KERO Mbezi Mwisho: Suala la kuwapunguzia nafasi Wafanyabiashara waliopo ilikuwaongeza wengine linatuathiri Wafanyabiashara wa chakula

KERO Mbezi Mwisho: Suala la kuwapunguzia nafasi Wafanyabiashara waliopo ilikuwaongeza wengine linatuathiri Wafanyabiashara wa chakula

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
Tumekuwa tukiona juhudi za kuboresha maeneo ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo kwa kuwekwa vibanda vya maturubai na wakati mwingine kuezekwa kwa bati kwa gharama zinazotolewa na wafanyabiashara wenyewe. Hili ni jambo zuri na la kupongezwa kwa kuwa linasaidia kuboresha mazingira ya biashara.

Hata hivyo, changamoto inaanza pale baadhi ya viongozi wanapotaka kuingiza wafanyabiashara wapya katika maeneo hayo na kusababisha wale waliokuwepo awali kupunguziwa nafasi zao za biashara. Hali hii imekuwa ikiathiri zaidi wafanyabiashara wadogo, hususan mama ntilie na wauzaji wa vyakula, ambao wanahitaji nafasi ya kutosha ili kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.

Baadhi ya wafanyabiashara walipohoji kuhusu changamoto hiyo, wamekuwa wakijibiwa kuwa si lazima waendelee na biashara ya chakula na kwamba kama wanaona haiwezekani wanapaswa kubadilisha biashara. Kauli kama hizi si suluhisho na hazizingatii hali halisi ya wafanyabiashara wengi ambao wamewekeza muda na nguvu zao katika biashara hizo.

Wafanyabiashara wengi wa chakula wana hali za kawaida kiuchumi na si rahisi kwao kupata mtaji wa kuanzisha biashara nyingine au kumudu gharama za kupanga fremu za biashara. Kuwalazimisha kubadilisha biashara bila kuwapatia njia mbadala ni kuwaongezea changamoto na kuhatarisha maisha yao ya kila siku.

Changamoto nyingine ni pale wananchi wanapoondolewa kwenye maeneo waliyokuwa wakifanyia biashara kwa maelezo kuwa maeneo hayo yanamilikiwa na watu binafsi. Kinachoshangaza ni kuona baadhi ya watu hao binafsi wakiruhusiwa kujenga vibanda vya biashara katika maeneo hayo na kisha kuvikodisha kwa wafanyabiashara wadogo kwa gharama kubwa, kati ya Shilingi 400,000 hadi 600,000 kwa mwezi.

Mfano ni eneo linalotazamana na Benki ya NMB, ambapo inadaiwa kuna mtu mmoja anayemiliki vibanda vinne na fremu sita, lakini bado anataka kupewa eneo lote la mbele ili ajenge vibanda zaidi na kuvipangisha. Hali hii inaathiri wafanyabiashara wadogo ambao wengi wao hutegemea maeneo hayo kufanya biashara zao na hata kununua bidhaa kwenye maduka ya jumla yaliyopo hapo.

Kwa kumalizia, tunaiomba Serikali na viongozi husika kusimamia kwa haki masuala ya maeneo ya biashara na kuwa mstari wa mbele kuwalinda wafanyabiashara wadogo. Katika nchi yenye changamoto ya ajira na idadi kubwa ya vijana wanaohitimu bila kupata ajira, biashara ndogo ndogo ni sehemu muhimu ya suluhisho la maisha ya wananchi wengi.

Kumpa mtu mmoja eneo linaloweza kusaidia maisha ya mamia ya familia si jambo la haki. Wafanyabiashara wengi wamejenga biashara zao kwa miaka mingi, wameweza kuhudumia familia zao na hata kutoa ajira kwa wengine. Kumwambia mtu aliyepambana kwa zaidi ya miaka 10 aachane na biashara yake na aanze nyingine bila kuangalia athari zake ni kuathiri maisha ya watu wengi wanaomtegemea.

Uamuzi wowote wa upangaji wa maeneo ya biashara unapaswa kuzingatia maslahi ya wananchi wengi, si manufaa ya mtu mmoja mwenye uwezo mkubwa wa kifedha.
 
Back
Top Bottom