Sikujua ni kwanini siku ile alipoapishwa kuwa Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano Samia Suluhu Hassana aliamua kuvaa rangi nyekundu kama sehemu ya mavazi yake. Ni baadae nikajulishwa kuwa ile rangi nyekundu ni ya mamlaka, ni ya kiongozi wa juu wa Taifa.
Amekuwa rais wetu kwa mwaka mmoja na miezi miwili, ni kipindi tosha kabisa cha kujipambanua urais wake unasimamia katika sera zipi. Na ameweza kujitofautisha na mtangulizi wake hayati JPM. Amefanana na jinsia yake kwa namna anavyoongoza Tanzania.
Kwa maana ya usikivu, ukarimu, kutojikweza na ile lugha ya kukaribisha watu, wawe ni wa humu humu ndani au wale wa jamii za kimataifa. Kwenda kwake huko nje na kujitambulisha kumeipa dunia picha halisi ya kiongozi tuliyenaye, kwamba hajitengi na mataifa mengine na ile mitazamo ya kiujumla ya kidunia.
Amekuwa ni rais mkweli siku zote. Nyeupe ataiita nyeupe, nyeusi anaiita nyeusi. Wapo walioozoea kuona kiongozi wa juu wa nchi akitumia uongo kidiplomasia. Uchumi wetu umetetereka kwa sababu ya COVID19, amekuwa mkweli kwamba lipo tatizo. Watu kwa wingi walikuwa wakifa, akawa mkweli kwamba tunapoteza nguvu kazi yetu kwa sababu ya maradhi haya. Uchumi wa nchi uliyumba na ukadorora na ni kweli hiyo ndio hali halisi. Anaweza asieleweka kwa wanasiasa waliozoea kuambiwa uongo wa kidiplomasia wa siku zote lakini ni hali inayoliponya taifa. Alipoongeza kodi za simu watu walilalamika sana, akasema ni makusanyo ya muhimu kama kweli tunataka kwenda sambamba na ahadi za mwaka 2025.
Amekuwa mkweli siku zote, na anajitahidi kuujenga hoja ukweli huo ili watu waelewe malengo haswa ya kile kinachoamuliwa. Angeweza akatupelekesha puta kijeshi na hakuna ambaye angekuja kulalamika mbele ya waandishi wa habari. Anatambua upana wa demokrasia hivyo inakuwa rahisi kwake kuzijibu kila tuhuma zinazoelekezwa serikalini kwa uwazi. Hiyo ni faida ya kuwa karibu na mitandao ya habari siku zote, kujua nini kinaendelea midomoni mwa watu na kukifanyia kazi, ukichunguza kwa undani ni tabia ya kiungwana kuliko tabia ya uswahili kama wanavyosema baadhi ya watanzania.
Neno la Mungu linasema Ukweli utatuweka huru. Anapokwenda huko nje, huku ndani anajikuta akidhihakiwa, kwamba anaiuza nchi, kwamba ni kibaraka wa mataifa ya magharibi, kwamba anajikomba kwa Marekani na wakubwa wengine. Yanasemwa mengi na wale waumini kindakindaki wa sera za hayati JPM. Walitegemea kuwa angeiga kila kitu kutoka kwake. Wanapoona anajitegemea kifalsafa ni lazima waumie na kusema kuwa remote ya kinachofanyika ikulu ipo Chalinze.
Pesa alizokwenda kuzitafuta huko nje, ndio hizi zinazoongeza bajeti ya kilimo, ndio hizi zinazoimalizia miradi ya awamu iliyopita mmoja baada ya mwingine. Ndio hizi zinazoongeza mishahara, na hapo ukichanganya na makusanyo ya kodi ya ndani. Amerudisha mahusiano mema kimataifa akiachana na kiburi na majivuno mengi ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa hayaonyeshi kwamba nchi yetu inao msimamo wake, bali walikuwa wakitushangaa tu wakishindwa kutuelewa. Humility is the best weapon, linapokuja suala la nchi yetu kuingiliana na mataifa mengine.
Ninaliona suala moja na ni la kutazamwa kwa kina kama anataka kukubalika zaidi ya anavyokubalika sasa. Wapambe wapo wa aina nyingi, wengine wanamuita Mama, wengine wanakuja na majina mengine na namna nyingine za kumpamba. Ni rais wa jinsi ya kike, anao udhaifu ule ule wa watu wa jinsia hiyo. Anaonekana kuuingia huu mtego wa kupambwa.
Siku zote binadamu anachojaribu kukionyesha machoni pake sicho kilichopo rohoni mwake, watu wanaishi wakiwa na nia mbili siku zote. Awe mwangalifu na upambe wa zile risala au hotuba kabla hajasimama na kuhutubia watu katika matukio rasmi ya kiserikali. Asimamie pale pale katika utendaji wenye kujishusha na unaoamini katika ukweli na usio na majivuno yanayopofusha nafsi za watu wakajikuta wakidondokea mtaroni na kupotea kabisa.
Wapambe na mitandao yao, ni wanasiasa kama wengine wowote wale. Awe nao makini ili wasipunguze dhamira aliyonayo moyoni mwake kwa watanzania.