Mambo Kumi kuhusu Denzel Trainer hadi kukutana na Doumbia wa Mnyama Simba 🦁..

Mambo Kumi kuhusu Denzel Trainer hadi kukutana na Doumbia wa Mnyama Simba 🦁..

BABU NYAU

JF-Expert Member
Joined
Feb 15, 2025
Posts
1,122
Reaction score
1,257
Baada ya Doumbia kutikisa nyavu zilianza kusambaa video za kiungo huyo akipewa mazoezi na mkufunzi wa mazoezi Godfrey Mkinga maarufu kama Denzel..

Dar es Salaam. Wiki hii imekuwa tamu kwa mashabiki wa soka na burudani baada ya mshambuliaji wa Simba SC 🦁, Ibrahim Doumbia, Oktoba 21, 2026 kuanza kujibu matarajio ya mashabiki wa timu hiyo kwa kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya de Agosto ya Guinea ya Ikweta, kwenye mchezo wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika..

32d6c421e5714a0896b4ee07dcd8c7a7.jpg

Doumbia alifunga mabao hayo ikiwa ni mara yake ya kwanza kutikisa nyavu tangu ajiunge na Simba katika dirisha kubwa la usajili, akivunja ukimya uliokuwa ukizunguka kiwango chake tangu alipowasili Msimbazi..

Katika mchezo huo wa hatua ya kuwania kufuzu hatua ya makundi, Simba ilipata mabao mengine kupitia Mpanzu, Toure, Keletso na Chilambo. Tuachane na soka tujadili hili..

6f75e11f94cb469dbac91f7c4820681f.jpg

Baada ya Doumbia kutikisa nyavu zilianza kusambaa video za kiungo huyo akipewa mazoezi na mkufunzi wa mazoezi Godfrey Mkinga maarufu kama Denzel..

Ingawa hatuwezi kusema Denzel ndiyo sababu pekee ya Doumbia kutikisa nyuvu, lakini kwa hatua hiyo imefanya mkufunzi huyo kumwagiwa sifa hasa ikiwa wachezaji wawili waliotikisa nyavu wamepita katika mikono yake kula tizi. Ifahamu vizuri safari ya Denzel..

1. Alitoka Songea na kuja kutafuta maisha Dar-es-Salaam 2008..

Denzel Trainer, alihamia Dar es Salaam mwaka 2008 baada ya kuhitimu kidato cha nne, akiwa na ndoto ya kwenda Afrika Kusini kutafuta maisha. Hata hivyo, mipango hiyo haikutimia kama alivyotarajia, kwani mtu aliyekuwa amemwahidi safari hiyo hakuwa na uwezo wa kumpeleka. Badala yake, Denzel alipokelewa na rafiki wa karibu wa baba yake na kuishi katika familia yake..

2. Alipitia msoto balaa..

Kabla ya kuwa mkufunzi wa mazoezi anayehudumia watu maarufu, Denzel alipitia hali ngumu ya maisha jijini Dar es Salaam. Alifanya kazi mbalimbali, zikiwemo kufyatua matofali, kufanya usafi na kuuza mkaa, ili kupata fedha za kujikimu na kumsaidia mama yake aliyekuwa mkoani Ruvuma..

Wakati mwingine alitembea kutoka Mburahati hadi Kimara kwenda kufyatua matofali kwa malipo ya Sh3,000 kwa siku.. 😂

3. Alipata mtu wa kumsaidia kupata kazi na kusoma IFM..

Katika harakati zake za kutafuta kazi, Denzel alikutana na mzee mmoja aliyemweleza hali ngumu aliyokuwa akiishi na kumwomba amsaidie kupata kazi yoyote..

Aliendelea kuwasiliana na mzee huyo hadi alipopewa nafasi ya kusaidia kuhamisha mizigo na kufanya usafi katika ofisi iliyokuwa ikihama kutoka Sinza kwenda Kinondoni..

Bidii yake iliwavutia waliomzunguka na hatimaye akapata ajira ya kufanya usafi kwa mshahara wa Sh50,000 kwa mwezi. Baadaye, mzee huyo alijitolea kumlipia masomo katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), ambako Denzel alisoma ngazi ya cheti ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (IT), kisha akaendelea na diploma ya uhasibu na benki..

4. Jina lake limetokana na muigizaji wa Marekani..

Jina la Denzel alilokuja kulitumia katika maisha yake lilitokana na kuvutiwa kwake na mwigizaji maarufu wa Marekani, Denzel Washington. Akiwa mwanafunzi wa IFM, alianza kujiita jina hilo, ambalo baadaye lilizidi kujulikana kadiri alivyopiga hatua katika kazi yake..

5. Alianza mazoezi bila ujuzi, baadae akawa mkufunzi..

Denzel alianza kwenda gym ya Kisutu akiwa mwanafunzi wa IFM, akifuatana na marafiki zake waliokuwa wakifanya mazoezi. Wakati huo hakujua mbinu za mazoezi, hivyo alikuwa akiiga kile ambacho wenzake walikuwa wakifanya..

Baadaye, rafiki yake alimshauri ajifunze ualimu wa mazoezi kwa sababu kulikuwa na fursa ya kuwafundisha watu wenye mahitaji mbalimbali. Rafiki huyo alisafiri naye hadi Kenya, ambako alipata mafunzo ya wiki mbili kutoka kwa mkufunzi aliyebobea. Aliporejea Tanzania, alianza kuwafundisha watu katika gym mbalimbali na baadaye akaajiriwa Dar Gym..

6. Alisafiri hadi Sauzi ili ampate Ali Kiba..

Moja ya hatua zilizobadili maisha ya Denzel ni namna alivyopata nafasi ya kuwa mkufunzi wa mwanamuziki Ali Kiba. Akiwa Dar Gym, alikutana na Aidan, meneja wa Alikiba, ambaye alianza kumfundisha mazoezi na hatimaye wakawa marafiki..

c0ff48da19f34fc606fe2f7b898048ba.jpg

Denzel alitamani kumfikia Alikiba ili amfundishe mazoezi, lakini ilimchukua muda kupata nafasi hiyo. Hatimaye, Aidan alimjulisha kuwa Alikiba angeenda Afrika Kusini kurekodi video ya muziki, hivyo Denzel aliamua kumfuata hukohuko ndipo akapata nafasi..

7. Kupitia Ali Kiba alipata nafasi ya kuwafundisha watu maarufu..

Baada ya kuwa mkufunzi wa Alikiba, Denzel alipata fursa nyingine za kuwafundisha watu wenye majina makubwa. Miongoni mwao ni Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete na familia yake! Ommy Dimpoz! Kajala Masanja na Hassan Joho, gavana wa zamani wa Mombasa nchini Kenya. Kwenye soka nako kawakamata wengi ikiwemo Ellie Mpanzu, Doumbia, Clatous Chama na wengine wengi..

8. Alivyopata dili kwa Kikwete..

Denzel alitamani kwa muda mrefu kumfikia Mama Salma Kikwete ili kumshukuru kwa msaada aliowahi kumpa alipokuwa na shida. Akiwa mwanafunzi, alipopata fedha za kujikimu kwa kufanya kazi makaburini Kisutu, Mama Salma alimpa Sh40,000 wakati mama yake alikuwa mgonjwa na alihitaji dawa zilizogharimu Sh20,000..

44a5ec4401b1c76199c81014e54353f8.jpg

Baadaye, kupitia ukaribu wake na Alikiba, alipata nafasi ya kuambatana naye kwenda nyumbani kwa Rais mstaafu Kikwete. Alitumia fursa hiyo kumshukuru Mama Salma na pia kumweleza Kikwete umuhimu wa mazoezi kwa afya, kisha akaomba kuwa mkufunzi wake. Kikwete alikubali ombi hilo, na Denzel akapata nafasi hiyo..

9. Anajulikana kwa kuwafundisha wazee na wagonjwa..

Tofauti na wakufunzi wengi wanaojikita zaidi katika mazoezi ya kawaida ya gym, Denzel amejipatia umaarufu pia kwa kuwahudumia wazee na watu wenye changamoto za kiafya. Ratiba yake ya kazi ni yenye shughuli nyingi, akianza kumfundisha mwanafunzi wa kwanza saa 10:40 alfajiri na kuhitimisha kwa mwanafunzi wa mwisho saa nne usiku..

b36eb04684ce8ac5c36a91bda22148e4.jpg

10. Siri ya mafanikio..

Denzel anazingatia katika kazi yake nidhamu, kwa sababu anaamini mwanafunzi hawezi kufikia malengo yake ikiwa hatakuwa tayari kufuata maelekezo ya mwalimu. Hata anapowafundisha watu wenye majina makubwa au wenye uwezo mkubwa kifedha, huwaweka katika nafasi ya wanafunzi wakati wa mazoezi, huku yeye akisimamia mafunzo kama mwalimu..
 
Back
Top Bottom