JK,
Katika kitabu cha Abdul Sykes kuna simulizi za kusisimua kuhusu Vita Vya Pili Vya Dunia.
Naweka hapa vipande kidogo:
View attachment 3703014
Askari wa King's African Rfles (KAR) Burma Infantry 6th Battalion
kulia Abdulwahid Sykes na kushoto ni Ally Sykes
Askari waliondoka na meli kuelekea vitani kupitia Kilindini, Mombasa. Meli hizo zilisindikizwa na Jeshi la Wanamaji wa Uingereza (Royal Navy) ili kuzilinda na mashambulizi kutoka nyambizi hatari za Wajapani. Waafrika walikuwa wa kwanza kupelekwa Ceylon kwa mafunzo ya vita vya msituni kuunda lile jeshi lililokuja kuwa maarufu la askari wa miguu la Burma (Burma Infantry). Jeshi hili ndilo lililokuja kupigana na Wajapani. Jeshi hili la askari wa miguu liliundwa na Waafrika kutoka nchi nyingi. Lilikuwa na Waafrika toka Northern Rhodesia (Zambia), Southern Rhodesia (Zimbabwe), Belgian Congo (Zaire), Nigeria, Gold Coast (Ghana), Kenya, Uganda na Tanganyika. Baadhi ya askari hawa waliwahi kupigana Abyssinia, (Ethiopia) na Somaliland (Somalia) ambako Waingereza na Makaburu wa Afrika ya Kusini walipambana na Wataliani. Kutokana na kampeni iliyofanikiwa ya kikosi hiki nchini Abyssinia, ilionekana kuwa ni muhimu kuunda kikosi kama hiki kwa haraka. Hii ndiyo ilikuwa sababu ya serikali kutoa wito kutaka watu wa kujitolea kujiunga na KAR. Hawa Waafrika waliojitolea katika vita hivi walileta taathira kubwa na kusababisha ushindi wa Waingereza katika vita ile.
Wakati msafara wa Ally ulipokuwa baharini kuelekea Colombo, moja ya meli ilipigwa kombora na nyambizi ya Wajapani. Chombo hicho kilizama na kuwaua askari wote pamoja na maafisa wao Wazungu. Askari mmoja tu kutoka Tanga aliyekuwa akijulikana kama Magembe ndiye aliyenusurika. Askari kwenye meli zingine hawakujulishwa juu ya msiba huu hadi walipowasili Colombo. Maafisa Wazungu walidhani kuwa kama Waafrika wangejulishwa kuhusu msiba ule wakiwa bado katika bahari wangetaharuki na kuvunjika moyo. Licha yA Waafrika kujitoa muhanga, Wazungu waliwabagua askari weusi. Waafrika walipachikwa jina la ëmilitary labourí (vibarua wa kijeshi), wakati ambapo Wazungu kutoka Marekani na New Zealand walitambulika kama ëalliesí (washirika) ingawa wote walikuwa wanapigana vita moja chini ya amri moja.
Gazeti la jeshi lililokuwa likijulikana kama Second Enchelon, lililokuwa likichapwa kila wiki na kusambazwa katika kambi za majeshi ya washirika, lilichapisha jina na nambari ya Ally kwa makosa likidai alikuwa miongoni mwa wale waliokufa baharini. Ally alipofika kwenye kambi ya Kurnegala, nje kidogo ya Colombo, Abdulwahid alikuwa amekaa hapo katika kikosi cha Service Corps kwa zaidi ya mwaka mmoja. Kikosi chake kilikuwa kikishughulikia usafirishaji na mawasiliano. Abdulwahid alikuwa anasema lugha zote mbili- Kiingereza na Kiarabu- vizuri sana; kwa sababu hii alipandishwa cheo kutoka Koplo hadi kuwa Sergeant.
Abdulwahid alipata habari ya ''kifo'' cha mdogo wake katika gazeti hilo la jeshi na kumpelekea habari hizo za kuhuzunisha baba yake. Ilikuwa pale tu Ally alipowasili Kurnegala na kuzungumza na Abdulwahid kwa simu ndipo ilipotambulikana kuwa alikuwa yu hai. Ally anakumbuka ilikuwa jioni alipowasili kwenye kambi hiyo. Amri ya kutotembea usiku tayari ilikuwa imeshaanza kuzingatiwa. Saa hizo hakuna askari aliyeruhusiwa kuwa nje ya kambi. Abdulwahid alikuwa katika kambi nyingine karibu na hiyo aliyofikia ndugu yake. Habari zilipomfikia kuwa mdogo wake amewasili, alipata shauku ya kumuona ndugu yake. Abdulwahid alichukua gari na kutoka kambini bila ya dereva na hali amri ya kutotembea usiku ingalipo. Wakati ule Abdulwahid alikuwa amepandishwa cheo na kuwa "Quarter Master Sergeant" na sheria za kambi hazikumzuia yeye kutoka nje ya kambi wakati wa usiku. Ingawaje kwa kawaida alikuwa na dereva wa kumuendesha, Abdulwahid aliamua kuendesha mwenyewe jeep yake kwenda kumwona mdogo wake na kupata habari kutoka nyumbani. Majaaliwa ya binadamu yalivyo hayatabiriki, kwani dereva aliyekuwa akimuendesha Abdulwahid Burma,alikuja kushika nafasi ya juu katika Jeshi la Ulinzi la Watu wa Tanzania.
View attachment 3703018
View attachment 3703015
Burma Infantry
Askari kutoka Tanganyika na Zanzibar
(Waliosimama nyuma Ally Sykes wa pili kushoto)
View attachment 3703016