Timu ilicheza vizuri kuanzia nyuma mpaka katikati japo kulikuwa na mapungufu ya Gadiel na Maganga kupiga krosi ambazo hazina macho. Makocha tuwape muda waendelee kwani sasa hivi japo timu inafungwa walau kidogo inaonyesha uhai wa kupambana. Nikiitizama timu ya sasa na ile ya Amunike naona hii ya sasa inahitaji marekebisho kwenye upande wa ushambuliaji kwani mabeki na viungo walipeleka mipira mbele lakini Nado, Chilunda na Lyanga walikuwa wanajigonga tu. Lakini makocha wetu nao wajifunze sio kila wakati lazima ucheze na washambuliaji mbele tunaona hata timu kubwa ulaya mara nyingine zinawatumia viungo waliotulia kuwa washambuliaji kwenye baadhi ya mechi. Kwa sababu kama mipira ilikuwa inafika mbele mara nyingi tu kilichohitajika ni mtu tu hata beki mwenye utulivu wa hali ya juu na jicho la mwewe kuutumbukiza mpira ndani ya goli.
Kwa upande wangu naona matatizo ya timu ya taifa yapo zaidi kwa washambuliaji namba 9 na 10. Boko umri umeanza kumtupa mkono na ana majeraha ya mara kwa mara, hawa Nado na Chilunda ni washambuliaji wa pembeni zaidi au nyuma ya striker namba 9 na tuwategemee zaidi baadaye na sio sasa. Kiujumla hatuna mshambuliaji mwenye uwezo binafsi wa kuamua matokeo ndio maana tulicheza sisi mpira muda mwingi wa mchezo lakini Sudan walifika kwetu mara mbili tu na hapo wakapata bao moja. Baada ya bao ndio wakaanza wao kucheza mpira. Watanzania kwa ujumla tuwape moyo vijana wetu wenye maumbo makubwa waanze kucheza soka badala ya kukimbilia basketball na kuwa mabaunsa kwani soka la sasa pamoja na ufundi linahitaji pia nguvu.