MATESO YA MASHEIKH WETU
Ananiambia, ‘’Nakwenda sijda natamani nilie kwenye sijda lakini nyoyo hizi ngumu zimekufa ganzi na pengine hata kuta zake zimesinyaa machozi ya wapi ndugu yangu?
Nanyanyuka natazama picha ya Sheikh Ponda katika pingu yuko mahakamani askari magereza anamfungua pingu zake.
Naiambia nafsi yangu pingu hizi kafungwa Sheikh Ponda si kwa kuwa ni jambazi, la hasha, kafungwa pingu hizi kwa kupigania haki za Waislam na wao waheshimike na wapewe kile ambacho wamekuwa wakikipata wengine toka uhuru upatikane mwaka wa 1961,
Naiambia nafsi yangu Sheikh Ponda yamemkuta yale kwa kupigania kile ambacho Waislam walikifikiria watakipata walipokuwa wanapigania uhuru wa Tanganyika.
Taratibu machozi yanatoka nafungua ukurasa mwingine nawaangalia masheikh wetu waliokuwa kifungoni kwa miaka takriban saba hawana kosa lolote na kesi inaahirishwa kwa miaka saba.
Sasa machozi utadhani bomba limefunguka.
Mume wangu anasikia kwikwi yangu ananifuata na kunipa glasi ya maji napokea.
Hasemi lolote kwani kazoea sasa na anajua kinachoniliza.
Nasoma dua na yeye ndiye muitikiaji wangu.
Mwanangu mkubwa siku moja kaniuliza, ‘’Mama unagombana na baba?
Nakusikia usiku unalia.’’
Wakati mwingine nawaona masheikh wengine katika runinga wamevaa kanzu nzuri za kupendeza kwa rangi zake na kofia za kumeremeta na makoti ya thamani juu wametupia kashda wako katika meza kuu na wakubwa wa chama serikali.
Nyuso zao zinang’ara kwa vyakula na vinywaji vizuri.
Inanijia picha ya masheikh wetu wako Segerea wanalalia virago na kupata shida zote za gerezani.
Nawafikira watoto na wake zao huko waliko na shida hizi za maisha.
Najiuliza hawa masheikh wengine vipi wanaweza kuoga na kujipara na kula na kunywa na wale ilhali ndugu zao wako jela wanateseka?
Tuko mezani na mume wangu na watoto wakati wa chakula cha jioni.
Runinga inawaleta masheikh wengine wamekaa na wale wamependeza wanacheka na kufurahi.
Nikiwafikiria masheikh wetu chakula kinanitumbukia nyongo nanyanyuka kimya kimya sitaki wanangu waone nalia nakwenda chumbani kujificha.
Mume wangu ananiambia, ‘’Honey usimsikilize Sheikh Mselem bin Ali akitafsiri Qur’an anakuliza na usidhani kuwa mimi siumii naumia sana lakini mimi mwanamme naweza kujikaza.
Usimsikilize Sheikh Mselem anakuliza Allah anakuelewa.’’