Mjadala kuhusu mikopo ya vijana inayotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Vijana umeendelea kushika kasi, huku wadau wakitoa maoni yanayolenga kuboresha ufanisi na upatikanaji wa fursa hizo. Moja ya hoja kuu ni mapitio ya vigezo vinavyotumika kuwafikia wanufaika.
Akizungumzia mjadala huo, Vian Vianelly ambaye ni mdau wa maendeleo ya vijana amependekeza kuongezwa kwa ukomo wa umri wa vijana hadi miaka 40, akieleza kuwa hatua hiyo itawezesha kundi kubwa zaidi kunufaika na mikopo yenye masharti nafuu.
Amesema mabadiliko hayo yanaendana na uhalisia wa kijamii na kiuchumi, ambapo vijana wengi huanza kujitegemea wakiwa na umri mkubwa zaidi.
Amebainisha kuwa mifumo ya elimu na changamoto za ajira husababisha Watanzania wengi kuingia rasmi kwenye shughuli za kiuchumi wakiwa na umri wa miaka 30 na kuendelea, hivyo ukomo wa sasa wa miaka 35 unawaacha nje wengi wanaostahili.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa utoaji wa mikopo kufanyika kwa umakini na ufanisi, akipendekeza pia mgawanyo wa wanufaika katika makundi mawili, wale wenye biashara tayari na wanaoanza, ili kuboresha usimamizi, kuongeza tija, na kuhakikisha urejeshaji wa mikopo unakuwa endelevu.