KAMATI hiyo imejumuisha wajumbe 16, wakiwamo vigogo wa Simba na Yanga, Injinia Hersi Said na Salim Abdallah ‘Try Again’ na wachambuzi wa soka kama Jemedari Said, Oscar Oscar. Pia kuna Baba Levo, Joti, Mwijaku, Bongo Zozo, Seven, Prisca Kishamba, Beatrice Singano, Michale Nchimbi, Hamis Ali, Paulo Makanza, Mohamed Soloka na Hassan Raza.
.
Katika taarifa yake, Wizara inasema kamati hiyo ina lengo la kuhamasisha mashabiki na wapenzi wa michezo wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kuzishangilia na kuziunga mkono timu hizo pamoja na kuratibu hafla maalumu ya harambee na kuichangia itakayofanyika Januari 10, jijini Dar es Salaam.
.
Arena kama wadau wakubwa wa michezo hususani soka, tunadhani serikali inarudia kosa lilelile ambalo limewahi kutokea siku za nyuma kwa kuunda kamati hizi za kisiasa badala ya kuwekeza zaidi kuwa na timu bora zinazowahamasisha mashabiki na wapenzi kwenda wenyewe viwanjani.
.
Inawezekana serikali ina lengo zuri la kutaka kuona mashabiki na wapenzi wanaziunga mkono timu zao kwenye michuano zinayoshiriki, lakini kwa bahati mbaya ni kamati hizi hizi zimekuwa tatizo la kuzikwamisha timu hizo hata pale wanapokuwa wamebakiza hatua chache wafuzu michuano shiriki.
.
Zimekuwa zikivuruga saikolojia za wachezaji na kibaya zaidi zinaundwa na baadhi ya watu wasiojua mchezo wenyewe na wala hawana maajabu ya kusaidia kuhamasisha timu zifanye vizuri kwa sababu watu kwenda viwanjani au kuziunga mkono timu hizo haiwezi kuwa kitu kama timu haifanyi vyema.
.
Tunaamini serikali na hasa Wizara ya Michezo, ingekuwa ikiunda kamati kwa kushirikisha nyota wa zamani wenye rekodi zao ambao hata wakienda katika kambi ya timu hizo za taifa na kuzungumza na wachezaji zinaweza kuwaongezea nguvu ya kupambana viwanjani kuzibeba timu hizo kama ambavyo England wanafanya kuwahusisha kina David Beckham.
.
Mwaka 2019, iliundwa kamati kama hiyo na kupelekwa Misri kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) na kipi kilichoiletea mafanikio Stars zaidi ya kumaliza michuano bila pointi hata moja, lakini malalamiko yakiwa mengi kutokana na aina ya watu waliotumia fedha za serikali kwenda kwenye fainali hizo.
View attachment 2863209