Maaskofu wametimiza wajibu wao kama watumishi wa kanisa. Inaelekea Musiba ameshalitambua na kujutia sana kosa lake, ijapokuwa amechelewa sana kuomba msamaha kwa Membe, na kwa wengine. Ameng'amua njia iliyobakia pekee kwake ni kuwatafuta viongozi wa kidini wenye ushawishi ili wapate kumuombea msamaha kwa Membe.
Sisi sote ni binadamu, na wote tunatenda makosa. Kama Mungu angalituhesabia makosa yetu tuyafanyayo kila iitwapo leo, hakika hakuna miongoni mwetu ambaye angestahili kuishi. Lakini ni vyema Musiba asitake kuuzunguka mbuyu, atoke hadharani tu na kumuomba msamaha Membe na wengine wote aliowakosea, tena kwa namna ile aliyoifanya kupitia vyombo vyake vya habari.Natambua Membe ni muumini mzuri, na tena ana kicho mbele ya Mungu wake. Anitambua amri kuwa anapaswa kumpenda jirani yake kama vile ambavyo anajipenda yeye mwenyewe. Ndiyo! Ni kweli alikosewa mno na Musiba, na dunia yote inatambua hivyo, na hata mahakama imethibitisha hivyo, lakini kama binadamu yeyote yule mwenye nafsi hai, anaweza kutafakari nukuu ifuatayo kutoka katika kipande cha Neno la Injili,
MATHAYO 18
15 “Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwambie kosa lake mkiwa ninyi wawili peke yenu. Akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako.
16 Kama hatakusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili kusudi wawepo mashahidi wawili au watatu wa kuthi bitisha jambo hilo.
17 Akikataa kuwasikiliza, liambie kanisa. Kama akikataa kulisikiliza kanisa, basi mhesabu yeye kama ni mpagani au mtoza ushuru.