JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,780
- 6,607
Siku tatu sasa tangu pacha Rehema na Neema waliokuwa wameungana kufanyiwa upasuaji na kutenganishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), mama mzazi wa pacha hao, Amina Amos amesimulia visa na mikasa aliyokumbana nayo baada ya kujifungua pacha hao.
"Niliambiwa nimezaa laana, nimeleta mkosi, kwenye jamii yangu wapo walionitenga, nikawa najiuliza marafiki zangu wamepata watoto lakini mbona hawapo kama wangu?!.. nilijiuliza mno kwa nini mimi?" amefunguka Amina.
Ni mara ya kwanza mama huyo mwenye umri wa miaka 17 kuzungumza na waandishi wa tangu alipofika Muhimbili na hadi pacha wake hao kufanyiwa upasuaji wa ubingwa wa juu ulioandika historia mpya kwa Tanzania Julai mosi, 2022.
"Nimepitia changamoto nyingi lakini sasa hivi nina furaha kwa sababu napata mahitaji ya watoto hapa Muhimbili wamenipa msaada mkubwa na nimelelewa vizuri pamoja na Wanangu.
"Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha wataalamu kufanikisha upasuaji wa pacha wangu. Napenda kushukuru Taifa letu na Muhimbili kwa kuweza kutenganishia pacha wangu salama pamoja na madaktari wote wa ndani na nje ya nchi.
"Nashukuru sana wauguzi wa kitengo cha PIKU (wodi maalum ya kulaza watoto wachanga wenye umri kuanzia miezi 28 hadi miaka 14), wamenilea vema na wanangu na wamenisaidia sana."
Amesema baba wa watoto hao alimtelekeza baada ya kuona watoto wameungana
"Mwanzo mtihani niliokuwa nao ni jinsi gani nitawalea wakiwa wameungana, wametenganishwa sasa nina furaha na nashukuru sana lakini sasa naanza kujiuliza nikitoka hapa itakuwaje?"
Akizungumza, Katibu Mkuu wa Wizata ya Afya, Profesa Abel Makubi aliyefika hospitalini hapo kumjulia hali mama huyo pamoja na pacha wake, kwanza amekemea tabia ya unyanyapaa kwa watu waliopata watoto wenye changamoto kama ilivyo kwa pacha hao.
"Nimewaona pacha wanaendelea vizuri baada ya upasuaji, tuzidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili hali zao zizidi kuimarika zaidi, lakini bado kunaonekana kuna unyanyapaa katika jamii kwa watoto hawa.
"Serikali itaendelea ku-support malezi/makuzi yao kwa kuwa tumeanza nao, lakıni pla natoa rai kwa wadau wengıne waje tushirikiane pamoja kuhakikisha wanapata lishe vizuri, wakue na waendelee na maisha yao," - Profesa Makubi
Pamoja na hayo, Profesa Makubi amewasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwa jopo la wataalamu waliofanikisha upasuaji huo.
"Mh. Rais Samia Suluhu na Mhe Ummy Ally Mwalimu Waziri wa afya, wanatoa pongezi sana kwa watalaamu wetu nchini wakishirikiana na wale wa chuo kikuu cha Bahrain kwa kufanikisha 'operation' kubwa ya upasuaji wa pacha hawa," amewasilisha salamu hizo.
Akizungumza, Mkuu wa Kitengo cha Watoto Muhimbili na Daktari Bingwa wa Upasuaji Watoto, Zaitun Bokhari ameshukuru wamepokea salamu za Rais Samia na Waziri Ummy.
"Tunaishukuru Serikali kwa sababu imefanya kazi kubwa kuwekeza katika miundombinu, imeimarika na leo tumeweza kutanya upasuaji huu.
"Hawa wataalamu wenzetu walipokuja na kuona miundombinu yetu, waliona ipo vizuri na wakasema tunaweza kufanya hapa hapa," amebainisha.
Upasuaji huo ni wa tatu kufanyika nchini na umefanyika kwa mafanikio makubwa na kuandikia Tanzania historia mpya.
Source: Matukionamaisha.blogspot.com
Pia soma >>
Muhimbili yasema upasuaji wa watoto pacha umefanyika kwa mafanikio
Watoto pacha walioungana kufanyiwa upasuaji Muhimbili, leo Julai 1, 2022