HakiElimu yabeza ushindi wasichana kidato cha IV
Imeandikwa na Lucy Lyatuu; Tarehe: 28th January 2011 @ 23:57 Imesomwa na watu: 203
BAADA ya wasichana waliomaliza kidato cha nne mwaka jana kufanya vizuri kwenye mitihani hiyo na kuchukua nafasi nane za kwanza, Shirika la HakiElimu na Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) wamebeza ushindi huo na kusema ni wa chini.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa Januari 26 na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) wasichana wanane walishika nafasi hizo huku wakiwaongoza wavulana wawili katika kundi la 10 bora.
Hata hivyo taasisi hizo mbili zisizo za Serikali zimesisitiza kuwa bado kiwango chao cha ufaulu kiko chini kikilinganishwa na cha wavulana ambao zimesema bado wako juu.
Aidha, wamesema ipo haja sasa ya kutenganisha taaluma na siasa na kusimamia kwa dhati sera na mikakati ya kuboresha elimu, ili ifikie mahali elimu iwe ya kumkomboa mwanafunzi.
Hali kadhalika walitoa mwito jana wa kutekelezwa ahadi za elimu zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni mwaka jana, ili kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kisiendelee kushuka.
Akitoa tathmini ya matokeo ya kidato cha nne jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Elizabeth Missokia, alisema matokeo ya kidato cha nne yaliyotolewa na Necta yanaashiria hali ya hatari kuhusu mwelekeo wa elimu nchini.
Katika matokeo hayo, wanafunzi 40,388 kati ya 352,840 ya waliofanya mtihani huo ndio waliofaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu, ambapo ni dhahiri kuwa ufaulu huo ni mdogo ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi 310,826 waliopata daraja la nne na sifuri.
Missokia alisema kwa mujibu wa matokeo ya jumla, wavulana wamefaulu kwa asilimia 56.28 na wasichana asilimia 43.47 huku takwimu hizo zikionesha kuwa wasichana wana ufaulu wa chini kwenye idadi ya ufaulu wa kiwango cha daraja la kwanza hadi la tatu.
Alisema takwimu zinaonesha wavulana waliofaulu kwenye ngazi hizo ni asilimia 14.6 na wasichana asilimia 7.81 ambayo ni tofauti kubwa na kwa ufaulu huo haiwezekani kujivunia idadi ndogo ya wasichana kuwa kwenye 10 bora wakati ufaulu kwa ujumla unaonesha bado wako chini.
Ikumbukwe, kuwa taarifa zinaeleza idadi kubwa ya wasichana wanaendelea kukatisha masomo yao kutokana na mimba za utotoni na mambo mengine, alisema na kuongeza.
Hatuwezi kujifariji kwa kuangalia ufaulu wa wenzao wachache wakati huo huo fursa za walio wengi zikibinywa, malengo ni kuwaendeleza wote; wasichana na wavulana kwa haki sawa, alisema Missokia.
Alisema anguko hilo la ufaulu limewakumba watoto wengi wanaosoma shule za kata ambapo wadau wengi wa elimu na watoto wenyewe, wamekuwa wakipigia kelele changamoto zinazowakabili kama uhaba wa walimu, mazingira duni ya kujifunzia, uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia na hamasa ndogo ya wanafunzi.
Missokia alisema hakuna haja ya kulumbana wala kuingiza siasa kwenye elimu, bali Serikali itekeleze mipango na sera zilizopo na kuondoa upungufu kwa kushirikisha wadau, kwa kuwa
nchi haiwezi kuendelezwa na watu wachache wanaopata fursa za kipekee kwenye shule chache huku elimu pana ikiwa shakani.
Ofisa Mchambuzi wa Sera na Uhamasishaji wa TENMET, Florence Francis, alisema matokeo hayo yanaashiria kwamba hatima ya watoto wengi walioko shuleni iko shakani kwa kuwa kati ya shule 4,266 za sekondari nchini, robo tatu yao ni za Serikali pamoja na shule za kata, ambako ndiko wanakosoma watoto wengi wa Watanzania masikini.
Alisema anguko kubwa la wanafunzi kwenye sekondari za kata na za Serikali linamaanisha ni anguko la maelfu ya Watanzania wanaosoma katika shule hizo.