Anaweza kuwa kitu chochote atakacho lakini na hakika hawezi kuwa Mungu...Awatishage ninyi..Wengine hatutishiki na miungu kwakua aliye ndani mwetu ni mkuu kuliko aliye nje ya mimi. Hapa napigania imani ambayo kwayo inapotoshwa na kusababisha wadogo ambao wangeliamini jina la Yesu wanakuwa na mashaka...Kila anayelitaja jina la Bwana na aache uovu. Hata mimi leo nikijiinua na kuanza kupigania ukuu wa jina langu hali nikijua jina la Yesu linadhihakiwa naamini Mungu hata niacha salama...
Leo hii wokovu unaanza kutiliwa mashaka kwasababu ya matendo ya watu wa jinsi hii ambao wanakuza majina yao zaidi kuliko lile la Yesu mwokozi asiye mbaguzi...Majina hayo lazima tuya demote na yatakuwa demoted kwa jina kuu la Yesu ili yeye abaki wa kuaminiwa na kuabudiwa!
KATIKA siku za hivi karibuni, kumezuka madai kutoka kwa wakristo , kwamba Yehova siyo Allah (s.w.).
Msingi mkuu wa dai hilo ni kwamba Yehova na Allah, wamekuwa ni miungu wawili tofauti eti kwa sababu Yehova ana mwana, lakini Allah hana mwana!
Ili uweze kupata ukweli wa mambo, fuatana nami, uone uchambuzi wa kina juu ya dai hilo pamoja na msingi wake huo.
Na kubwa zaidi, uweze kuona kama majina haya yanamhusu Mwenyezi Mungu mmoja (Mungu wa Ibrahimu, Ishmaeli, Isaka na Yakobo). Aidha, uweze kuona kama kuna uhusiano wowote kati ya Yehova na Wakristo.
Ukweli kuhusu Yehova
Kulingana na maelezo ya Biblia, Yehova ni jina takatifu la Mwenyezi Mungu walilolitumia Wayahudi kwa mnasaba wa lugha yao ya Kiebrania. (Tazama the Holy Bible in Kiswahili, Union Version Uk. vi). Aidha,, kwa mujibu wa mafundisho ya Biblia, jina hilo Mungu alilifunua kwa mara ya kwanza kwa Nabii Musa (a.s.). Maandiko yafuatayo yanathibitisha ukweli huu:
"Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni Yehova, mami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka na Yakobo kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu Yehova sikujulikana kwao". (Kutoka 6:2-3)
Kulingana na maandiko hayo juu, tunachojifunza hapa ni kwamba Yehova ni Mwenyezi Mungu. Aidha, Mwenyezi Mungu anathibitisha wazi kuwa hakuwahi kujitambulisha kwa jina hilo (la Yehova) kwa Manabii wake wengine aliowataja katika maandiko hayo ambao walikuwepo kabla ya Nabii Musa (a.s.). Lakini anasema alijifunua kwao kama "Mungu Mwenyezi".
Aidha, kwa kuzingatia shuhuda hiyo, tunajifunza pia kuwa tokea zamani ilikuwa ni desturi ya Mungu kujifunua kwa Manabii wake mbali mbali akijitambulisha kwa majina tofauti. Ni dhahiri kwa shuhuda hiyo peke yake yatosha kukubali vile vile kwamba Mwenyezi Mungu alipojitambulisha kwa jina la "Allah" kwa Nabii wake wa mwisho, Mtume Muhammad (s.a.w.) pia ilikuwa ni katika ile ile desturi yake ya kujifunua kwa Manabii wake kwa majina tofauti ambayo mara nyingi yalinasibihiana na lugha zao.
Zaidi ya hivyo, lakini hoja ya msingi inayoweza kudhihirisha majina ya Allah na Yehova kwamba ni majina yanayomhusu Mwenyezi Mungu yule yule mmoja ni kazi, utukufu na sifa zake, kama zilivyoelezwa vizuri na Qur'an tukufu na Biblia takatifu. InshaAllah hoja hizo tutakuja kuziona kwa mapana na marefu hapo baadae. Na ndipo tutakapoyakinisha kama kweli Mungu huyo anaye mwana au la. Hata hivyo, kabla sijazibainisha hoja hizo, ni vyema kwanza tukaangalia zaidi jinsi Mungu huyo huyo mmoja alivyojifunua na kujitambulisha kwa Manabii wake mbalimbali lakini kwa majina tofauti.
Mungu alivyojitambulisha kwa Nabii Ibrahimu (a.s.)
Kulingana na mafundisho ya Biblia, Mungu alijitambulisha kwa Nabii Ibrahimu (a.s.) kama "Mungu Mwenyezi". Ukweli huu unathibitishwa na andiko lifuatalo:
"Abrahamu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, BWANA akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu". (Mwanzo 17:1)
Mungu alivyojitambulisha kwa Nabii Isaka (a.s.)
Mafundisho ya Biblia pia yanaeleza kuwa Mungu alijitambulisha kwa Nabii Isaka (a.s.) kwamba ndiye Mungu yule yule wa Baba yake (Nabii Ibrahimu a.s.) kama tunavyojifunza maandiko yafuatayo:
"Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; ... BWANA akamtokea usiku ule ule akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana Mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu". (Mwanzo 26:18,24).
Mungu alivyojitambulisha kwa Nabii Yakobo (a.s.)
Vile vile kulingana na mafundisho ya Biblia, Mungu alijitambulisha pia kwa Nabii Yakobo (a.s.), kama maandiko yafuatayo yanavyobainisha ukweli huu:
"Mungu akamtokea Yakobo tena, aliporudi kutoka padan - aramu akamwambia, Jina lako ni Yakobo, hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli. Mungu akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uzidi ukaongezeke". (Mwanzo 35:9-11).
Mungu alivyojitambulisha kwa Nabii Musa (a.s.)
Tofauti na alivyojitambulisha kwa Manabii wake wa kabla ya Nabii Musa (a.s.), Biblia inafundisha kuwa Mungu alijitambulisha kwa Nabii Musa (a.s.) na kwa Waisraeli wengine kwa majina ya "Yehova" na "BWANA".
Kuhusu jina la Yehova, andiko lifuatalo linathibitisha kama ifuatavyo:
"Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni Yehova". (Kutoka 6:2).
Kuhusu BWANA, maandiko yafuatayo yanabainisha:
"Ilikuwa siku hiyo BWANA aliponena na Musa katika nchi ya Misri, BWANA akamwambia Musa, akasema, Mimi ni BWANA, mwambie Farao mfalme wa Misri maneno yote nikuambiayo". (Kutoka 6:28-29).
Mungu alivyojitambulisha kwa Nabii Daudi (a.s.)
Maandiko ya Biblia yanaonyesha pia kuwa Mungu alijifunua na kutambuliwa na Nabii Daudi (a.s.) kwa majina ya Yehova, Yahu na BWANA.
Kuhusu jina Yehova, Nabii Daudi baada ya Mungu kumfunulia, alitangaza kwa kusema:
"Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako Yehova, ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote". (Zaburi 83:18)
Kuhusu jina Yahu, Nabii Daudi pia alifunuliwa na kusema:
"BWANA, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee Yahu?" (Zaburi 89:8)
Ama kuhusu BWANA, Nabii Daudi vile vile alisema:
"Kwa kuwa BWANA ni Mungu mkuu, Na mfalme mkuu juu ya miungu yote". (Zaburi 95:3).
Mungu alivyojitambulisha kwa Nabii Isaya (a.s.)
Kulingana na mafundisho ya Biblia, Mungu kupitia kinywa cha Nabii Isaya (a.s.) alijitambulisha kwa jina la BWANA. Aidha, kwa upande mwingine, maandiko ya Biblia yanaonyesha kuwa Mungu pia alijifunua kwa Nabii Isaya kwa jina la BABA.
Kuhusu kujitambulisha kwa jina la BWANA, Mungu mwenyewe alisema:
"Mimi ni BWANA, ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu". (Isaya 42:8)
Ama kuhusu jina la BABA, Nabii Isaya alisema:
"Lakini sasa, Ee BWANA, Wewe U baba yetu, sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu, sisi sote tu kazi ya mikono yako". (Isaya 64:8)
Mungu alivyojitambulisha kwa Nabii Yesu (a.s.)
Sawa sawa na Nabii Isaya (a.s.), Biblia inafundisha kuwa Mungu alijifunua na kutambuliwa na Nabii Isa au Yesu (a.s.) kwa majina ya BABA MTAKATIFU na BWANA.
Kuhusu BABA MTAKATIFU, Yesu naye alifunuliwa na kusema:
"Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako Baba Mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo". (Yohana 17:11)
"Yesu akamwambia. Usinishike; kwa manaa sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu". (Yohana 20:17)
Ama kuhusu BWANA, Yesu vile vile alifunuliwa na kusema:
"...Ya kwanza ndiyo hii, sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja, nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote na kwa nguvu zako zote:. (Marko 12:29-30)
Kwa ufupi, hivi ndivyo Bwana Yesu naye alivyofunuliwa na kumtambua Mungu kwa majina hayo (ya BABA na BWANA). Na kwa ujumla, ukimtoa Nabii Ibrahimu, Ishmaeli, Isaka na Yakobo (a.s.) ambao walimtambua Mungu kwa jina la Mwenyezi, Manabii waliokuja baada yao pamoja na Waisraeli kwa ujumla walimtambua Mungu kwa jina ama la Yehova, BWANA, Yahu au BABA, kama Mungu mwenyewe alivyojifunua kwao.
Mungu alivyojitambulisha kwa Nabii Muhammad (s.a.w.)
Kama alivyojifunua na kujitambulisha kwa Manabii wake wengine kwa majina tofauti (kama tulivyoona hapo juu), Mwenyezi Mungu pia hakuacha kuiendeleza kawaida (desturi) yake hiyo hata kwa Nabii wake wa mwisho, Mtume Muhammad (s.a.w.). Kwake aliamua kujitambulisha kwa jina lake kuu la Allah, akama aya ifuatayo inavyobainisha:
"Jua ya kwamba hakuna aabudiwaye kwa haki ila Allah (Mwenyezi Mungu)...". (Qur. 47:19)
Pamoja na kujitambulisha kwa jina hilo (la Allah), Mwenyezi Mungu pia hakuacha kujionyesha kuwa Yeye ndiye Mungu yule aliyewafunulia Manabii wake waliomtangulia Nabii Muhammad (s.a.w.) kama aya ifuatayo ya Qur'an inavyo mwambia Mtume Muhammad (s.a.w.) na Waislamu wengine wa umma wake kwa ujumla:
"Amekupeni sheria ya dini ile ile aliyomuusia Nuhu na tuliyokufunulia wewe na tuliyowausia Ibrahimu na Musa na Isa (Yesu)..." (Qur. 42:13).
Kulingana na aya hiyo ya Qur'an tukufu hapo juu, ni wazi kuwa Mungu - Allah ndiye Mungu - Yehova, ndiye Mungu-Mwenyezi, ndiye BWANA na ndiye Mungu-BABA aliyejifunua kwa Manabii wake wote wa kabla ya Nabii Muhammad (s.a.w.).
Hivyo basi, kwa kuzingatia uwazi wa shuhuda hizo nilizozitaja hapo juu, ni upotofu wa dhahiri kudai kwamba Yehova siyo Allah (s.w.). Kwani hata Bwana Yesu (a.s.), maandiko ya Biblia hayaonyeshi kwamba Mungu alijifunua kwake kwa jina la Yehova. Kwa hali hiyo, hatuwezi kusema kuwa Mungu - Yehova aliyejifunua kwa Nabii Musa (a.s.) siyo Mungu - Baba aliyejifunua kwa Nabii Isa au Yesu (a.s.). Au Mungu - Baba aliyejifunua kwa Yesu siyo Mungu - Mwenyezi aliyejifunua kwa Nabii Ibrahimu, Isaka na Yakobo (a.s.).
Lakini ukweli ni kwamba huyo ni Mungu yule yule mmoja ambaye anadhihirika kwa kazi, utukufu na sifa zake kamilifu, kama tutakavyokuja kuona hapo baadae katika maandiko ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu, InshaAllah.