Kombe hili halikuwa kipaumbele cha Simba kwa dalili na kigezo gani? Ya Mwenyekiti wa Bodi kujiuzulu baada ya kulikosa? Ya kocha kupeleka timu kamili, hasa baada ya kuingia nusu fainali? Ya kutomjumuisha Manula, ambaye kwa vyovyote asingekuwa sawa kisaikolojia baada ya ‘kuangushiwa jumba bovu‘ kwa matokeo ya 2-2 dhidi ya Yanga? Ya kutotaka kulipiza kisasi kwa Azam iliyowafunga kwenye fainali ya mwaka jana? Ya kauli za viongozi na washabiki kwamba timu imeifuata Yanga Zanzibar ili kujua ile Sare ya 2-2 imepatikanaje? Ya kuwa Kishingo ni kocha mjinga kiasi cha kutothamini nafasi ya kutwaa taji lake la kwanza tangu apewe timu? Ya viongozi na washabiki wa Simba kuhimizana kuja kwa wingi kwenye fainali, wakafanya hivyo na wakashangilia kwa nguvu zote? Ya wachambuzi wa michezo (mf. Sport Arena) kwamba Yanga ilifanya utoto kudhani imemaliza mechi ya nusu fainali baada ya kuiongoza Mtibwa na pia kupeleka wachezaji wengi wasiopata nafasi ya kucheza, tofauti na wenzao Simba? Ya vyombo vya habari vilivyotabiri kwamba rekodi zinaibeba Simba kwenye fainali huku Simba wenyewe wakifurahi? Ya viongozi wa Simba walioanza‘Maandalizi‘ ya mechi ya Mtibwa tangu usiku wa Januari 12 kwa kupewa fursa ya kuingia kiwanjani na ‘kufanya yao’? Kipi kitamshawishi mwenye akili timamu kwamba Simba ilidharau Kombe la Mapinduzi?