Date::10/20/2008
Walimu: Hatutazungumza tena na serikali
Na Mwandishi Wetu
Mwananchi
RAIS wa Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mukoba amesema kuwa hakuna mtu anayeweza kusema kuwa madai yao yametekelezwa, isipokuwa walimu wenyewe na kwamba hawatarudi kwenye mazungumzo kwa kuwa hatua hiyo ilishapita.
Walimu wanaidai serikali zaidi ya Sh16 bilioni, ambazo ni malimbikizo ya posho zao mbalimbali, fedha za nauli. Pia wanadai kupandishwa madaraja, lakini serikali katika taarifa yake ya Oktoba 15 ilieleza kuwa imeshalipa zaidi ya nusu ya fedha ambazo walimu wanadai na kwamba imeshaanza kutekeleza zoezi la kupandisha madaraja walimu, huku ikieleza kuwa inaendelea na uhakiki wa madai hayo kwa wale ambao hawajalipwa.
Jana, akizungumza kwenye kipindi cha televisheni ya Star asubuhi, Mukoba alisema CWT haitarudi kwenye mazungumzo kama Jaji William Mandia alivyoshauri kwenye hukumu yake ya kuzuia mgomo kwa muda, akisema kuwa hatua hiyo ya majadiliano ilishapita.
"Tunachosubiri ni utekelezwaji wa kile tulichokubaliana na si kuanza tena mazungumzo," alisema Mukoba. "Mazungumzo yalishafanyika na kulikuwa na makubaliano ambayo serikali inatakiwa iyatekeleze.
"Nilishangaa kuona serikali inadai kuwa ilikutana na CWT na kukubaliana kuwa serikali inatekeleza madai ya walimu. Ukweli ni kwamba sisi tulikaa nao kwa lengo la kutaka kujua serikali inatekeleza vipi makubaliano yaliyofikiwa. Ni hilo tu.
"Hatukukaa na kukubaliana kuwa eti serikali imefanya juhudi za kutosha. Tulitaka kujua jinsi inavyotekeleza makubaliano kwa kuwa yalishafikiwa. Kwa hiyo hatuko tayari kurudi kwenye mazungumzo kwa kuwa kufanya hivyo itakuwa ni kurudi nyuma.
"Tunataka twende kwenye mgomo hadi hapo serikali itakapowalipa walimu madai yao.
"Serikali kudai kuwa imetekeleza madai yetu ni uongo wa mchana kweupe, walichokifanya wao ni mambo ya hovyo hovyo tu, wanadai wamepandisha walimu madaraja, lakini siyo kweli unaweza kukuta walimu walioanza kazi pamoja, mmoja kapanda madaraja mawili, mwingine hakuna, sasa huu ni utaratibu gani, upandishaji madaraja una taratibu zake,"alisema.
"Huu ni mgomo unaotajwa na sheria. Ni mgomo halali kabisa kwa kuwa umefuata taratibu zote. Hivyo walimu wanayo haki ya kugoma ndio maana tumekata rufaa kutaka amri ya kuuzuia mgomo iondolewe.
"Juzi tulikuwa na semina ya Tucta kuhusu vyama vya wafanyakazi. Mtoa mada mmoja kutoka Nigeria, alishangaa kwamba serikali imekimbilia mahakamani kuuzuia mgomo. Alituambia kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa serikali kukimbilia mahakamani.
"Na sisi tunasema, kama serikali inadai kuwa imetekeleza madai ya walimu, ilienda mahakamani kufanya nini. Si imeshatekeleza."
Alikuwa akimaanisha kuwa kama ilishalipa madai ya walimu, basi mgomo ungekuwa batili na wale wote ambao wangehusika, wangeadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
"Kuna zile nyongeza za kila mwaka ambazo tulikubaliana ziongezwe, cha kushangaza katika mishahara waliyochukua walimu, hakuna hiyo nyongeza, sasa wanataka sisi tufanyeje,"alisema.
Kuhusu taarifa kuwa CWT na serikali walifikia maafikiano ambayo yalisainiwa na katibu wa chama hicho, Mukoba alisema taarifa iliyotolewa na serikali ililenga kupotosha umma.
"Anayeweza kusema kuwa walimu wamelipwa madai yao ni walimu wenyewe tu," alisema Mukoba katika kipindi hicho kilichorushwa moja kwa moja.
"Walimu ndio wanaoidai serikali na hivyo wakilipwa, ndio watakaoamua kuacha mgomo, lakini si mtu mwingine yeyote."
Mukoba pia alieleza kusikitishwa na kitendo cha serikali kuugeuza mgomo wa walimu kuwa wa viongozi wa CWT tu, akisema hizo ni mbinu za kuudhoofisha.
Mukoba alinusurika kupigwa wakati alipoenda kwenye mkutano, ambao ulikuwa uwe wa uzinduzi wa mgomo, kuwaeleza walimu kuwa Mahakama Kuu imeagiza mgomo huo usifanyike.
"Haikuwa kauli yangu mimi," alisema. "Nilikuwa natekeleza maagizo ya Mahakama Kuu ambayo iliagiza pande zote mbili zinazovutana kutoa matangazo kueleza wanachama wao kuwa mgomo umezuiwa na mahakama.
"Ile ilikuwa ni kauli ya mahakama na mimi ndio nilikuwa natekeleza amri ya mahakama. Lakini msimamo wa walimu umeonekana."
Pamoja na Jaji William Mandia wa Mahakama Kuu, kitengo cha kazi, kutoa amri ya muda ya kuzuia mgomo huo, walimu walipuuza na hadi sasa wanaendelea na mgomo baridi kwenye shule kadhaa, hasa za msingi.
Mukoba alisema CWT inasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuhusu ombi lao la kutaka amri ya kuzuia mgomo huo iondolewe ili serikali iwajibike kuwalipa walimu.
"Huu ni mgomo ambao unatajwa na sheria ya nchi," alisema kiongozi huyo. "Tumefanya.