mwanamwana
JF-Expert Member
- Aug 1, 2011
- 1,309
- 4,798
Fedha hizo zimepotea na hazijapata majibu kuanzia mwaka 2016, baada ya harambee iliyoongozwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Makonda ameelekeza TAKUKURU kumuhoji Mbunge Gambo kwa kuwa alikuwa ni miongoni mwa waasisi wa ukusanyaji wa fedha hizo.
Maelekezo haya ameyatoa leo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichowakutanisha wadau mbalimbali na taasisi za serikali.
"Fedha ni ngumu, tulishachangiwa hapa na matajiri shilingi milioni 400, iliwekwa kwenye akaunti, lakini ilipowekwa tukaambiwa kuwa hizi fedha ni za bodaboda na wametuchangia matajiri zetu hapa mjini. Tulipochaguliwa kuwa viongozi wa bodaboda na kwenda kuangalia kwenye akaunti hatukukuta hata shilingi mia moja, sasa tunauliza zimeliwa na nani? Mimi nilipambana hadi TAKUKURU," alisema mmoja wa viongozi wa waendesha bodaboda na kuongeza,
"Mbunge (Gambo) alielekeza shilingi milioni 120 iende kwa akina mama kwenye kikundi kinachoitwa UWAWAJA."
Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, amesema kwamba, alikumbana na madai ya upotevu wa fedha hizo hata alivyokuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi pindi alipofanya ziara katika mkoa huo.
"Hata nilipokuja hapa niliambiwa kuna hela za boda, sasa hivi mkiniambia kuwa mna milioni 20 ambazo Mheshimiwa Rais amechanga na mnatakiwa milioni 100 ili mpewe pikipiki, najiuliza hizi fedha zinazochangwa sasa zitakuwa salama vipi wakati zile milioni 400 hazijulikani ziko wapi?" aliongeza Makonda.
Kwa sasa, wananchi wanajiuliza ni nani alihusika na upotevu wa fedha hizo, huku matumaini yakielekezwa kwa TAKUKURU kufanya uchunguzi wa haki na kutoa majibu kwa umma.