Hatua ya Bandari ya Dar es Salaam kuwa chaguo la wawekezaji, imetajwa kuchagizwa na maboresho ya miundombinu yaliyofanyika na ujuzi wa wafanyakazi.
Vingine vinavyowavutia wasafirishaji kutumia Bandari hiyo kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ni uwepo wake katika jiografia sahihi na usalama wa mizigo.
Kulingana na TPA, huduma bora katika bandari hiyo ndizo zinazoifanya itumike kusafirishia vifaa mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ya Reli ya Kisasa (SGR) na mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP).
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana Jumapili, Januari 7, 2024 na Meneja wa Shehena ya Mizigo Mchanganyiko katika Bandari ya Dar es Salaam, Abel Garlus alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali.
Garlus ametaja maboresho yaliyofanyika katika bandari hiyo ni kununuliwa kwa vifaa maalumu vya kubebea mizigo yaani ‘folklift’ 98 na mitambo mikubwa miwili na ya kisasa ya kushushia makasha yaani ‘SSG’.
“Vitendea kazi hivi vimefanya sasa tuwe na mitambo yenye uwezo wa kubeba mzigo wa hadi tani 200 kwa wakati mmoja na kuifanya bandari yetu ya Dar es Salaam kuwa ya kisasa na yenye uwezo zaidi,” amesema.
Vingine vilivyopokelewa, alisema ni tani 7,000 za reli ya kisasa kwa ajili ya ujenzi wa loti ya tano na mabehewa 27 ya abiria.
Awali, akipokea vifaa kwa ajili ya maboresho ya bandari hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa alisema vitasaidia kuongeza ufanisi na uwezo wa bandari.
Alisema bandari za Tanzania kwa sasa zinaendeshwa katika hali ya ushindani kama zilivyo bandari nyingine duniani hivyo mazingira hayo yanachagizwa na mabadiliko ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji majini, teknolojia na uchumi.