Licha ya kuwa chimbuko lake bado linashindaniwa, Malkia wa Sheba – anaejulikana pia kwa jina la Makeda – ni jina muhimu kwa Waethiopia. Kwa wengi ni alama ya uzuri, upendo, amani, na mtu aliyependa kutafuta elimu na maarifa. Lakini kwa Waethiopia, Malkia wa Sheba kwao ni kila kitu. Kukutana kwake na Mfalme Sulemani miaka 3,000 iliyopita, ni jambo la kihistoria. Hii hapa hadithi yake.
Malkia wa Sheba aliishi lini?
Anaaminika aliishi zaidi ya miaka elfu tatu iliyopita.
Malkia wa Sheba anajulikana kwa lipi?
Kufuatia kiu chake cha kupata maarifa, malikia huyu anasemekana alimtembelea mfalme Sulemani wa Israel aliyekuwa na hekima nyingi mjini Jerusalem. Historia iliyoandikwa inadokeza kuwa malkia huyu alimzalia mfalme Sulemani mwana wa kiume ambaye alikuja kuwa mfalme wa kwanza wa Ethiopia wa utawala wa Kisulemani.
Tunajuaje kuhusu kuishi kwake? Tukio hilo la Jerusalem lilinakiliwa katika nyaraka mbali mbali ikiwemo bibilia na katika kitabu cha kale cha Ethiopia kinachojulikana Kebre Negast ambamo anajulikana kwa jina Makeda. Ametajwa na YESU pia katika agano jipya la Bibilia kama malkia wa Kusini.
Matayo 12:42
42 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kukihukumu kizazi hiki; kwa kuwa yeye alisafiri kutoka miisho ya dunia ili akaisikilize hekima ya Sulemani; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.”
Kebre Negast ni nini?
Kebre Negast mwanzo ilikusanywa katika karne ya kumi na nne nchini Ethiopia. Baadhi ya matukio yaliyomo katika nyaraka hizo yalitoka katika agano la kale na jipya, kutoka kwa Wamisri, Waarabu na Waethiopia. Kebre Negast inaeleza kwa undani kukutana kwa Malkia Sheba na Mfalme Sulemani. Hadithi hiyo inaeleza kuwa baada ya kumpa Makeda hekima yake, Sulemani alilala naye kwa usiku mmoja, tendo lililopelekea kuzaliwa kwa Mfalme Menelik wa kwanza, muasisi wa utawala wa Kisulemani nchini Ethiopia ambao uliendelea kutawala hadi Wakati Mfalme Haile Selassie alipoondolewa mwaka 1974.
Queen Of Sheba Palace Ethiopia