Shahidi wa tatu katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis inayowakabili maofisa Saba wa Polisi mkoani Mtwara; Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Yustino Mgonja amehitimisha ushahidi wake huku akichambua jinsi baadhi ya washtakiwa wanavyohusika katika tuhuma hizo.
ACP Mgonja ametoa uchambuzi huo wakati akijibu maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa utetezi na maswali ya ufafanuzi kutoka kwa mwendesha mashtaka, kuhusiana na maswali hayo ya dodoso, akihitimisha ushahidi wake leo jioni baada ya kusimama kizimbani kwa siku tatu.
Wakati wa tukio la mauaji hayo ACP Mgonja alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Mtwara na kwa sasa ni Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kipolisi Ilala jijini Dar es Salaam.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje; na aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Charles Maurice Onyango.