Serikali ya Zambia imesema jana Alhamisi kuwa imeahirisha kuanza kwa muhula mpya ya masomo kwa wiki tatu zaidi kutokana mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambao umeshaua watu 150 tangu Oktoba, 2023.
Waziri wa Elimu, Douglas Syakalima amesema shule nchini humo zilipaswa kufunguliwa Januari 8, 2024 lakini sasa zitafunguliwa Januari 29, 2024,
Zaidi ya watu 4,000 wameugua kipindupindu na vifo 150 vimeripotiwa, takwimu za hivi karibuni za Serikali zinaonyesha kiwango cha vifo ni asilimia 3.7.
Pia wagonjwa wapya 342 wameripotiwa katika saa 24 zilizopita, huku vifo 23 vikiripotiwa.
"Serikali ina wasiwasi kuhusu athari za mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika sekta ya elimu, hivyo hatua hiyo imechukuliwa ili kulinda afya za wanafunzi," amesema Syakalima.
Desemba, 2023 Zambia iliendesha kampeni ya kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na usambazaji dawa ya klorini ili kuua wadudu kwenye maji machafu.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wa kipindupindu kote ulimwenguni katika miaka ya hivi karibuni, huku Afrika ikiwa na hali mbaya.