JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 685
- 1,124
Novemba 27, 2024, Watanzania walishiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa lengo la kuchagua viongozi wa vijiji, vitongoji, na mitaa. Uchaguzi huu, kama chombo muhimu cha kukuza ushiriki wa wananchi katika uongozi wa maeneo yao, umekuja na matukio mbalimbali yanayostahili kujadiliwa kwa kina.
Maswali Muhimu:
- Mchakato wa Uchaguzi: Je, uchaguzi ulikuwa wa haki na huru? Kuna changamoto zipi zilijitokeza kabla, wakati, na baada ya upigaji kura?
- Ushiriki wa Wananchi: Je, mwitikio wa wananchi ulikuwa wa kuridhisha? Ni kwa nini baadhi ya watu hawakushiriki ipasavyo?
- Nafasi ya Vyama vya Siasa: Vyama vya siasa vilipata nafasi gani katika kushawishi uchaguzi huu? Je, wagombea wa vyama vyote walipata haki sawa?
- Ushiriki wa Vijana na Wanawake: Je, makundi haya yalihamasishwa ipasavyo kushiriki au kugombea nafasi za uongozi?
- Mafanikio na Mapungufu: Ni nini kilichofanikiwa, na ni maeneo gani yanahitaji kuboreshwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025?
- Mustakabali wa Demokrasia: Je, uchaguzi huu umeonesha ukuaji wa demokrasia nchini au bado kuna changamoto kubwa zinazohitaji kushughulikiwa?
Tunakaribisha mawazo, uzoefu, na mapendekezo yenu. Tafadhali shiriki kwa hoja za msingi na mifano halisi ili kujenga mjadala wenye tija kwa maendeleo ya nchi yetu.
Kushiriki mjadala kupitia XSpaces ya JamiiForums ingia hapa
Kupata taarifa na matukio ya kimkoa kuhusu Uchaguzi Serikali za Mitaa ingia hapa: LGE2024 - Special Thread: Orodha ya Mijadala ya Mikoa yote Tanzania Bara inayoshiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024
========================================
MAONI YA WACHANGIAJI WALIOPO KWENYE MJADALA
Esther Thomas - Naibu Katibu Mkuu ACT Wazalendo Bara
"Kwa kilichotokea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, imeonesha hatuko tayari kwa Demokrasia ya Nchi huru na Haki"
"Mambo yalivyoonekana katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yametuonesha tuna safari ndefu sana kufikia safari yetu ya kuwa Nchi ya Demokrasia"
"Uchaguzi ulisimamiwa kwa asilimia kubwa na Watumishi wa Umma, hivyo unapozungumzia watu waliofanya hujuma ni Watumishi wa Serikali, mfano Watendaji wa Kijiji, Walimu, Jeshi la Polisi"
"Wananchi wanapaswa kufahamu wahujumu wa Uchaguzi uliopita ni Watumishi wa Umma na aliyeharibu uchaguzi wote ni Serikali, kwa kuwa msimamizi wa Uchaguzi ni Idara ya Serikali"
"Kilichofanyika wakati wa Uchaguzi kinaonesha hata TAMISEMI wenyewe hawakujiandaa, kulikuwa na baadhi ya vitu havina maandalizi"
"Pia, ujumbe mwingine ni kuwa Serikali inaonesha haipo tayari kwa maendeleo ya Wananchi, walichokifanya ni kuwa wao walihitaji kupata madaraka na sio kwaajili ya Wananchi"
"Kutokea kwa Vitisho, Kutekwa, Kupigwa yanaonesha kuwa Wananchi wanafikishiwa ujumbe wa kutosema chochote au kulalamika, badala yake wawe tayari kutawaliwa"
"Viongozi walioteuliwa (Nawaita hivyo kwa kuwa sioni kama wamechaguliwa) sioni kama wanaweza kuwa na ujasiri wa kusimama hadharani na kuzungumzia maendeleo ya maeneo yao kwa kile kilichotokea katika Uchaguzi"
"Mtu anapokaa mezani kuzungumza na wewe kutafuta utatuzi sio dhaifu, hilo ndilo ambalo linaonekana upande wa pili kuwa kile ambacho kinafanyika wanadhani sisi ni dhaifu"
"Unapoona suala la utekaji unahisi halikuhusu, siku likitokea kwako au kwa mtu wako wa karibu au mtu unayemfahamu ndio utafahamu kuwa ni jinsi gani watu wanapata maumivu"
"Yote hayo yanatokana na kukosekana kwa Uwajibikaji wa Kikatiba na kufinywa kwa Demokrasia"
"Wasifurahie kushinda kwa Asilimia 99 wakati wanashindana kukimbia na mtu ambaye wamemkata miguu, watambue kuwa ipo siku huyo ambaye amekatwa miguu atapona na ndipo watatambua kuwa walikuwa wanashindana na Mtu wa aina gani"
John Pambalu - Mwenyekiti BAVICHA Taifa
"Kilichotokea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 pamoja na matukio yake ikiwemo kutumia Wanafunzi kujiandikisha Kupiga Kura, Wizi wa Kura, Mauaji, imetufanya CHADEMA kutoa wito kwa Wadau mbalimbali kuwa ni wakati sahihi kuunganisha nguvu ili kupambania Katiba Mpya"
"Wadau wote kwa pamoja tunahitaji kuwa pamoja na kupata Katiba Mpya, ambayo italeta Haki na Usawa kwa watu wote"
"Hilo likiwa gumu basi tufanye mabadiliko madogo (minimum reform), ili tushughulikie masuala yetu Kikatiba, kwa kuwa inawezekana ikawa ngumu kutimiza hilo kabla ya Uchaguzi ujao"
"Inahitajika presha ya Umma katika kudai mabadiliko, ili Watawala wajione hawatakuwa salama na utulivu kama hakutakuwa na mabadiliko ya Katiba"
"Ninapozungumzia nguvu ya Wadau inatakiwa wale wote wanaofanya uhuni wakiwa katika nafasi Serikalini wajue kuwa Umma unahitaji mabadiliko na wajue Wananchi wanahitaji Uchaguzi Huru na Haki"
"Uchaguzi uliopita inawezekana tuliwaonesha kuwaamini na tukajisahau lakini kilichotokea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (2024) kimeonesha hawa watu ni walewale"
"Tunatakiwa kuunganisha nguvu tukiweka pembeni itikadi za Kisiasa na nyingine, zikiwemo za Kiimani ili tuwe kitu kimoja"
"Historia ya Vyama vya Upinzani kupinga Vyama vingine vya Upinzani inaonesha imekuwepo kwa miaka mingi, ilikuwa hivyo pia hata wakati wa harakati za kudai uhuru wa Nchi mbalimbali"
"CHADEMA tumesimamisha Wagombea lakini wamekutana na Upinzani kutoka kwa Vyama kadhaa vidogo vya Upinzani, ACT pia nao walikutana na changamoto kama hiyo"
"Kuna mauaji yametokea wakati wa Uchaguzi, lakini huwezi kusikia wanaoona Uchaguzi ulikuwa wa Haki wanadema chochote katika hilo, wanatafuta kile wanachoona wao kinafaa"
"Uchaguzi huu ulikuwa unatuma ujumbe kuwa bila kuwa CCM huwezi kupata Madaraka, ndio maana unaona wameshinda kwa 99%"
"Napongeza baadhi ya Watu mashuhuri wakiwemo kina Mzee Butiku na Viongozi wengine wa Dini walijitokeza na kukemea kilichofanyika wakati wa Uchaguzi (Serikali za Mitaa 2024), kuwa haukuwa sawa na Haki haikutendeka"
"Natoa wito kuwa kuna haja ya kuwa Wamoja na kuunganisha nguvu kujadiliana kuhusu Haki na Demokrasia kwa kuwa ni suala la Kitaifa, suala la uwepo wa Vyama vya Upinzani vinavyoweza kupinga vingine vya upinzani hilo lipo kihistoria"
Idd Mkanza - Katibu Mtendaji Jumuiya ya Vijana wa CUF
"Uchaguzi uliopita (Serikali za Mitaa 2024) CCM imeshinda kwa 99% lakini kuna Vijiji vingi ambapo mbali na wale walioenguliwa kulikuwa na maeneo mengi ambapo Wapiga Kura waliingia wakakuta wagombea ni wa Chama kimoja"
"Kuna watu wengi wamekatwa kwa makusudi. Wanatumia muda mwingi kufanya Kampeni lakini mwisho wake hakuna wanachokipata"
"Nadhani ni wakati wa Jumuiya za Kimataifa kusitisha misaada Nchini kwa kuwa tunachokifanya ni kuwadanganya wao na kuidanganya Dunia"
"Mfano; Wilaya ya Mtwara Vijijini, milango ilifunguliwa Saa Mbili asubuhi hadi saa Sita Mchana, kulikuwa na Kura batili na Mamlaka za Ulinzi zilihusika kusaidia hilo"
"Tunahubiri Demokrasia wakati kuna vitu vingi ambavyo haviendani na uhalisia, sisi kama Chama tunatarajia kutoa tamko kuhusiana na kilichotokea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024"
"Umuhimu wa kuwa na Serikali za Mitaani ni kumfanya Mwananchi awe karibu na Serikali yake na kushiriki katika kufanya maamuzi"
Majalio Kyara - Katibu Mkuu Sauti ya Umma
"Tunatakiwa kumshukuru Mungu kwa kumaliza Uchaguzi kukiwa na hali ya Amani na Salama"
"Niwapongeze TAMISEMI kwa kuwa walitushirikisha kuanzia mwanzo, japokuwa katika utekelezaji kuna mambo ambayo hata sisi yalitubana"
"Haiwezekani jambo kubwa kama hili likose changamoto, lakini kinachotakiwa kuangaliwa ni kuwa changamoto ni kubwa kiasi gani?"
"Pamoja na hivyo tunapokuwa tunalalamika tunatakiwa kujiuliza pia, Je, hakukuwa na mazuri? Au kila kitu kilikuwa kibaya?"
"Kuna tukio lilitokea Muheza, Jeshi la Polisi lilitutaka tuondoke sehemu tulipokuwa tunapiga Kampeni, baadhi ya Watu wakasema tusiondoke, tubaki ili tupate ‘kiki’ kwa kubishia maelekezo"
"Hatukufanya hivyo, tulifuata maelekezo kwa kuwa tulikiuka, hatukufuata maelekezo mapema, tukalazimika kuondoka hapo kwa amani"
"Jambo lingine ni kuwa sisi Wanasiasa tunatakiwa kuwa makini na maamuzi yetu wakati wa kutunga Sheria na Kanuni"
"Wenzetu CHADEMA walikuwa wanajiona wanaenda wao tu, walisema Vyama ni Viwili tu CCM na CHADEMA, sasa hivi wanarudi nyuma na wanataka ushirikiano, walitaka kupambana wao lakini tungeweza kwenda pamoja tangu kipindi hicho tungefika mbali"
"Mazingira ya kujitenga na kujiona bora yalikuwepo tangu wakati wa UKAWA, hakukuwa na umoja, kulikuwa na mazingira ya kujitenga na ndio maana hakukuwa na mafanikio"
"Kauli ya CHADEMA Taifa kuhusu Uchaguzi (wa Serikali za Mitaa 2024) imesema haukuwa Huru na wa Haki, wakati huo CHADEMA Kinondoni walisema Uchaguzi ulienda vizuri"
"Matukio ya Watu kuuawa wakati wa Uchaguzi yamekuwa yakitokea sehemu tofauti hata katika Nchi nyingine, tunachotakiwa kujiuliza ni je, kulikuwa na mazuri mangapi na mabaya mangapi, kisha ndio tunaweza kutoa kauli kwa ujumla"
"Kuna wakati sisi Wanasiasa tunajichanganya, unamsikia mtu anasema Uchaguzi huu usisimamiwe na TAMISEMI, usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi, lakini kuelekea Uchaguzi Mkuu wanasema, Uchaguzi usisimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi. Unajiuliza hawa watu wanataka nini? Huo ndio ninaosema ni ubinafsi"
"Viongozi wanasahau kuwa katika Chama kila mmoja anafiti kwa sehemu yake, ndio maana ninasisitiza umoja wa Vyama, wao (CHADEMA) walikuwa wanataka kufanya kila kitu wao ndio maana wameenda imefika hatua unaona wanashindwa kuendelea, wanaturudia"
"Kuna siku nilimwambia Mnyika (CHADEMA), kuwa nyie mnafanya Maandamano lakini mnafeli, na nikamwambia mbona mnafeli hata kabla ya kuanza maandamano?"
"Kuhusu Takwimu kuwa kuna Vyama vya Upinzani vilipinga Vyama vingine vya Upinzani, hizo ni historia tu, sasa hivi tunatakiwa kuishi tulivyo kulingana na uhalisia"
Thobiasi Mgisha (Mdau)
"Tuna mchakato wa Uchaguzi ambao hauna mazingira ya Haki, Wapinzani wanatakiwa kujipanga na kujianda kutokana na hali halisi iliyopo, kwa kuwa CCM haiwezi kujitokeza na kusema "Tumeshindwa Uchaguzi"
"Kote Duniani, sehemu wanapopambania Haki dhidi ya Chama Tawala, Dola ya Wapinzani ni Wananchi, hiyo ipo hivyo katika Nchi nyingi"
"Hali ilivyo inaonesha Wapinzani hawajawapa Wananchi elimu na uelewa wa nini wanatakiwa kukifanya, wanatakiwa kutengeneza msingi wa Umma kuelewa umuhimu na nguvu yao"
"Katika Uchaguzi uliopita (Serikali za Mitaa), kulikuwa na upigaji kura wa Ndio na Hapana, jiulize huo upande wa Hapana unasimamiwa na nani?"
"Mara baada ya Rais Samia kuruhusu uwepo wa Mikutano ya Kisiasa ambalo ni suala la Kikatiba, napongeza ACT Wazelendo na CHADEMA kwa kuwa ndani ya muda mfupi waliweza kuwa ‘active’ na kuwajibika kufanya shughuli zao inavyotakiwa"