SAFARI SABA ZA SINDBAD, BAHARIA
KATIKA enzi ya Khalifa Harun Rashid, paliondokea mchukuzi mmoja masikini aliyekuwa akikaa katika mji wa Baghdadi, jina lake Hindbad. Siku moja jua lilipokuwa kali mno alitumwa kuchukua mzigo toka mwanzo wa mji mpaka mwisho wa mji, basi kabla hajafika nusu ya safari yake, akatokea katika njia moja iliyonyunyizwa marashi na upepo mzuri ulikuwa ukimpiga usoni,
akatua mzigo wake na kukaa kitako kando ya njia karibu na jumba
kubwa, ili kujiburudisha.
Alipokuwa amekaa hapo, akafurahi sana kusikia harufu za udi na ambari zikitokea mle ndani ya ile nyumba, na zaidi ya hayo alisikia ngoma na sauti za ndege zikiimba vizuri. Pia alisikia harufu ya vyakula vizuri na akafahamu kuwa ndani ya nyumba ile mna karamu. Basi kwa vile alivyokuwa hapiti njia ile mara kwa mara wala hana habari za mtu anayekaa katika jumba lile, akafanya hamu kupeleleza ili ajue, basi alipomwona mtumishi aliyekaa mlangoni akamwendea, na kumwuliza jina la bwana wake.
Mtumishi akajibu akistaajabu, 'Oh! Wewe umekaa hapa Baghdadi kwa siku kadha wa kadha, nawe hata leo hujajua kuwa jumba hili ni la Sindbad Baharia, msafiri mkubwa aliyezunguka dunia?
Mchukuzi aliposikia hivi akakumbuka maneno aliyoyasikia zamani kuhusu utajiri wa Sindbad; akiifikiri hali yake na hali ya Sindbad alimwonea kijicho. Akawaza kuwa kiasi cha furaha ya Sindbad ni sawasawa na kiasi cha taabu zake, naye akajinung’unikia sana hata moyo ukamchafuka, ndipo akainua macho yake mbinguni na kunena kwa sauti kuu, 'Ewe Mwenyezi Mungu, muumba wa vitu vyote, angalia tofauti kati ya Maisha yangu mimi na Maisha ya Sindbad! Kila siku naumia kwa taabu na mashaka hata ule mkate wa kula mimi na watoto wangu ni shida kuupata, huku kumbe Sindbad anatumia atakavyo na maisha yake ni furaha tupu! Amefanya nini hata ukampa raha hii, na mimi nimefanyaje hata nikastahili taabu hizi?'
Alipokwisha kusema hivi akainamisha kichwa kama mtu anayekata tamaa kabisa.
Basi mara ile ile nmtumshi akaja kutoka kwenye ile nyumba kumshika mkono akimwambia ‘Nifutuate, kwani bwana wangu, Sindbad, anataka kusema nawe.’
Hindbad akastaajabu sana maana hakujua analoitiwa, hata alipokumbuka yale maneno aliyokuwa akisema akaogopa sana akifikiri kuwa labda Sindband amesikia na sasa anaitwa kusudi kwenda kuadhibiwa. Kwa hivyo akatoa udhuru na kusema,
‘Siwezi kuacha mzigo wangu njiani’
Lakini watumishi wa Sindbad wakamwambia, ‘Sisi tutakutunzia
mzigo wako’, kisha wakazidi kumshurutisha mpaka akakubali. Basi wale watumishi wakamchukua kumpeleka katika chumba kikubwa ambamo aliona watu waliokaa juu ya meza iliyoandaliwa vyakula vizuri vya kila namna, na mwisho wa ile meza kulikuwa na mtu mmoja mwenye sura nzuri amekaa, naye alikuwa na ndevu nyingi nyeupe. Nyuma yake walisimama watumishi wengi tayari kufanya watakaloambiwa. Mtu huyo alikuwa ndiye Sindbad maarufu. Basi yule mchukuzi alipoona watu wengi kama wale akafanya hofu: akawaamkia huku anatetemeka, lakini Sindbad mwenyewe akamkaribisha akaa upande wa mkono wake wa kulia, kisha akamgawia chakula na mvinyo kwa mkono wake mwenyewe.
Walipokwisha kula Sindbad akawa anaongea naye kama watu waliojuana zamani, akamwuliza jina lake na habari zake. Mchukuzi akajibu, ‘Bwana wangu, Jina langu naitwa Hindbad.’
Sindbad akasema, 'Nimefurahi kukuona, nami nawasemea wote waliopo kuwa nao pia wamefurahi kukuona. Na sasa napenda uniambie yale maneno uliyokuwa ukisema kule njiani,’ maana Sindbad mwenyewe alimsikia akisema chini ya dirisha lake ndiyo sababu akamwita na kumkaribisha.
Alipoambiwa hivi, Hindbad akainamisha kichwa kwa haya, akajibu, 'Bwana wangu, wakati nilipokuwa nikisema maneno hayo nilikuwa nimechoka sana, na sasa naomba uniwie radhi.’
Sindbad akamwambia, ‘Usidhani kuwa raha hii na vitu hivi vya anasa nilivyo navyo sasa, nimevipata bure bila kusumbuka kwa taabu na mashaka ya dunia, la! Osifikiri hivyo, imefika hali hii niliyo, baada ya kuteseka miaka mingi kwa taabu za kiwiliwili na moyo pia.’ Kisha akawageukia watu waliokuwapo akawaambia, ‘Rafiki zangu, matajiri wako wengi-lakini kama wangalipata taabu namna nilivyopata mimi, wangalikata tamaa ya kupata utajiri tangu mwanzo, tena wangalikuwa radhi kurudi makwao katika hali ya umasikini. Labda hamjasikia habari za safari zangu saba za ajabu! Na hatari zilizonipata. Basi maadam leo nimepata nafasi ya kukwambieni habari za safari hizo, nitakwambieni.’ Na kwa kuwa Sindbad alitaka yule mchukuzi naye asikilize habari hizo, akamwamuru mtumishi wake aende kumchukulia ule mzigo wake ampelekee huko alikotaka kuupeleka, kusudi yeye akae kusikiliza hadithi.
SAFARI YA KWANZA
BASI Sindbad akaanza kutoa hadithi yake hivi: -Babaangu alipokufa aliniachia mali mengi mno isiyo idadi; na fungu kubwa la mali hiyo nililitumia katüka starehe za ujana wangu, lakint halafu yake nikaona kuwa napoteza mali na hali pia, tena nikakumbuka kwamba mtu kuwa mzee kisha masikini ni mashaka makubwa mno. Baada ya kuingiwa na fikira hii, nikakusanya mali yangu yote iliyosalia nikaondoka na kwenda kujipakia chomboni pamoja na wafanyaji biashara, nikaenda Basra.
Tukasafiri kuelekea upande wa Mashariki kupita ghuba ya Ajemi. Awali ya safari yetu nilitaabika sana kwa bahari jinsi ilivyonilevya lakini baadaye nikaizoea, wala sikutaabika tena. Katika kusafiri kwetu tukapita visiwa vingi, tukawahi kuuza bidhaa zetu kidogo na zingine tukazibadılisha kwa vitu visivyopatikana katika nchi yetu. Hata siku moja tukafika katika kisiwa kingine kidogo kilichokuwa kimeinuka kidogo tu juu ya bahari. Basi baada ya kutua matanga, nahodha akatoa ruhusa kwa watu watakao kushuka pwani, washuke, na mimi nilikuwa mmoja wao.
Basi wakati tulipokuwa katika furaha zetu za kula na kunywa, na kujisahaulisha taabu za bahari, mara kile kisiwa kikaanza kuti- kisika sana hata wale wenzetu waliokuwa wamebaki chomboni wakakiona kikitikisika, nao wakatwita turudi upesi ili tujipakie tujiponye, kwani kile tulichodhani kuwa ni kisiwa hakikuwa kisiwa, ila ni mgongo Wa nyangumi. Waliokuwa wepesi wakangia mashuani tulioshukia pwani na wengine wakajitosa baharini kuogelea, na mimi kabla sijawahi kujiponya, kwa ghafla nyangumi akajizamisha baharini na kuniacha nikitapatapa majini kukimbilia kipande cha mti tulichokileta kutoka chomboni kwa kufanya kuni.