kuna jamaa anaitwa John Baptist Ngatunga,kaandika kuhusu kuzikwa kwa Yesu,nahisi kuna mmoja wao kachungulia andiko kwa mwenzie,nikifanikiwa kupata ile post nitaicopy
FAHAMU KIDOGO KUHUSU "MSIBA WA YESU"
Na. John-Baptist Ngatunga
__________________________
Jana ilikuwa SIKU YA IJUMAA KUU ambapo Wakristo tulikuwa tunaadhimisha: Mateso, Kifo na Mazishi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kutokana na hayo, hatukutakiwa kula nyama. Leo naomba nikuoneshe jinsi Msiba wa Yesu Kristo ulivyoendeshwa Kitajiri (Yohane 19:38-42)
Watu wawili waliokuwa Matajiri sana ndio waliogharimia Mazishi ya Yesu Kristo. Wa kwanza ni YUSUFU WA ARMATAYA ambaye aligharimia KABURI na wa pili ni NIKODEMO ambae aligharimia MARASHI (Myrrh).
YUSUFU WA ARMATAYA anatajwa kwamba alikuwa mtu Msomi wa kiwango cha juu, aliyekuwa mashuhuri, mwenye kuheshimika sana na mjumbe wa ngazi ya juu katika Baraza la Utawala la Mji (Noble and honourable).
Kwa mujibu wa historia ya Wayahudi ni kwamba Wajumbe wa Mji walikuwa wanapatikana kwa vigezo takribani sita, kigezo kilichotumika kwa Yusufu wa Armataya ni kwa kuwa alitokea katika familia ya kitajiri (Noble Family).
NIKODEMO, ndiye yule aliemwendea Yesu usiku kuulizia namna ya kuurithi ufalme wa Mbinguni (Yohane 3:1-21) kisha Yesu akamwambia auze kila kitu. Japokuwa Nikodemo alikatishwa tamaa lakini kumbe aliendelea kuwa Mwanafunzi wa Yesu kwa siri kwaajili ya kuwaogopa Wayahudi.
Ndiye yule ambaye waliongea na Yesu kuhusu Kuzaliwa mara ya pili yaani kwa Maji na Roho Mtakatifu ili kuingia katika Ufalme wa Mungu (Yohane 3:3). Naye alikuwa Mjumbe wa Baraza la mji, ingawa cheo chake kilikuwa cha chini ukilinganisha na kile cha Yusufu wa Armataya.
Nikodemo alikua mfanyabiashara mkubwa, tajiri na mashuhuri katika mji ule. Kwa kimombo inaweka vizuri ya kwamba alikuwa, "Young Rich Ruler".
Nikikwambia Nikodemo alikuwa tajiri pengine unaweza usinielewe mpaka nikuoneshe thamani ya Marashi aliyogharimia kumzikia Yesu Kristo. Tunaambiwa kuwa Nikodemo alitumia Marashi (Manemane na Udi) yenye uzito wa ratli mia moja (100 pounds).
Kitu unachotakiwa kufahamu ni kuwa enzi zile, watu Mashuhuri na Matajiri wakiwemo Wafalme; walikuwa wanazikwa kwa wastani wa juu wa Marashi ya ratli 40 pekee. Kwa hiyo, utaona kwamba Marashi ya Yesu yaligharimu karibu mara mbili na nusu ya ilivyozoeleka kwa watu maarufu.
Twende kwenye hesabu:
Kwa utafiti uliofanywa katika masoko ya Marashi duniani ni kwamba, mchanganyiko wa marashi ya Manemane na Udi, wa uzito wa ratli 100, kwa bei ya sasa unagharimu takribani dola 140,000 hadi 210,000. Hizi ni sawa na takribani shilingi za Kitanzania (140,000 × 2324.80 = 325,472,000) hadi (210000 × 2324.80 = 488,208,000) yaani ni kati ya Milioni 325,472,000 na Milioni 488,208,000.
Yaani Nikodemo alitoa mchango wa msiba wa Milioni 500 kasoro za wakati ule! Usisahau kwamba msiba wenyewe ulikuwa wa ghafla maana hawakutegemea wala kuamini kama Yesu angeuawa, "kiukweli-kwelii".
Hebu fikiria vizuri, msiba wa ghafla Nikodemo akamwaga karibu milioni mia tano za wakati ule. Je, kungekuwa na kujiandaa!!!!!?
Shikamoo, Nikodemo............!!!
Sijajua kama inakuingia akilini kama inavyotakiwa unapoambiwa Yusufu wa Armataya alikuwa mtu tajiri, mashuhuri, mwenye cheo na mwenye kuheshimika!!! Labda nikuoneshe thamani ya kaburi alilotoa kuuzikia mwili wa Yesu, huenda ukaelewa.
Kaburi alimozikwa Yesu tunaambiwa lilikuwa na sifa kubwa tatu: Lilikuwa Bustanini, Lilikuwa Jipya (yaani hajazikwa Mtu ndani) na Lilikuwa Limechongwa mwenye Mwamba (Yoh. 19:41).
Makaburi ya hivi walikuwa wanazikiwa Wafalme, Viongozi wakubwa wa Serikali na Matajiri wachache. Rekodi zinathibitisha kwamba makaburi ya aina na mtindo hii yalikuwa yana gharama kushinda bei ya nyumba na viwanja pale Yerusalem enzi zile.
Ukitaka kupata picha halisi angalia bei ya viwanja na nyumba pale Yerusalem hata sasa. Na hata tangu enzi za Abrahim viwanja vilikuwa ni ghali sana pale Yerusalem.
Bei ya kiwanja cha kawaida cha ukubwa wa mita square (msq) 3,000 pale Jijini Yerusalem, kwa leo, sio chini ya shilingi za Kitanzania Bilioni moja (1,000,000,000). Hivyo, utaona kwamba eneo alilolitoa Yusufu wa Armataya kumzikia Yesu lilikuwa na thamani ya mamilioni ya shilingi kwa wakati ule.
Anyway; kwa leo sitaki kukupigia hesabu za marashi waliyobeba wale wanawake walioamka asubuhi kwenda kumpaka Yesu kutokana na kuchelewa jana yake wakati kina Nikodemo wakizika.
Kumbuka kwamba katika wale wanawake walikuwemo wale ambao ndio walikua wadhamini wakubwa wa huduma ya Yesu (kwa mali zao). Kwa hiyo uwe na uhakika kwamba thamani ya marashi waliyoyabeba nikikupigia hesabu yake utashangaa mwenyewe!
Nataka kusema nini?
Suala la kumtumikia Mungu na kujitoa kwa huduma za Kiimani na Kiroho usilipe sababu za kulikwepa. Hao watu wawili ni watu maarufu, Matajiri, Wasomi, nk. Lakini waliona hayo yote sio kitu mbele ya Suala la kujitoa kwa Mungu.
Wewe na Mimi ambao sio maarufu na hatujulikani hata mtaa wa pili labda tu siku hizi sura zetu walaunzinaonekana Mitandao. Hatuna utajiri ila tumejaa umasikini na ukurutu, shida na maisha yetu ni magumu yanayokandamizwa na 'vifurushi' na 'tozo' za hapa na pale. Tukija kwenye usomi ndio usiseme; Elimu yetu inayumbayumba na kukatikati utadhani 'Umeme wa Mgao'
Lakini tukiambiwa tujitoe kwenye mambo ya Kanisani tumekuwa wabishi, wagumu na wazito utadhani vifurushi vya 2G. Tumekuwa wepesi sana kushabikia mambo ya kipuuzi. Tena tuna Moyo wa haraka kukimbilia mambo ya kidunia utadhani yanavyoisha mabando ya internet.