Wizara ya Ardhi
Govt Institution
- May 14, 2024
- 306
- 165
MOSHI, KILIMANJARO
Mkoa wa Kilimanjaro umejiunga na mikoa mingine inayotoa huduma za ardhi kwa wananchi kwa njia ya kidijiti kupitia mfumo wa e-Ardhi ambao unarahisisha na kuharakisha huduma za sekta ya ardhi nchini.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta hiyo mkoani humo, Afisa TEHAMA na Mkufunzi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Christopher William Kyando, alibainisha kuwa mabadiliko hayo yanalenga kuondoa urasimu na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.
Bw. Kyando alisema kuwa kimsingi Mkoa wa Kilimanjaro umeingia kwenye orodha ya mikoa ambayo inatumia mfumo wa e-Ardhi kutoa huduma kwa wananchi.
Mfumo huo unatumiwa na idara zote kuu za sekta ya ardhi ikiwemo Mipango Miji, Upimaji, Ramani, na Uthamini chini ya dirisha moja la mtandao kupitia kiunganishi cha (e-ardhi.lands.go.tz) ambapo mwananchi anaweza kuomba huduma akiwa mahali popote, kufuatilia hatua za ombi lake, kujikadiria kodi ya pango la ardhi, pamoja na kupata taarifa za huduma aliyoomba kupitia mfumo huo.
Hatua hiyo inaleta tija kwa Serikali kwa kuwa inatokomeza migogoro kwa kuzuia usajili wa maombi mapya kwenye viwanja ambavyo tayari vilimilikishwa awali.
Bw. Kyando alieleza kuwa Mfumo huo unamruhusu mwananchi kufanya maombi na kufuatilia hatua zote akiwa popote kule alipo, huku ukipunguza muda wa utoaji huduma na kuzuia maombi mapya kwenye viwanja vilivyokwisha pata wamiliki.
Kwa upande wa usimamizi, e-Ardhi umeunganishwa moja kwa moja na Mfumo wa Malipo wa Serikali (GePG) ili kurahisisha upatikanaji wa namba za malipo (Control Numbers) na kudhibiti uvujaji wa mapato ya Serikali.
Aidha, mfumo unawapa viongozi uwezo wa kufuatilia utendaji kazi wa kila mtumishi na kuhamisha miamala iliyokwama ili kuzuia ucheleweshaji wa huduma na mfumo huo ni msaada mkubwa kwa kuwa unarahisisha kukusanya maduhuli ya Serikali.