Nimeisoma hoja ya mwandishi nguli na mwanasheria, Paschal Mayalla, akihoji:
"Nani alitoa amri ya kufyatua risasi?" Ni haki yake kikatiba kutoa maoni, lakini kama mwanasheria na mtu aliyekulia kwenye mikono ya mfumo wa usalama (tukimkumbuka mzee wetu Mayalla, Mungu amrehemu), Paschal anajua fika kuwa swali lake ni la upendeleo linalokwepa mzizi wa tukio.
Paschal anataja "risasi" kana kwamba Polisi waliamka asubuhi na kuamua kufanya mazoezi ya shabaha kwa raia. Anasahau makusudi kutaja mazingira yaliyopelekea matumizi ya nguvu.
1. Mazingira ya Uhalifu: Zaidi ya Maandamano
Kabla ya risasi hazijalia, kulikuwa na mfululizo wa matukio ya kihalifu ambayo Paschal na baadhi ya viongozi wa dini wamepata "upofu" wa ghafla kuyaona:
- Kuchomwa kwa Vituo vya Polisi: Hivi ni vituo vyenye maghala ya silaha. Unapovamia na kuchoma kituo chenye silaha za moto, unatangaza vita na umma.
- Uvamizi wa Miundombinu: Uvamizi wa ATM na vituo vya mafuta (Petrol Stations). Hapa hatuzungumzii maandamano ya amani; tunazungumzaji uhujumu uchumi na uporaji.
2. Mchanganyiko wa Damu: Maandamano, Uasi, na Mapinduzi
Mhamasishaji mkuu kutoka ughaibuni alitangaza wazi kuwa siku hiyo ina mambo matatu:
Maandamano, Uasi wa Jeshi, na Mapinduzi. Kitaalamu, mchanganyiko huu unaitwa
Reflexive Control—mbinu ya kijasusi ambapo adui anasoma saikolojia yako na kukufanya uchukue hatua itakayokuharibu wewe mwenyewe. Lengo lilikuwa ni kutengeneza maaafa (damu) ili "wakubwa" wa ulimwengu wapate sababu ya kuingilia kati (International Intervention). Paschal anajua hili ni mchezo wa kijasusi, kwanini anakaa kimya?
Kwanini viongozi wa dini na wasomi wenye PhD hawakulaani mchanganyiko huu wa uasi na mapinduzi? Ukikaa kimya wakati nchi inachomwa, unatoa baraka kwa vijana wetu kutolewa kafara kwa mradi wa watu wa nje.
3. Jibu la Kisheria: Je, Amri Ilihitajika?
Swali la Paschal ni la kitoto kisheria. Kwenye mazingira ya shambulio la hatari, sheria inatoa mamlaka (Mandatory Power):
- Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16, Kifungu cha 18A na 18B: Inatoa haki ya Self-Defense (Ulinzi Binafsi) na ulinzi wa mali. Askari anayevamiwa akiwa analinda ghala la silaha au kituo cha mafuta hahitaji kumpigia simu Kamanda wake kuomba amri; sheria inamtaka kuzuia uhalifu huo kwa nguvu inayostahili ili kuzuia maafa makubwa zaidi.
- Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi (Police Force and Auxiliary Services Act): Inampa askari mamlaka ya kutumia silaha kuzuia mtu yeyote anayetaka kutoroka na silaha au anayevamia eneo la hatari.
Watu wanapochoma kituo cha mafuta katikati ya mji, wanataka kuua maelfu ya watu. Unahitaji amri ya nani kufyatua risasi kuzuia mlipuko huo?
4. Uhaini na Uasi: Makosa ya Jinai Yaliyofichwa
Paschal kama mwanasheria anakwepa kusema ukweli huu:
- Uhaini (Treason): Kutangaza "Mapinduzi" dhidi ya Jamhuri ni kosa la Uhaini chini ya Kifungu cha 39 cha Kanuni ya Adhabu. Hili ni kosa la kunyongwa.
- Uchochezi wa Uasi (Inciting Mutiny): Kutaka Jeshi liasi ni kosa chini ya Kifungu cha 45 cha Kanuni ya Adhabu. Ni kosa la jinai lenye adhabu kali.
- Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 28: Inamtaka kila raia kulinda mamlaka, uhuru, na umoja wa nchi. Kitendo cha kuhamasisha mapinduzi ni uvunjaji wa moja kwa moja wa Katiba.
Hitimisho
Nashangazwa na ukimya wa viongozi wa dini. Je, PhD zenu hazikuona hatari ya kuchanganya "Dini" na "Mapinduzi"? Paschal Mayalla, kwa kukwepa maswali ya kwanini vituo vya silaha vilichomwa na kwanini uasi ulihamasishwa, unatuacha na wasiwasi:
Kuna nini kinafichwa?
Vijana wetu wametolewa kafara na watu waliojificha nyuma ya kioo cha simu ughaibuni. Paschal, badala ya kuuliza nani aliamuru risasi, uliza:
"Nani aliamuru vijana wetu wakachome vituo vya mafuta na kuvamia maghala ya silaha?" Hilo ndilo swali la mzalendo.
Tanzania ni nchi ya kisheria. Jamhuri itajilinda, na sheria itasimama dhidi ya uhaini wowote, iwe ni wa kalamu au wa barabarani.