Mchango wa timu za madaktari wa China watambuliwa na kuthaminiwa zaidi watu wa Afrika

Mchango wa timu za madaktari wa China watambuliwa na kuthaminiwa zaidi watu wa Afrika

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,116
Reaction score
1,121
689.jpg


Pili Mwinyi

China na Afrika zinaendelea kuwa na ushirikiano mkubwa kwenye sekta mbalimbali muhimu ikiwemo ya afya. Uwepo wa timu za madaktari wa China katika nchi za Afrika kwa sasa unaonekana ni jambo la kawaida na limeshazoeleka, ambapo madaktari hawa wanajitahidi kadiri wawezavyo kuokoa maisha ya maelfu ya watu wa Afrika.

Tangu China itume timu yake ya kwanza ya madaktari bingwa Afrika mwaka 1963, imekuwa ikitumia nguvu zake zote kuisaidia Afrika, ikiwemo kujenga taasisi za afya, kutoa dawa na vifaa vya matibabu, kuandaa mafunzo na kutoa udhamini wa masomo kwa ajili ya kujenga miundombinu ya afya, kuwajengea uwezo madaktari na kuwapatia mafunzo wanafunzi wanaosomea mambo ya afya ili kuibua madaktari bingwa katika nchi zao.

Nchini Tanzania, Timu za madaktari wa China ni maarufu sana na mara kwa mara zimekuwa zikipongezwa kwa mchango wake mkubwa wa kutibu magonjwa ambayo hapo awali yalionekana kushindikana. Kutokana na juhudi hizo, rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi hivi majuzi tu aliwapa nishani ya heshima madaktari 21 wa timu ya matibabu ya China huko ikulu ya Zanzibar, kutokana na huduma zao kubwa walizotoa katika kipindi cha mwaka mmoja waliokuwepo Zanzibar kuwahudumia Wazanzibari, ikiwemo kufanya upasuaji wa magonjwa mbalimbali.

Katika hotuba yake rais Mwinyi alisema wana kila sababu ya kushukuru na kutambua kazi nzuri iliyofanywa na madaktari hao kutoka China ambao wamehakikisha watu wa Zanzibar wanapata huduma bora kabisa za matibabu katika mwaka mmoja uliopita.

Ni lazima tukiri kwamba wanachofanya madaktari wa China ni zaidi ya kuwatibu wagonjwa, kwani timu hiyo pia ilitoa vifaa ya matibabu na dawa na kuwafunza madaktari wenyeji. Ndio maana rais Mwinyi amesisitiza kuwa madaktari hao wamesaidia kuimarisha mfumo mzima wa afya.

Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja iliyopo Mji Mkongwe, ni hospitali ya mafunzo huko Zanzibar. Kwa miongo kadhaa, wagonjwa wanaokwenda hospitalini hapa wanatibiwa na madaktari Wachina. China imekuwa ikituma timu zake za madaktari Zanzibar kwa miaka 50 iliyopita, na kila timu inakaa kwa miaka miwili. Akielezea uzoefu wake kiongozi wa timu ya madaktari ya China, Dkt Liu Yaping anasema wanakwenda kuchangia ujuzi wao na kupeleka upendo wao kwa watu wa Zanzibar.

“Kazi yetu ni kutoa huduma za afya kwa wenyeji wa Zanzibar na kuwaondolea magonjwa. Lakini lengo letu kuu ni kukuza urafiki kati ya China na Tanzania na kati ya Zanzibar na China.” alisema Dkt Liu Yaping

Mwezi Novemba mwaka 2017, meli ya matibabu ya China "Peace Ark" ilikwenda Tanzania na kukaa kwa siku nane jijini Dar es Salaam, ikiwapatia Watanzania 6,441 huduma bure za matibabu. Ujio wa meli hiyo ulionekana kuandika historia mpya ya urafiki na ushirikiano wa nchi hizi mbili.

Kisiwani Zanzibar madaktari wa China wanaheshimika sana, mmoja wa wagonjwa aliyekwenda kupatiwa matibabu na madaktari hawa anasema Wachina wanakwenda Zanzibar na kutoa mchango wao katika sekta mbalimbali lakini sekta hii ya matibabu imekuwa ni nzuri sana kwao hasa kwa wanaopata matibabu.

Timu za madaktari za China zimekuwa zikitumwa katika nchi mbalimbali za Afrika na kusaidia kupambana na magonjwa makubwa na hata ya hatari zaidi. Mwaka 2015, Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Johannesburg uliorodhesha ushirikiano wa afya ya umma kama sehemu ya mipango 10 ya ushirikiano kati ya China na Afrika, na kuufanya ushirikiano huu upande ngazi ya juu zaidi.

Licha ya kwamba China ipo mstari wa mbele kutoa huduma za afya Afrika, pia imekuwa ikiyarai hata mashirika mengine ya kimataifa na nchi zote duniani kushirikiana pamoja kukabiliana na changamoto za afya duniani na kusaidia kujenga sekta ya afya katika nchi zinazoendelea kupitia ushirikiano wa Kusini-Kusini.

China daima itaendelea kuongeza juhudi zake katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya barani Afrika, kuimarisha mfumo wa kukinga na kudhibiti afya ya umma katika Afrika, kuunga mkono zaidi mahitaji ya afya kwa vijana na wanawake ambao ndio wanaonekana wahanga wakubwa, kuimarisha mawasiliano baina ya mtu na mtu kwenye masuala ya afya na kunufaisha watu zaidi kupitia ushirikiano kati ya China na Afrika.
 
Back
Top Bottom