Mgombea binafsi aumiza vichwa vigogo: Raia Mwema
UAMUZI Mahakama kuruhusu kuwapo mgombea binafsi unaelezwa kuwa tishio na sasa unaangaliwa kwa jicho la karibu na wanasiasa na wafanyabiashara wanaoweza kuamua kuingia katika kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa, Raia Mwema limegundua.
Wakati Mahakama ikiamini hakuna sababu za msingi za kuzuia mgombea binafsi, wabunge waliozungumza na
Raia Mwema, wanaamini kumchagua mgombea binafsi katika ubunge au urais ni kujimaliza na wengine wakisisitiza, kilio cha umma kutaka mgombea binafsi ni dalili za kufeli kwa vyama vya siasa vilivyopo nchini.
Wanaamini ni dalili za kufeli kwa vyama vya siasa vilivyopo kutokana na vyama hivyo kuzongwa na rushwa, ubabaishaji, uonevu na mizengwe isiyo na mantiki wala maslahi kwa Taifa.
Tayari wananchi mbalimbali wameanza kuwaangalia wanasiasa na wafanyabiashara kwamba sasa vyama vya siasa vitalazimika kuwa na nidhamu na kuacha kuwatisha kwa kuwa kuna nafasi ya watu kuingia katika siasa bila kupitia vyama.
Wanaotajwa kuwa uamuzi huo unazidi kuwapa nguvu ni pamoja na wanasiasa wa pande zote zinazovutana ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na hata ndani ya vyama vikuu vya upinzani, ambavyo vilikuwa vikiwatisha baadhi yao kwamba vitawatimua kabla ama wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Miongoni mwa wanasiasa wanaotajwa ni pamoja na Spika wa Bunge Samuel Sitta, Waziri Mkuu wa zamani aliyejiuzulu Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, pamoja na wabunge wanaowaunga mkono wanasiasa hao.
Wengine wanaotajwa kuwa tishio wakiamua kugombea bila kupitia vyama ni pamoja na mawaziri wakuu wastaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye, ambao wote wanaelezwa kuwatisha wanasiasa wa sasa.
Kwa upande wa wafanyabiashara, wanaotajwa ni pamoja na Reginald Mengi, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, ambaye amekuwa akisema kuwa mwanachama wa CCM huku baadhi ya viongozi wa chama hicho wakitaka kumhusisha na vyama vya upinzani.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ni mmoja wa wanasiasa wanaotajwa kuweza kuamua kuingia katika uchaguzi bila kupitia chama chochote kutokana na kuwapo misuguano kati yake na chama chake cha CHADEMA.
Akizungumzia uamuzi huo, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, amesema: kesi bado na tatizo wagombea binafsi waje au la, tatizo mahakama inapata wapi power ya kuamua suala linalogusa mabadiliko ya Katiba. Mwenye mamlaka hayo ni Bunge.
Wabunge waliozungumzia uamuzi huo ni pamoja na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye alisema anaamini kuwa kilio cha baadhi ya Watanzania kutaka mgombea binafsi ni dalili za wazi za vyama vya siasa vilivyopo kutokuwa katika kiwango cha juu cha utendaji, kisichotiliwa shaka na wananchi.
Hata hivyo, kwa upande mwingine mbunge huyo anaeleza kuwa mgombea binafsi si suala linaloweza kuwa na mshindo mkubwa katika Bunge au Serikali.
Katika nchi ambazo mfumo wa katiba unaruhusu mgombea binafsi sijawahi kuona
serious impact inayotokana na wagombea binafsi, kwamba robo tatu ya Bunge kwa mfano iwe ni wagombea binafsi.
Nadhani wakati mwingine kunakuwa na uwoga usio wa lazima kuhusu kuwapo kwa wagombea binafsi, lakini ukitazama zaidi suala hili nchini unaweza kujiuliza kwa nini kuwa na kilio kikubwa cha mgombea binafsi?
Jibu ni kwamba, kilio hicho ni dalili za wazi za kushindwa kwa mifumo ya vyama vya siasa nchini.
Demand ya mgombea binafsi ni dalili ya udhaifu mkubwa wa mifumo ya uendeshaji vyama.
Unajua mfumo wetu ni wa demokrasia ya uwakilishi wa kibunge, mtu anachaguliwa kuwa mbunge kuwakilisha na anawajibika kwa chama anachotoka. Sasa unapochagua mgombea binafsi, ni kupotosha dhana ya uwakilishi kwa mfano, huyo mgombea akikaidi ahadi zake au kufanya masuala ya ovyo, mtamwajibisha vipi au mtakwenda kwa mkewe?
Kwa hiyo nasema mgombea binafsi si mfumo wa maana kwa kuwa hau-
reflect real democratic value, kilio hiki kipo kwa kuwa tu vyama vya siasa vilivyopo vimezongwa na uonevu, ukosefu wa uwajibikaji, rushwa, na ubabaishaji.
Naye Mwenyekiti Mstaafu wa Umoja wa Wanawake wa CCM- UWT na Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah, akizungumzia mgombea binafsi anahoji: Kwa nini watu walitaka mfumo wa vyama vingi? Na huyo mgombea binafsi atakuwa na sera zipi?
Anasema; Mimi naona mfumo mzuri na wa kidemokrasia zaidi ni kuwa na wagombea kutoka vyama vya siasa, mgombea binafsi ni ubinafsi.
Chama ndiyo kinatoa ahadi na ni jukwaa zuri la kumwajibisha kiongozi wake kwa niaba ya wananchi. Mimi hadi sasa sielewi na akili ya kawaida ya kuzaliwa inakataa kabisa, huyu mgombea binafsi atasimamia nini, na akiamua kufanya mambo yake binafsi itakuwaje. Hili suala halina maana yoyote, anasema Anna Abdallah aliyepata kuwa Waziri katika wizara mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia anasema; Kuchagua mgombea binafsi ni kujimaliza kabisa, nani atamsimamia huyu na hasa utekelezaji wa ahadi zake. Ninavyojua chama cha siasa ndiyo chenye sera na katiba.
Kuchagua mgombea binafsi ni sawa na kuchagua kiongozi asiye na mfumo rasmi wa kudhibiti nidhamu yake. Na zaidi hakuna
forum ya kumuadabisha anapoonekana kuyumba katika utekelezaji wa ahadi au kimaadili,.
Naye Mbunge Ludovick Mwananzila anaamini kuwa Tanzania haina haja ya kuwa na mgombea binafsi kwa wakati huu, kwa kuwa mazingira halisi ya kisiasa yanakataa.
Anasema: Nadhani tunataka vitu ambavyo bado hatujawa tayari kwa kiwango cha kuridhisha. Kuna vyama vya siasa 19, hivi kweli kuna Watanzania wanaokosa hiari ya kugombea kupitia chama chochote kati ya hivyo?
Alipoulizwa kwamba suala la mgombea binafsi ni la kikatiba kwa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza kuwa kila raia ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa, Mwananzila alisisitiza; Haki hiyo inalindwa hata katika mfumo usio wa mgombea binafsi, kuna hivyo vyama 19 nimekwambiasasa si kweli mtu anakosa haki ya kupiga na kupigiwa kura hapo.
Kwa upande wake, Mbunge Richard Ndassa anasema mgombea binafsi si suala la maana sana kwa nchi inayotaka kupiga hatua katika tafsiri pana ya kidemokrasia.
Alisema: Hili ni suala la kuminya demokrasia. Demokrasia nzuri zaidi ni ile ya kwanza kuchujwa na wenzako, kushirikiana na wenzako kuanzia kwenye chama na baadaye kwenye umma.
Alipoulizwa kama mgombea binafsi ni suala linaloweza kubomoa vyama vya siasa kikiwamo chama chake cha CCM, alisema; Si rahisi iwe hivyo. Wananchi watapenda chama chenye ilani, ili wakishindwa kufukuzana na mgombea asiyewajibika basi wanakigeukia chama ambacho kilimdhamini huyo mgombea.
Kati ya viongozi wa CCM wanaounga mkono mgombea binafsi ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa sasa, Pius Msekwa, ambaye wiki kadhaa baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Butiama, alizungumza na gazeti moja la kila siku akisema anaunga mkono mgombea binafsi kwa kuwa huko ni kumuenzi kwa vitendo, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye ingawa hakuamini kuwa mgombea binafsi ni demokrasia bora zaidi kuliko vyama vya siasa, lakini hakuona mantiki ya kuzuia suala hilo.
Suala la mgombea binafsi lilifikishwa mahakamani na Mwenyekiti wa Chama Cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, akitaka aruhusiwe na Mahakama kukubaliana na hoja zake na hivyo kutoa hukumu inayoruhusu.
Hata hivyo, Serikali imekuwa ikionyesha kutokukubaliana na suala hilo kwa kutumia mianya ya kisheria na kuamua kukataa rufaa na rufaa hiyo kusikilizwa na Majaji saba, wakiongozwa na Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani.