Wakuu, habari Kuna sehemu nimepitia nikaona kuwa John okelo ndiye rais wa kwanza wa zanzibar, wakati tunajua kuwa ni Karume, mwenye kujua hili atusaidie,wakuu
USIKU wa Jumamosi ya kuamkia Januari 11-12 mwaka 1964, kulitokea mapinduzi yaliyouondoa madarakani utawala wa Kisultani katika visiwa vya Zanzibar.
Mapinduzi ya Zanzibar ni miongoni mwa mlolongo wa mambo yaliyosababisha maasi ya Jeshi la Tanganyika yaliyofanyika juma moja tu baada ya Mapinduzi hayo.
Maasi ya Tanganyika, ambayo yalianzia kwenye Kambi ya Jeshi ya Colito (Sasa Lugalo) usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili ya Januari 19, 1964. Matukio hayo mawili yaliyofuatana.Mapinduzi ya Zanzibar na maasi ya kijeshi ya Tanganyika yalitoa mchango mkubwa kwa Tanganyika kuungana na Zanzibar kiasi cha siku 100 baadaye.
Hata hivyo, historia rasmi ya Tanzania haionyeshi wazi ni watu gani hasa waliohusika katika mapinduzi hayo na ni namna gani yalitokea. Hata ile sehemu ya historia inayozungumzia mapinduzi ya Zanzibar, haimtaji mtu anayeitwa John Gideon Okello, ambaye anatajwa katika kumbukumbu nyingine kama mmoja wa watu muhimu walioshiriki kuuondoa utawala wa kisultani.
Baadhi ya machapisho yanaonyesha kuwa mwaka 1959, ikiwa ni miaka minne kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar, jamii ya wafanyakazi kutoka nchi za Uganda, Kenya, Tanganyika, Rwanda, Burundi, Malawi na Msumbiji waliokuwa visiwa vya Unguja na Pemba waliungana na John Okello, mzaliwa na raia wa Uganda ambaye baadaye alitokea kupata sifa kubwa maeneo kadhaa ya dunia kama ‘kiongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar’, kwa mujibu wa Encyclopedia of the Developing World, Volume 3.
Lakini sifa yake ilidumu kwa kipindi kifupi tu, kisha ikafifia, ikafutika, halafu ikasahauliwa kabisa.
Taarifa za kihistoria
Ingawa kumbukumbu za kihistoria ya Tanzania hazijadokeza mambo mengi juu ya watu hasa waliohusika katika mapinduzi, uchunguzi, udadisi na uchanganuzi wa marejeo mengine mengi ya ndani na nje ya Tanzania unaonyesha hali tofauti na jinsi historia yenyewe inavyosema.
Baadhi ya wanahistoria wanadai kuwa Okello alikuwa mchonga matofali na wala hakushiriki katika mapinduzi hayo. Lakini inajulikana kuwa alikuwa mmoja wa walioshiriki na sauti yake ndiyo iliyotangaza kwamba mapinduzi hayo yamefanikiwa.
Katika kulitetea hilo, baadhi wanasema baada ya mapinduzi kufanikiwa, Okello aliitwa ili atangaze kuwa mapinduzi yamefanikiwa kutokana na sauti yake ya mamlaka tofauti na Wazanzibari.
Katika picha ya pamoja waliyopiga wanamapinduzi, Okello anaonekana amekaa mkao wa kiongozi mbele ya wengine, akiwa amezungukwa na wanachama wa Baraza la Mapinduzi.
Kati ya wote hao ni yeye peke yake anaonekana tofauti, akiwa amevalia nguo ama za kijeshi au za polisi na kofia yake. Wengine wote wamevalia kiraia. Ni watu watatu tu walikalia viti mbele ya wengine.
Katika picha hiyo, kulia kwa Okello amekaa Ramadhani Haji na kushoto kwake ni Seif Bakari. Nyuma yake wamesimama watu wengine; Khamisi Daruwesh, Said Idd Bavuai, Abdallah Said Natepe, Pili Khamisi na Hafidh Suleiman. Kati ya wote hao walioko katika picha ya pamoja, ni Okello peke yake ambaye kweli kweli anaonekana kuwa mwanajeshi au polisi.
Uhusika wa Okello kwenye mapinduzi
Kuhusika kwa Okello katika mapinduzi ya Zanzibar kunazungumziwa na ripoti tofauti za magazeti. Gazeti la serikali ya Tanganyika la Tanganyika Standard la Januari 13, 1964, liliandika katika ukurasa wake wa mbele kuwa “wapigania uhuru waliokuwa na silaha wametwaa kisiwa cha Zanzibar. Wamekamata majengo yote muhimu ya Serikali kwa muda usiozidi saa 24. Usiku kiongozi wa mapinduzi alitangaza muundo wa Serikali mpya ya ‘Jamhuri ya Zanzibar na Pemba’
Sheikh Karume akiwa Rais na Kassim Hanga kama Waziri Mkuu”.
Watu hawa waliotangazwa kuwa viongozi wapya; Karume, Hanga na wengine, hawakuwa Unguja wakati mtangazaji huyo akitaja vyeo vyao. Walikuwa wamekimbilia Dar es Salaam kujificha.
Gazeti hilo linasema kuwa mtangazaji huyo ni “kiongozi wa mapinduzi” na kwamba ndiye “alitangaza muundo wa Serikali mpya ya Jamhuri ya Zanzibar na Pemba.”
Habari ya gazeti hilo inaongeza kuwa hata Abdulrahman Mohamed Babu mwenyewe hakuamini kama naye alikuwa amejumuishwa katika Serikali mpya.
Walioshuhudia na waliosikia jinsi yalivyofanyika, hawakuamini kama kweli kiongozi wa mapinduzi hayo alikuwa wa kawaida.
Maswali mengi kumhusu Okello kuongoza mapinduzi hayo yalianza kuulizwa. Wengine walidhani kuwa Mganda huyo aliwahi kupata mafunzo ya kijeshi nchini China au Cuba.
Maswali na uvumi wa aina hiyo ulisambaa sana kila kona kiasi cha kulisukuma gazeti Tanganyika Standard kwenda kumuuliza maswali hayo. Baadaye gazeti hilo liliripoti jinsi alivyotamba kuhusika kuandaa mapinduzi hayo.
“Field Marshal John Okello leo amesema yeye ni mtu thabiti wa mapinduzi ya Zanzibar na ni yeye aliyemteua Sheikh Abeid Karume kuwa Rais. Kiongozi huyo wa maasi mwenye umri wa miaka 27, ambaye anadai aliwahi kutafsiri ndoto za kundi la (wapiganaji wa) Mau Mau la Kenya, amesema anachoitakia Zanzibar ni demokrasia na uhuru,” liliandika gazeti hilo.
“Field Marshal amefanya mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari katika ofisi za kurushia matangazo ya redio ambazo zilikuwa zimechukuliwa kama makao makuu mapya ya serikali.
Rundo la bastola aina ya ‘.22’ lilikuwa mbele ya meza yake. Walinzi waliokuwa na bastola na bunduki mbalimbali walisimama kumzunguka.
“Kiongozi huyu wa waasi aliye mfupi amesema hakuwahi kuwa na mafunzo yoyote yanayohusu uasi nje ya nchi na kukanusha taarifa kuwa aliwahi kwenda Cuba au Perking (China). Alisema alipanga kuiangusha Serikali ya Zanzibar akisaidiana na Kamati Kuu yake ya watu waliopewa siku 14 tu ya mafunzo msituni.”