Ni soko ambalo kipindi cha msimu linahusisha wafanyabiashara kutoka mataifa mengine yakiwemo Kenya, Uganda Malawi kuja kufanyabiashara kwenye soko hili.
Jambo la kusikitisha ni kuwa mazingira ya soko hili ni duni, hayavutii, soko halina hadhi ile ya 'kimataifa' kama lijulikanavyo.
Kipindi hiki cha mvua hali ni mbaya, ukifika eneo la tukio unakutana na matope, dampo la soko lilipo pembeni hapo ni chafu. Wafanyabiashara wa soko hilo wako katika mazingira magumu.
Wakati wa kiangazi Wafanyabiashara wanateseka juani wakati kipindi cha masika wanalazimika kufunika vitunguu na maturubai ili visinyeshewe.
Wafanyabiashara hao hulipia pesa ya taa Tsh. 1,500 kila wiki, kulipia taa zinazowaka usiku kwa ajili ya ulinzi wa vitunguu lakini sio taa zote zinazowaka, kati ya taa 6 zilizopo tatu zinawaka na tatu haziwaki.
Vilevile wafanyabiashara hao hulazimika kulipia ushuru wa kila gunia moja wanalonunua kwa Tsh 2,000/-. Mapato ya pesa hizo yanafanya kazi gani?
Tangu Serikali itoe ahadi ya kujenga soko imeshakuwa hadithi.
Soko hili lina jina kubwa na linaingizia Serikali pesa nyingi hasa msimu wa mavuno ya vitunguu ukifika lakini sasa ni wakati Serikali nayo iipe hadhi inayostahili kwa kufanya maboresho.
Ikiwa soko litajengwa uhifadhi wa vitunguu utakuwa mzuri, Wafanyabiashara wataondokana na hatari ya kuharibika kwa bidhaa hiyo.
Mbali na hapo hali ilivyo sio salama kwa afya, kumekuwa na taarifa kuwa kuna watu wanaokota vitunguu eneo hilo na kwenda kuuza sehemu nyingine.