Ndugu zangu watanzania,
Ukiwa mbunge wa jimbo lazima ufahamu na kutambua kuwa wewe ni kiongozi mkubwa sana ndani ya jamii,sauti yako ni kubwa ,una uwezo wa kufikisha chochote na kikasikilizwa na kupokelewa na Serikali,wewe ni sauti ya wananchi na mwakilishi wa watu waliokupigia kura na ambao hawajakupigia kura. Hivyo usimamapo popote pale bila kujali umejaa furaha kiasi gani au hasira kiasi gani ndani ya kifua chako ,wakati wote na muda wote unapaswa kuuchunga sana ulimi na mdomo wako.
Unapaswa kuwa mwenye kifua ,mwenye kupima kauli kabla ya kutamka hadharani,mwenye kudhibiti furaha,jaziba ,mihemuko,sifa na hata kujiepusha kutoa neno au maneno ambayo yataleta athari na sintofahamu katika jamii. Mbunge ni mtu anayeshiriki vikao vingi vya wazi na siri,mwenye kujuwa mambo mengi mazito na mepesi,machungu na matamu,ya viapo na miiko,ya siri na nyeti. Hivyo mbunge ni mtu anayepaswa kuwa timamu kiakili hata akiwa amelewa hapaswi kuendeshwa na pombe kichwani pasipo tafakari au kujielewa nini anatamka na anakusudia kutamka.
Kitendo cha mbunge kusimama Hadharani na kusema kuwa Alipitisha na kupigia kura kitu ambacho alikuwa Hakijuwi ni fedheha na aibu kwa mbunge mwenyewe ,ni kujidhalilisha na kukidhalilisha chama na wanachama waliomuamini na kumpitisha katika kura za maoni,ni kuwavunja moyo waliompigia kura kuwa mwakilishi wao Bungeni na kuwakatisha Tamaa viongozi wetu wa chama wanaokipigania chama usiku na mchana ,kwa jasho na machozi katika kuhakikisha kuwa chama kinapata ushindi katika kila uchaguzi wa ngazi zote na kuwatumikia wananchi kwa bidii na maarifa katika kuhakikisha kuwa wanapata huduma iliyo bora kutoka kwa serikali yao.
Amenifedhehesha na kunikwaza sana kama mwana CCM kindaki ndaki,Amenishangaza na kunisononesha Sana .Hapaswi kupewa nafasi ya kugombea tena uchaguzi ujao ,anapaswa kukatwa jina lake mapema sana .Hata kama pia anajuwa hatagombea uchaguzi ujao hakupaswa kuzungumza aliyoyazungumza kwa kuwa amekichafua chama na kuleta Taswira mbaya kwa chama. Ameonyesha kuwa hapaswi kuendelea kuaminiwa na chama ,hapaswi kushirikishwa mipango na mikakati mikubwa kwa kuwa ameonyesha kuwa na kifua kidogo na kukosa utulivu ,hekima na busara za kiuongozi,Ameonyesha kuwa chama kilikosea kumuamini na kumpa nafasi ya kupeperusha bendera ya chama ,anaonyesha kuwa chama kinapaswa kuwaomba msamaha wananchi wake kwa kuwapa mtu ambaye kumbe hana uelewa wa kufanya uchambuzi wa miswaada ilihali alikuwa anajuwa kuwa kazi ya Bunge na mbunge ni kutunga sheria,kuisimamia serikali n.k na wala hatoshi kuwa mbunge na kuwa Bungeni.
Anapaswa kukatwa jina lake kwa kuwa amejikata mwenyewe kabla ya kukatwa kwa kuwa ameonyesha hatoshi kuwa mbunge, hatoshi kuwa mwakilishi wa wananchi,hapaswi kushiriki wala kushirikishwa kwenye mipango na mikakati mikubwa ya aina yoyote ile , chama kina paswa kuwa naye chonjo sana ili asiendelee kukichafua chama na kuharibu Taswira njema ya chama chetu cha CCM. Kulikuwa na sababu gani ya kuongea aliyo yaongea hadharani? Alikuwa anamfaidisha nani? Alikuwa anatuma ujumbe gani kwa chama? Alikuwa anataka kuwaambia nini wapiga kura wake? Alikuwa anataka kupeleka ujumbe gani kwa jamii? Msimamo wake ni upi kwa sasa?
Kama mtu huna cha kuongea ni bora ukae kimya tu, hata kama umepewa nafasi ya kuongea ni bora uishie kusalimia tu na kukabidhi maiki.
Kazi iendelee, mama Ametufikia na kuwafikia watanzania kwa utumishi wake uliotukuka wa kugusa maisha ya watanzania wanyonge wasio na Sauti.
Lucas Hebel mwashambwa, kijana mzalendo na mpenda nchi yangu.
0742-676627.