MWENYEKITI wa TLP, Augustine Mrema, ambaye katika siku za karibuni amekuwa akizungumzia sana masuala ya baadhi ya viongozi wa CCM, jana alitamba kuwa ana utajiri wa Sh37 milioni kwenye akaunti yake na hivyo ni tajiri kuliko Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Alikuwa akijibu kauli iliyotolewa na Spika Samuel Sitta ambaye alimuelezea waziri huyo wa zamani wa mambo ya ndani kuwa amefilisika kisiasa na kifedha na ndio maana anahaha kujikwamua kwa kuipigia debe CCM.
Sitta, ambaye ameongoza kipindi cha mwisho cha uspika wake kwa mapambano dhidi ya watu aliowaita maadui wake wa kisiasa, alidiriki kumuelezea Mrema kuwa amefilisika na kwamba huenda anapata fedha kutoka chama hicho tawala.
Sitta alitoa tuhuma hizo nzito baada ya Mrema kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kumtuhumu spika kuwa ana makundi ndani ya Bunge na kwamba anaendelea kuzungumzia sakata la utoaji zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa Richmond Development LLC kwa kuwa mjadala huo ulishafungwa na Bunge.
Jana Mrema alikanusha tuhuma zote hizo na kudai kuwa yeye hajafulia wala hajafilisika kisiasa na kifedha na kwamba hajachanganyikiwa wala kuhongwa na CCM ili akipigie debe na akamtaka Spika Sitta atoe ushahidi wa tuhuma zake.
Pia Mrema alitangaza kuwa atamfikisha mahakamani Sitta kwa madai kuwa amemkashfu na kumvunjia heshima mbele ya jamii na pia atamshtaki kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa kwa kuwa amevunja kanuni za vyama vya siasa kwa kutoa maelezo ya uongo dhidi yake.
"Mimi nilimuonya mheshimiwa spika kwamba aache kuwa na makundi ndani ya Bunge na asiendelee kulalamikia suala la Richmond kwa sababu mjadala huo ulishafungwa na Bunge. Na kama haridhiki yeye pamoja na wenzake wajiondoe CCM kama nilivyofanya mimi mwaka 2005,"alisema Mrema katika mkutano wake na waandishi jana.
"Lakini badala ya kujibu hoja, Mheshimiwa Sitta akaamua kunikashfu na kunitukana mimi kama mtu binafsi, jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za vyama vya siasa zilizopitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa mwaka 2007, Ibara ya 5(d) inayotaka kutotoa maneno yoyote au maandishi ambayo ni ya uongo kuhusu mtu yeyote au chama chochote cha siasa."
Akifafanua kuhusu tuhuma hizo, Mrema alisema kifedha hajafilisika bali yeye ni tajiri kuliko hata Pinda kwa kuwa anamiliki Sh.37.75 milioni kwenye akaunti yake.
Mimi sijafulia. Kufulia kwa lugha ya mitaani ni kufilisika hata kukosa fedha ya Chakula. Namhakikishia mheshimiwa spika kwa kuwa sijafulia kama anavyodai kwani nina uwezo wa kujilisha na familia yangu pamoja na kusomesha watoto wangu na kujitibu ninapoumwa bila ya msaada wa mtu yeyote," alisema Mrema.
"Nimefanya kazi serikalini kwa zaidi ya miaka 30 nikiwa ofisa wa Usalama wa Taifa, mbunge, waziri na baadaye naibu waziri mkuu.
Wakati wote huo nilikuwa najiwekea akiba kutokana na mshahara na marupurupu niliyokuwa nikilipwa. Kufikia jana Machi 5 ninayo akiba ya Sh.37.751,451.79 kwenye akaunti namba 2017800187 ya benki ya NMB, tawi la Bank House.
"Kwa hiyo mimi ni tajiri tena kuliko waziri mkuu ambaye alitangaza mali zake na kusema ana Sh25 milioni kwenye akaunti yake, sasa iweje Sitta aseme eti Mrema amefulia... maana yake ni nini?"
Mrema alikuwa akisema hayo huku akionyesha taarifa yake ya benki inayoeleza kiasi kilichomo na masuala mengine.
Kuhusu kufilisika kisiasa Mrema alisema chama anachokiongoza ni cha nne nchini kati ya vyama 18, na kwamba hata katika uchaguzi wa serikali za mitaa, TLP ilifanya vizuri na ina viongozi katika ngazi zote tangu mitaa, vijiji na vitongoji.
Mrema, ambaye ameshagombea urais kwa tiketi ya NCCR Mageuzi na baadaye TLP kabla ya kutangaza kurudi kugombea ubunge kwenye jimbo lake la zamani la Vunjo, alisema kuwa chama chake kilishinda kwenye vijiji 20 na vitongoji 48 kwenye jimbo la Vunjo katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kuhusu madai kuwa amechanganyikiwa na kuhongwa na CCM ili akipigie debe chama hicho tawala, Mrema alimtaka Spika Sitta atoe ushahidi wa tuhuma hizo kwa kuwa zimemdhalilisha, zimemvunjia heshima na kumpaka matope mbele ya jamii. Alisema atamshtaki mahakamani kwa kumkashifu na kumsingizia mambo ya uwongo.
"Kuchanganyikiwa maana yake ni kutokuwa na akili timamu. Sasa mimi kama ningekuwa sina akili timamu wanachama wa TLP wangenichagua niwe mwenyekiti wao? Namuomba Spika aonyeshe ushahidi wa cheti cha hospitalini kuonyesha kuwa mimi nimechanganyikiwa,"alisema Mrema.
Mrema pia alisema:"Mimi sijahongwa na CCM wala na mtu yeyote. Hizi ni tuhuma mbaya kwangu binafsi, kwa chama changu na kwa CCM. Namtaka atoe ushahidi aonyeshe âpay rollâ mahali ninakosaini huko CCM."
Mrema alisisitiza kuwa CCM ina uwezo wa kushinda uchaguzi bila hata ya kupigiwa debe na yeye wala TLP kudai kuwa imeweza kushinda katika uchaguzi mwaka 1995, 2000 na 2005 bila yeye kuipigia debe.
Alisema Spika Sitta anashindwa kumuelewa kwa kuwa yeye huzungumzia mambo ya kitaifa ambayo yako juu ya vyama vya siasa kama vile mshikamano, amani na utulivu, ambayo hayana chama kwa kuwa amani ikivunjika watu wote wanaathirika bila kujali nani yuko chama gani.
"Vile vile masuala ya Bunge hayahusu chama chochote cha siasa kwani bunge ni la wananchi wote, hivyo ninapomkosoa spika wa Bunge, siingilii mambo ya CCM kama ambavyo anadai," alisema Mrema.
Mrema alisisitiza kuwa yeye hajafilisika kisiasa bali Spika Sitta ndiye amefilisika kisiasa kwa kuwa anafanya siasa makanisani.
"Kwa muda mrefu spika amekuwa akifanya siasa makanisani kama alivyofanya hivi majuzi huko mkoani Ruvuma ambako alitangaza kuwa CCM walitaka kumfukuza uanachama kutokana na msimamo wake katika suala la Richmond. Spika aelewe kuwa nchi hii siyo ya Wakristo peke yao, hivyo kufanya siasa makanisani kunahatarisha mshikamano wa nchi yetu," alisema Mrema.