Mbunge Eric Shigongo Asema Atayafikisha Mahakamani Malalamiko ya Watumiaji Kuhusu Bando za Intaneti

Mbunge Eric Shigongo Asema Atayafikisha Mahakamani Malalamiko ya Watumiaji Kuhusu Bando za Intaneti

Joined
Dec 6, 2025
Posts
7
Reaction score
5
Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo, ametangaza dhamira ya kulifikisha mahakamani suala la malalamiko yanayoendelea kutolewa na watumiaji wa huduma za intaneti kuhusu bando kuisha au kukatwa kabla ya muda wanaotarajia.

Hatua hiyo imekuja baada ya kusambaa kwa video ya Niffer akielezea changamoto ya bando la intaneti kuonekana kuisha kwa muda mfupi licha ya kuendelea kununua vifurushi mara kwa mara. Katika maelezo yake, Niffer hakutaja mtandao wowote wa simu nchini Tanzania, lakini alizungumzia tatizo ambalo limekuwa likilalamikiwa na watumiaji wengi.

Akizungumzia suala hilo, Shigongo amesema kuwa licha ya kulifikisha Bungeni hapo awali, bado malalamiko kutoka kwa wananchi yanaendelea kuongezeka.

“Baada ya kuongea suala hili Bungeni, bado hali inazidi kuwa mbaya. Malalamiko yanaongezeka. Nimeamua kwa niaba ya watumiaji kulipeleka suala hili mahakamani kama walivyofanya Afrika Kusini walioishitaki ICASA, ambayo kwa hapa kwetu ni TCRA, pamoja na kampuni za simu,” alisema.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, lengo la kwenda mahakamani ni kutafuta suluhisho la kudumu na kupata ufafanuzi kuhusu madai ya watumiaji kwamba baadhi ya bando huisha kabla ya muda uliowekwa.

Aidha, Shigongo amesema anatarajia mahakama inaweza kuagiza uchunguzi maalumu kufanyika ili kubaini iwapo kuna dosari katika mfumo wa matumizi ya bando au la. Pia anapendekeza kuwepo kwa utaratibu wa kuruhusu salio la bando ambalo halijatumika kuendelea kutumika hata baada ya muda wa kifurushi kuisha.

Mbunge huyo ameongeza kuwa endapo kutahitajika ushirikiano wa watumiaji katika hatua za kisheria zitakazofuata, atatoa taarifa rasmi kwa umma ili waweze kushiriki katika mchakato huo.

Suala la matumizi ya bando za intaneti limeendelea kuwa miongoni mwa hoja zinazojadiliwa mara kwa mara na watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini, huku wengi wakitaka uwazi zaidi kuhusu namna matumizi ya data yanavyohesabiwa na kusimamiwa.


View: https://www.instagram.com/reel/DaCfehvgw-w/?igsh=cjUwcmtuaHRqY2Q4
 
Back
Top Bottom