliyonona yamejipanga kwenye mzoga ule! Basi, akapakua na kula asali ile mpaka akashiba, na akabeba asali nyingine nyumbani kwa ajili a mama.
Hivyo, kumbe adui yako anaweza kugeuka msaada kwako! Simba aliyetaka kumuua Samsoni amekuwa nyumba ya nyuki ya kutengenezea asali. Unaweza kuona Mungu anavyotenda maajabu. Usiulize inawezekaje asali ikatengenezwa kwa siku moja!