Mende ni maarufu kwa ukakamavu wao, na mara nyingi hutajwa kuwa ndio walionusurika zaidi katika vita vya nyuklia. Wengine hata wanadai kwamba wanaweza kuishi bila vichwa vyao.
Suala la mende kuendelea kushi hata baada ya kukatwa kichwa lipoje?
- Tunachokijua
- Mende ni miongoni mwa wadudu wanaopatikana katika makundi mengi yanayotajwa kuwa zaidi ya 4600. Wadudu hawa husifika kwa kuwa na vichwa bapa na huwa na antena ndefu kichwani.
Aidha, mende wa kiume huwa na mabawa, lakini mende wa kike kwa aina nyingi huwa hawana mabawa na hutaga mayai.
Mende aweza kuishi hata baada ya kukatwa kichwa?
wanasayansi wanathibitisha kuwa mende anaweza kuendelea kuishi kwa siku kadhaa baada ya kukatwa kichwa.
Ili kuelewa ni kwa nini mende na wadudu wengine wengi wanaweza kustahimili kukatwa kichwa, inabidi kwanza kuelewa ni kwa nini binadamu hawezi.
Kwanza kabisa, kukata kichwa kwa binadamu husababisha kupoteza damu na kushuka kwa shinikizo la damu hupunguza usafirishaji wa oksijeni na virutubisho muhimu kwa tishu za mwili.
Kwa kuongezea, wanadamu hupumua kupitia midomo au pua zao na ubongo hudhibiti kazi hiyo muhimu, kwa hivyo kupumua kungeacha. Zaidi ya hayo, mwili wa mwanadamu hauwezi kula bila kichwa, na hivyo kuhakikisha kifo cha haraka kutokana na njaa.
Lakini mende hawana msukumo wa damu kama watu. Hawana mtandao mkubwa wa mishipa ya damu kama ile ya wanadamu, au mishipa midogo zaidi ya damu ambayo huhitaji shinikizo kubwa ili kutiririsha damu.
Mende huwa na mfumo wa wazi wa mzunguko wa damu, ambao kuna shinikizo kidogo sana. Baada ya kuwakata vichwa vyao, mara nyingi shingo zao huziba haraka kwa kugandisha damu.
Sababu muhimu zinazowafanya waendelee kuishi
Mende hupumua kupitia matundu madogo (Spiracles) yanayopatikana katika kila sehemu ya mwili hivyo hawahitaji kichwa ili wapumue.
Zaidi, ubongo wa mende haudhibiti kupumua na damu haibebi oksijeni katika mwili wote. Badala yake, spiracles hupitisha hewa moja kwa moja hadi kwenye tishu kupitia seti ya mirija maaalum ambayo kisayansi huitwa tracheae.
Mende pia ni wadudu wenye damu baridi hivyo huhitaji chakula kidogo sana kuliko wanadamu ili waweze kuishi na kutengeneza joto lao la kiasi mwilini. Sifa hii inamfanya mende aweze kuishi kwa wiki kwa chakula alichokula siku moja.
Mfumo wa upumuaji wa Mende
Mfumo wa neva zao za mwili upo tofauti, kwa hivyo bila ubongo, mwili bado unaweza kufanya kazi.
Kukatwa kichwa kwa mende kunaweza kuonekana kuwa mbaya, lakini wanasayansi wamefanya majaribio mengi ya aina hii na kuhakiki kuwa wanaweza kuishi hata kwa zaidi ya wiki 1 bila kichwa.
Majaribio mengi yaliyofanyika bado hayajatoa hitimisho la idadi ya siku maalum anazoweza kuishi bila kichwa.
Hata hivyo, sehemu nyingi zinataja kuwa wadudu hawa wanaweza kuishi hadi siku 7 baada ya kukatwa kichwa chao wakiwa bado wapo hai.