NINA HAKI YA KUTOA MAONI KWA DR.JOHN POMBE MAGUFULI RAIS WA JMT AWAMU YA TANO.
Ninaomba kutoa angalizo kwa Mh.Dr.John Pombe Magufuli katika kipindi cha miaka 5 atakachokuwa akiongoza JMT.
1. Ni vyema akaepuka watu wachonganishi watakaomchonganisha na Watendaji wake kwa manufaa ya watu hao.Kwa kutumia vyombo vya dola na utashi wake kama Rais ni vyema akachuja kila taarifa atakayopewa kabla ya kuchukua maamuzi stahiki.Kama ilivyokuwa wakati wa Kampeni,watu wengi watajisogeza kwake kwa njia ya kumpa ushauri katika mambo mbalimbali.
2. Ni vyema akatafakari sana katika uteuzi wa Watendaji atakao ufanya maana hao ndio watakuwa wafuatiliaji wa shughuli zake za kila siku.Kama kuna mahalia mbapo JPM anapaswa kuwa makini ni katika teuzi mbalimbali atakazozifanya.Asifanye uteuzi wenye nia ya kulipa fadhila.Bali weledi na uchapakazi pamoja na uaminifu katika utendaji wa kazi.
3. Ni vyema JPM akashughulikia kwa moyo wake wote suala la Zanzibar kabla hali ya amani haijavurugika ZAIDI.Mshindi halali atangazwe na kazi iendelee.Imani kwamba CUF watavunja Muungano si ya kujenga na Imani kwamba CCM pekee ndiyo yenye kuleta amani na utulivu si hoja makini na jadidi.
4. Ni vyema akaweka mikakati thabiti ya kushughulikia ahadi lukuki alizoziahidi ili imani ya Wananchi kwake na kwa Chama chake irudi na Maisha ya Wananchi yawe bora zaidi.Watangilizi wake hawakutimiza ahadi zao lukuki walizotoa kwa mbwembwe majukwaani.
5. Ni vyema akaepuka kuongozwa na watangulizi wake ambao kwa nguvu kubwa walimbeba na kumweka madarakani.Akumbuke yeye ndiye rais wa JMT na watangulizi wake walikwisha maliza vipindi vyao.
6. Ni vyema akafanya kazi na makundi yote hususani vyama pinzani na wanaharakati wapenda maendeleo.Kushinda uchaguzi sio kushinda kila kitu.Hata walioshindwa wanaweza kupewa ushirikiano kwa ajli ya kuleta maendeleo yanayohitajika.
7. Ni vyema harakati za kufufua Viwanda vilivyokuwa vimebinafsishwa na kutelekezwa ama kubadilishwa kuwa magodauni ziendane na kuboresha upatikanaji wa uhakika wa nishati ya umeme pamoja na kuondoa Michango lukuki inayoitwa ya kisheria katika Viwanda hivyo kama OSHA,FIRE RESCUE,NEMC,VIPIMO,MAJI,TBS,LESENI,CESS ZA VIJIJI,MITAA NA WILAYA,NK.Hizi zote huwa ni kero kwa Wenye viwanda.Pia ni vyema soko la ndani la bidhaa husika lilindwe kwa ajili ya kuhakikisha bidhaa hizo zinauzwa na tija kupatikana.
8. Ni vyema akaondoa kabisa kodi katika pembejeo za kilimo kama matrekta, mbolea, powertiller, mbegu bora n.k.Jitihada za kuboresha sekta ya Kilimo ziwe za dhati na zenye tija na wala sio blah blah.
9. Ni vyema suala la Bunge kuwa la mipasho badala ya chombo cha kutunga sheria na kujadili matatizo ya wananchi likemewe kwa sauti kuu na yeye awe mfano bora wa kulisimamia hilo.Jambo baya katika hotuba yake alisisitiza hilo na papo hapo yeye mwenyewe akatoa mipasho kwa kuwaita wapinzani ?watoto?
10. Ajira kwa vijana ni bomu hatari.Ni lazima tatizo hili litatuliwe kwa jitihada kubwa kwa kufufua viwanda na kuimarisha kilimo sambamba na kukomesha ajira za upendeleo.
Haya ni maoni yangu binafsi, hata hivyo michango kwa wengine ni muhimu kwa nia ya kutupeleka katika maisha bora zaidi.Aidha kutofautiana mitizamo ni chanzo cha Maarifa mengine.