RAIS SAMIA ANASTAHILI HESHIMA NA PONGEZI .
Na. Amon Nguma .
Tarehe 18 April 2024 Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania ametunukiwa na Chuo Kikuu cha Ankara- Uturuki Shahada Heshima ya Udaktari (Honoris Causa) ya Uchumi, wakitambua mchango na jitihada za Rais Samia katika kujenga Taifa na kuletea wananchi wa Tanzania maendeleo ya Kiuchumi ,tukio hilo limefanyika Ankara katika ziara ya Rais kufuatia mualiko wa Rais wa Uturuki.
Ikumbukwe hii ni Degree ya Nne ya Heshima Rais anatunukiwa ikitanguliwa na Shahada ya Juu ya Heshima ya Udaktari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( Doctor of Letters Honoris Causa), Shahada ya Heshima ya Uzamivu(PhD) ya Usimamizi wa Masoko na Utalii kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar(SUZA) pamoja na Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa( Doctorate Honoris Causa) ya Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha Nchini India Oktoba 10, 2023.
Zote hizi ni udhihirisho wa kazi kubwa na nzuri aliyofanya Rais Samia katika kipindi chake ya kupambana na changamoto, kutafuta fursa na kuleta ustawi kwa jamii anayoingoza, kuisogeza Tanzania katika hali bora zaidi ya iliyokuwepo awali .
Je ni nani asiyeona jitihada za Rais Samia katika utunzaji wa Mazingira pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabia ya Nchi? Rais ameongoza operesheni za utunzaji Mazingira ikiwemo upandaji miti, uzinduzi na upelekaji wa Nishati safi ya Kupikia ambayo ina dhamira ya kuwalinda Kina Mama na athari za Nishati hatari na chafuzi kwa mazingira pamoja na miradi ya umwagiliaji kwa ajili ya kilimo.Dhamira ni njema na jitihada zinaonekana.
Je, ni nani asiyeona jitihada za Rais Samia katika Sekta ya Elimu? Ni katika kipindi kifupi cha Uongozi wake tumeshuhudia ujenzi wa madarasa katika kiwango ambacho Nchi yetu haijapata kushuhudia ,ujenzi wa Madarasa zaidi ya 20,000 ujenzi wa Shule za Wasichana za Sayansi katika Kila Mkoa ,uboreshaji wa Mitaala ,Elimu bila Ada , Uzinduzi wa Mikopo ya Elimu kwa Vyuo vya kati na kuongeza Mikopo Elimu ya Juu pamoja na utoaji wa Mafunzo kwa Watumishi na Wananchi wote ikiwemo Wakulima, Wafugali na Wavuvi ili kuwaongezea uwezo.Kiongozi yeyote anayefanya Elimu kuwa kipaumbele amezingatia utu ( humanity) na kesho ya Jamii anayoiongoza .
Je ni nani asiyeona ama kutambua kazi na mapinduzi makubwa katika sekta ya Afya? Katika Historia ya Taifa letu hakuna kipindi ambacho Taifa ketu limeshuhudia mapinduzi makubwa katika sekta ya Afya kama kipindi cha Rais Samia Suluhu Hassan ni katika kipindi hiki ambacho Vyumba vya ICU vimeongezeka na vitanda kuongezeka kutoka 200 na kidogo mpaka zaidi ya vitanda 1000 vya ICU, Mitambo ya MRI na CT -Scan iliyokuwa Muhimbili sasa imefikishwa katika kila hospitali ya Rufaa na Mikoa, uzinduzi wa mitambo ya kuzalisha Hewa Tiba ( Oksijeni) katika Hospitali za kanda ,kusomesha na kuendeleza Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi ndani na Nje ya Nchi sanjari na huduma za kibingwa katika Hospitali za kanda na Mikoa pamoja na Taifa kwa zile ambazo hazikuwepo awali .
Haihitaji Darubini kuona Mapinduzi makubwa anayofanya katika Sekta ya Kilimo ,Mifugo na Uvuvi. Ni katika kipindi kifupi cha uongozi wake ambapo Bajeti kwa sekta ya Kilimo ilipanda kutoka Bilioni 290 mpaka zaidi ya Bilioni 750 na sasa inaelekea zaidi ya Trilioni ,ujenzi wa Skimu za Umwagiliaji pamoja na uchimbaji wa Visima zaidi ya 67,000 ,ugawaji wa Ardhi kwa vijana pamoja na uwezeshaji mitaji kwa wakulima ( BBT Financing) yote haya kati ya mengi ni udhihirisho kuwa Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan ni mwanamapinduzi wa kweli wa kiuchumi .
Je, ni nani asiyeona ukuaji wa kasi wa sekta ya Utalii ? Kama hujajionea kwa Macho fanya tafiti au ulizia kwa maeneo ya utalii namna ambavyo hali imeimarika na kustawi kwa muda mfupi kutokana na jitihada za utangazaji wa Sekta ya Utalii na Rais Samia kuiweka sekta ya Utalii kuwa moja ya kipaumbele chake na kuzungumzia vivutio vyetu kila anapopata jukwaa au nafasi .Je, kwa hali kama hii ni nani asiyeona ? Je ni nani asiyeona fursa zitokanazo na utalii kwa Watanzania na ongezeko la mapato pamoja na sekta ya utalii kuwa kinara katika kuingiza fedha za kigeni ?
Je, ni nani asiyeona jitihada za Rais Samia katika kuinua vipaji na maendeleo ya sekta ya Michezo Sanaa na Utamaduni pamoja na ujenzi wa Miundombinu ya Michezo ikiwemo Viwanja ? Wasanii kupewa Mikopo ili kujiinua kiuchumi pamoja na kuinua kazi zao za sanaa .
Je, ni nani asiyeona ama kushuhudia namna ambavyo miradi ya kimkakati yenye mchango mkubwa katika uchumi kama mradi wa umeme STIGLERS ikikamilika na mengine ya SGR ikienda kwa kasi ? Ni nani asiyeona uboreshaji wa viwanja vya ndege pamoja na ununuzi wa ndege za abiria na mizigo ?
Inawezekana mengine yasionekane kwa urahisi vipi miradi ya maji ambayo inachemka nchi nzima ? Kuweka Rekodi sawa hakuna kipindi ambacho Wizara ya Maji ilipata bajeti kubwa kama kipindi cha Samia na katika historia ya Taifa letu hakuna kipindi ambacho Nchi yetu inatekeleza na imetekeleza miradi mingi ya maji kwa kasi na kwa mpigo kama kipindi hiki .Kiongozi anayezingatia upatikanaji wa Maji safi na salama anajali utu ,afya na uhai wa jamii anayoiongoza.
Kwa hali ya kawaida ni nani asiyeona ama kufahamu jitihada za Rais Samia katika Diplomasia ya Uchumi ? Ni katika kipindi hiki ambacho tumeshuhudia uwekezaji katika viwanda pamoja na usajili wa miradi iliyotoa ajira nyingi kwa Watanzania ,lakini ni kipindi hiki ambayo Wakulima wa Mbaazi walifanya sherehe kwa kupata soko lenye tija na kutengeneza faida pamoja na wa mazao mengine .Yote haya na mengine mengi ni udhihirisho kuwa Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan anatafuta na kutengeneza tija kwa jamii anayoiongoza .
Uungwana ni Vitendo na Rais Samia amedhihirisha ,kupongeza ni uungwana pongezi kwa Mhe. Rais ,anastahili Shahada za heshima nyingi zaidi na pongezi kwa kazi anayoifanya , Rais Samia anaisogeza jamii ya Watanzania katika hali bora zaidi ya iliyokuwepo awali na matumaini ni makubwa zaidi kwa siku za usoni .
Kazi Iendelee
Amon Nguma
0620615659