Kula mle kuuliza tusiwaulize?
Lula wa Ndali-Mwananzela
Disemba 30, 2009
BENKI Kuu wanataka kula tena; wanataka kula bila kuulizwa na yeyote; wanataka kula huku tukiwatazama. Si huku tunawatazama tu bali wanataka wale huku tukiwapigia makofi kwa jinsi gani wanakula vizuri.
Habari kuwa Benki Kuu imetumia zaidi ya shilingi bilioni moja na nusu kujenga upya nyumba ya gavana wake ni habari za ulaji mwingine kwenye taasisi hiyo ulaji ambao walaji wake hawataki waulizwe!
Habari hizi zilizoripotiwa na gazeti moja la kila siku nchini zinadokeza kuwa Benki Kuu imetumia fedha hizo katika kumpatia Gavana wa Benki hiyo Profesa Benno Ndulu jumba la uhakika linaloendana na hadhi ya Gavana (wa Tanzania). Ingawa habari hizo zilidai kuwa fedha hizo zilitumika katika ukarabati siku chache baadaye gavana mwenyewe alijitokeza na kudai kuwa fedha hizo (au zaidi) hazikutumika katika ukarabati kama gazeti hilo lilivyodai bali zilitumika katika ujenzi mpya wa jumba la Gavana.
Ndullu alinukuliwa kudai kuwa "Nyumba haijakarabatiwa, imejengwa from the ground (kutoka chini)... ni tofauti kukarabati na kujenga nyumba mpya huu ni upotoshaji wa wazi na kujaribu kuchafua mema" na hivyo kuhalalisha matumizi hayo ya fedha. Lakini zaidi alionekana kuchukizwa kwa kupatikana kwa habari hiyo akidai kuwa "Napenda taarifa sahihi ambazo hazipotoshi ukweli, kwa maana taarifa kama hizo zinaharibu kila kitu kizuri na kujengwa taswira mbaya kwa wananchi, kitu ambacho si sahihi. Pia si kweli kuhusu hizo gharama kwani hakuna tathmini kamili ambayo imekamilika hadi sasa".
Gavana Ndulu hakutaka kusema gharama halisi ya ujenzi wa jumba hilo ni kiasi gani na ni kwa nini ni kiasi hicho. Katika kufikiria suala hilo nimejikuta tena napigwa na bumbuazi la aibu; bumbuazi lililoniacha na maswali mengi kuliko majibu yake. Nilikuwa ninaamini kuwa mambo haya yalikuwa yanatokea wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa lakini sasa tunayashuhudia katika utawala wa Jakaya Kikwete na sitashangaa mwaka huu mmoja uliosalia tutaona mambo makubwa sana ya "ukarabati" hadi tunyofoe nywele zetu!
Ninajiuliza:
Profesa Ndulu amesema kuwa walichofanya si ukarabati bali ni ujenzi wa jumba jipya kabisa.
Ningependa kujua kabla ya ujenzi wa jumba hilo eneo hilo lilikuwa na nyumba ya aina gani na kwa nini ililazimika kuvunjwa? Jibu hili ni muhimu kwani tusipoangalia wakuu wa taasisi mbalimbali watakapopewa majumba ya waliowatangulia nao watataka kujenga majumba mapya. Hivyo, ningependa kupewa jibu kwa nini Gavana wa BoT alihitaji jumba jipya?
Kwa vile jumba hili linadaiwa kugharibu zaidi ya shilingi bilioni moja na nusu Gavana Ndulu anaweza kutupatia mchakato wa gharama za ujenzi wa jumba hili kiasi cha kuhalalisha matumizi makubwa ya fedha kiasi hicho?
Fedha zilizotumika zimetokana na mfuko gani? Swali hili ni muhimu kwani tangu habari hizi zimevuja kumekuwa na mjadala mkubwa wa fedha zilizotumika ni za walipa kodi au ni za Benki Kuu wenyewe na haziko katika usimamizi wa umma? Kama jawabu ni kuwa ni fedha za walipa kodi ni utaratibu gani ulitumiwa kuhalalisha hasa tukizingatia kuwa Gavana wa Benki Kuu ndiye pia Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo? Na kama ni fedha za "benki kuu" kama baadhi ya watu wanavyoamini tunajuaje kuwa mchakato wa matumizi yake hauna mazingira ya kifisadi?
Kutokana na swali hilo hapo juu, hatuna budi kujiuliza kama Benki Kuu yetu ilivyo sasa haina tofauti na Benki Kuu ya Dk. Daudi Ballali? Mojawapo ya matatizo tuliyoyashuhudia wakati wa Gavana Ballali ni uwezo wa Gavana yule kuhalalisha malipo na matumizi makubwa ndani ya benki hiyo kwenda kwa makampuni hewa na hivyo kuwa sehemu ya ufisadi mkubwa.
Je, Gavana Ndulu kwa kuhalalisha matumizi haya anaweza kuelezea kuwa yanaendana na thamani kweli ya ujenzi wa jumba hilo na kwamba uchunguzi huru ukifanyika utahalalisha matumizi hayo?
Je, Gavana Ndulu yuko tayari kufungua vitabu vya Benki Kuu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) au mkaguzi wa nje atakayeteuliwa na CAG kupitia mahesabu ya mapato na matumizi, hususan kwenye suala hili la ujenzi?
Katika kufanya hilo hapo juu, je, Gavana Ndulu anaweza kutuambia kuwa ujenzi huu wa hili jumba ulifanywa na kampuni gani iliyofanya hivyo kwa kushinda tenda gani iliyotangazwa lini na yenye vigezo gani?
Je, Benki Kuu inaweza kutuambia kuwa jumba hilo lililojengwa kwa fedha za Watanzania (ziwe zinazotokana na kodi yao au mtaji wao kwenye benki hiyo) lilitumia kiasi gani cha vifaa, ufundi, utaalamu, samani n.k kutoka ndani ya nchi yetu au ni yale yale ambapo hadi vitasa tunaagiza nje, mazuria nje, madirisha nje, makochi na vitambaa vya makochi kutoka nje?
Swali la mwisho ambalo ningependa kujua jibu lake ni kwa Gavana Ndulu kutuhalalishia kwa nini Gavana wa Tanzania akae kwenye jumba lenye gharama inayoshinda jumba la Gavana wa Benki Kuu ya Marekani, taifa kubwa zaidi lenye uchumi mkubwa na lenye matatizo ya kiuchumi ya kutosha tu?
Nina uhakika yapo maswali mengine lakini ningependa tuanze na haya. Napendekeza katika kuonyesha uongozi bora Waziri wa Fedha amwombe CAG kufanya ukaguzi wa haraka wa Benki Kuu hasa kwenye matumizi ya ujenzi na ukarabati wa majumba yao yote na kuona kama taratibu zimefuata na gharama inaendana na kile kilichofanyika au kudaiwa kufanyika (value for money).
Ndugu zangu Benki Kuu haina rekodi nzuri inapokuja kwenye masuala ya matumizi ya fedha zetu; imekuwa ni sehemu ya mtandao wa kifisadi na hadi hivi sasa hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa kuisafisha isipokuwa kubadilisha mapambo tu ya utendaji wa Benki hiyo. Tusipoangalia fedha za Uchaguzi Mkuu kwa chama kimoja nchini zitapatikana tena kwa mtindo huu huu wa ulaghai.
Ninachosema ni kuwa mkila tutawauliza, kama hamtaki tuwaulize…