Ze Bulldozer
JF-Expert Member
- Jun 12, 2020
- 1,070
- 568
===
Arusha. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa amewaagiza waajiri wote nchini kuchukua hatua kuwaondoa katika nafasi zao baadhi ya maofisa utumishi walioshiriki kuficha sifa za watumishi wenzao hali iliyosababisha kutopandishwa madaraja.
Akizungumza katika mafunzo ya viongozi wa matawi ya Chama cha wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) na waajiri yaliyofanyikia jijini Arusha, Mchengerwa amesema waajiri waende kuwashusha vyeo maofisa utumishi hao na nafasi hizo wawekwe watu wenye uwezo ambao watakuwa tayari kusikiliza kero za watumishi wenzio.
Amesema si watumishi ambao wapo katika ofisi kwa ajili ya matumbo yao hiyo haikubaliki hivyo ni lazima kila mmoja akabadilisha mitazamo yake kwa sababu Serikali ya sasa haitaki uonevu.
"Kila kiongozi lazima atengeneze ushawishi wa kuleta mapinduzi ya kifkra kama tunakuwa na watendaji ambao hawapendi kuona wenzao wanafanikiwa na wakipewa nafasi wanadhani miji yote ya kwao, hawafahamu kuwa vyeo hivi ni vya kupita tu pia wanasahau kwamba utumishi wa umma una muda," amesema waziri huyo.
Waziri huyo amehimiza waajiri kujenga utamaduni wa kuwajengea uwezo watumishi wao ili kuweza kupata weledi na kuleta uelewa ambao utakwenda kutoa kasoro ambazo zitakwenda kuleta ajali kazini.
Naye Katibu Mkuu wa Tughe, Hery Mkunda amesema mafunzo hayo yanalenga kuleta uelewa wa pamoja katika masuala ya waajiri na watumishi lakini pamoja na ushirikiano huo bado wanakabiliwa na changamoto ya uwepo wa baadhi ya vifungu vya sheria na kanuni ambazo zinaweza kuleta mgongano katika utendaji kazi.
Source: Mwanachi