Kutokana na kuongezeka kwa changamato za mabadiliko ya tabia nchi, mahitaji ya mabadiliko ya nishati duniani yameongezeka katika miaka ya hivi karibuni, na kuonyesha umuhimu wa kimkakati wa Afrika ambayo ina asilimia 30 ya rasilimali za madini duniani. Hii imekuwa fursa muhimu kwa Afrika. Marekani, bila kujali maslahi ya Afrika, inajaribu tena kuchochea uwanja wa vita wa kijiografia barani Afrika. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani hivi karibuni ilisema kuwa kipaumbele ni kuzuia “udhibiti” wa China katika sekta ya madini muhimu barani Afrika.
Kwanza, ni lazima kudhihirisha kuwa, kwa muda mrefu, rasilimali za madini za Afrika zimekuwa zikimilikiwa na nchi za Magharibi na makampuni yao ya kimataifa, ambayo yanachukua takriban theluthi mbili ya uzalishaji wote wa madini barani Afrika. China, kwa upande mwingine, imekuwa ikiongeza kasi ya ushirikiano na nchi za Afrika katika sekta ya madini, na uzalishaji unafikia chini ya asilimia 7. Hata hivyo Marekani imeonyesha wasiwasi mara kadhaa kuhusu maendeleo ya haraka ya ushirikiano wa maliasili kati ya China na Afrika. Katika mkutano wa kilele uliofanyika Hiroshima mwaka jana, Marekani ilipendekeza kushirikiana na Umoja wa Ulaya na wanachama wengine wa Kundi la G7 kuunda "Klabu ya Wanunuzi wa Madini Muhimu", ikijaribu kuiondoa China katika mnyororo wa ugavi wa madini kupitia Afrika. Kuhusu kauli hii, afisa wa biashara na viwanda wa Umoja wa Afrika alisema hadharani, "enzi za ukoloni zimepita, Afrika inahitaji washirika wa kweli wa ushirikiano wa kibiashara, haitakubali kuendelea kutumiwa kama eneo la uchimbaji wa maliasili."
Kwa kweli, jambo muhimu si Afrika kuwa na maliasili nyingi, bali ni jinsi gani ya kuzitumia kwa thamani. Hili linahusu sio tu mustakabali wa maendeleo ya bara zima la Afrika, bali pia linahusu suala la ajira kwa watu wa Afrika wanaoongezeka kwa kasi. Hivi sasa, China kama kinara katika sekta ya nishati mbadala duniani, inajitahidi kusaidia nchi za Afrika kuimarisha uwezo wao wa uchunguzi, uchimbaji na usindikaji wa madini, na kujadili uwezekano wa kuhamishia sehemu ya viwanda barani Afrika. Ikiwa maliasili zitasindikwa na kuzalishwa kati nchi za Afrika, hii itainua sana thamani ya madini ya Afrika, na kusaidia maendeleo ya viwanda barani Afrika. Wakati huo huo, wale wanaofahamu ushirikiano wa madini kati ya China na Afrika wanajua kuwa miundombinu duni pia ni kikwazo kikubwa cha uzalishaji wa maliasili barani Afrika. Katika hili, makampuni ya China yamezisaidia nchi nyingi za Afrika kutatua matatizo ya maji na umeme kwa ajili ya uchimbaji, na kujenga barabara na reli zinazoelekea bandarini, hivyo kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa maliasili, na kuweka msingi wa maendeleo ya sekta ya madini barani Afrika.
Hata hivyo Marekani na washirika wake wa Magharibi ambao wanapenda kuchafua na kushambulia ushirikiano wa China na Afrika wamefanya nini kuhusu maliasili za Afrika? Zinatekeleza ukoloni mamboleo kupitia taasisi za kimataifa na makampuni yao ya kimataifa yanayohudumia maslahi yao! Kwa mfano, Nigeria, kama nchi yenye utajiri wa mafuta barani Afrika, asilimia kubwa ya uzalishaji wa mafuta inadhibitiwa na makampuni makubwa ya kimataifa ya Magharibi. Wanajenga tu miundombinu ya uchimbaji, lakini hawajengi viwanda. Matokeo yake ni kwamba mafuta ghafi yanauzwa nje kwa bei ya chini, bidhaa za mafuta zinazouzwa kwa bei ya juu zinaagizwa Nigeria, na faida kubwa zinachukuliwa na makampuni ya Magharibi, hivyo sekta ya mafuta ya Nigeria haiwezi kuendelea. Hii ndiyo sababu, licha ya Afrika kuwa na maliasili mingi, bado ni bara maskini zaidi na lenye kiwango cha chini cha viwanda.
Baada ya kuichafua China kwa kauli ya "mtego wa madeni", "udhibiti wa maliasili za Afrika" umekuwa uongo mwingine ambao Marekani inasambaza kuhusu China barani Afrika. Lakini ukweli unapodhihiri, uongo mwishowe hujitenga. Kwenye mitandao ya kijamii, watu wengi wa Afrika wameonyesha kutoridhishwa na kauli zisizo za kweli za Marekani - "Ni wazi kuwa nchi za Magharibi kama vile Marekani ndizo zinadhibiti maliasili za Afrika, lakini wanasiasa wa Marekani wanailaumu China, hii ni kama mwizi anaponadi kumshika mwizi." "Kama ninyi watu wa Magharibi mngeacha kusumbua, Afrika ingekuwa bora mara mia moja kuliko ilivyo sasa. Ninyi ni wanyang'anyi na wezi." Marekani inajaribu kutumia Afrika kuendeleza maslahi yake ya kijiografia, jambo ambalo ni dharau kwa nchi na watu wa Afrika. Ingawa enzi za ukoloni zimepita, Afrika bado inahitaji kuwa makini na uwezekano wa "ubabe wa maliasili" wa Marekani na hata uwezekano wa kujirudia kwa historia ya unyang'anyi wa maliasili wa nchi za Magharibi.