Hizi ni double standards za ajabu kabisa! Huko Zimbabwe Jongwe anafanza uchaguzi wa kiinimacho (ambao majeshi yanatangaza KABLA ya uchaguzi kuwa hayatakubali rais mwingine zaidi ya Jongwe), hakuna anayepeleka majeshi! Somalia, kwa miaka zaidi ya 15 hakuna serikali, ni mabwana wa vita (warlords) wanapokezana mji mkuu wa Mogadishu na hata nchi nzima imegawanyika kiwango kisichotawalika, OAU iliwaachia Marekani (ambao waliumbuliwa vibaya), na sasa uwepo wa majeshi ya AU hauonekani wala haieleweki kama nayo ni ajenda ya AU au la! Kule Togo kulikuwa na jamaa akiitwa Gnassingbe Eyadema, alipindua nchi akiwa na umri wa miaka 31, na akatawala kwa mkono wa chuma hadi alipojifia mwenyewe akiwa na umri wa miaka 69 baada ya kutawala miaka 38. Jeshi la nchi likamteua mwanawe Faure, kinyume kabisa na katiba na taratibu za utawala, kurithi urais wa baba yake. Hakuna AU iliyosema chochote! Nao pia wakafanya uchaguzi wa "danganya toto" (sawa tu na huo aliofanya Col Mohamed Bacar huko Anjuan, Comoro), lakini hakuna AU iliyoinua pua kusema kuna chochote kilichotokea, au kumtaka aachie ngazi! Na huyo Col Mohamed Bacar huko Comoro wala hajapindua serikali ya Comoro, amechukua madaraka na kuitisha uchaguzi katika kisiwa kimojawapo kinachounda shirikisho la Comoro (ambalo lina marais watatu kama sikosei, yeye ni mmojawapo kati ya hao watatu, tatizo ni kuwa serikali kuu haikubaliani na jinsi alivyopata madaraka). Sasa inaelekea "tunakaonea" haka ka-kisiwa, kiasi tunajua wapiganaji 1,800 (kama batallions 2 tu) wanatosha kuwafyatisha mkia. Bob Denard alikuwa anatumia wapiganaji 150 tu (hazifiki kombania 2) kusambaratisha visiwa vyote hivyo! Au kuna dili fulani jama hatuambiwi? Nani katoa dau hilo Col Bacar apigwe? Kinachonishangaza ni kuwa hata AU walipoamua kuwa inapaswa kupeleka jeshi Darfur, nchi nyingi zilizojitolea kupeleka majeshi zilikuwa zinasuasua kupeleka askari wao, wakidai wanasubiri kuhakikishiwa financing (hela haikuwepo!) Uganda walianza kujitolea kwa hela yao kabla hata fungu halijaingia kwa sababu zao za kiusalama na Sudan, wakatanguliza ndege moja na askari. Hizi hela za "fastafasta" za kuwahisha majeshi Comoro zimetoka wapi?