CCM watishika na migomo ya waalimu washawisi serikali kuikomesha
Na Jackson Odoyo
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka serikali iwachukulie hatua za kisheria viongozi wa Chama cha Walimu nchini (CWT), kikidai viongozi hao wana agenda ya siri ya kutaka kuharibu utulivu na mshikamano wa nchi kwa kuhamasisha migomo ya walimu.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana ofisini kwake jijini Dar es Salam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itifaki na Uenezi, John Chiligati alisema Serikali inapaswa kuwashughulikia viongozi hao na kwamba, ina haki ya kufanya hivyo kwa sababu ndiyo mwajiri wao.
''Serikali kama mwajiri wao ina haki kuwashughulikia viongozi wa Chama cha Walimu wanaohamasisha mgomo huu kwa kuwa, wana agenda ya siri ya kuharibu utulivu na mshikamano wa nchi yetu, serikali isiwaonee huruma,'' alisema Chiligati.
Alisema CCM imeshangazwa na kauli ya Rais wa CWT ya kuitisha mgomo usio na ukomo wa nchi nzima, wakati uhakiki wa madeni ya walimu umekamilika na wataanza kulipwa kunzia leo.
Katika mazingira haya tunajiuliza mgomo huo una nia gani hasa wakati kile Walimu walichokuwa wanakipigania sasa kimepatikana, tunajiuliza mgomo wa nini na hao wanaopigania mgomo uanze kesho (leo) nia yao ni ipi?, alihoji Chiligati.
Hata hiyo Chiligati alisema CCM inawasihii na kuwashauri Walimu wenye nia safi kutojiingiza katika mgomo huo aliosema una nia mbaya na badala yake waendelee na kazi.
Aliongeza kuwa kitendo cha Walimu hao kuingia kwenye mgomo huo batili na haramu kwa kuwa malengo yake ni kuumiza watoto na kuingiza wasiwasi ndani ya nchi bila ya sababu za msingi.
Katika hatua nyingine Chiligati alisema kwamba, iwapo kuna mtu yeyote mwenye ushahidi kuwa Tanil Somaiya anahusika na tuhuma za rushwa ya rada pamoja na kukwepa kodi za Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) apeleke ushahidi huo katika vyombo vya dola.
''Somaiya alitoa Sh400 milioni kwa ajili ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM utakaofanyika Desemba 16 mwaka huu Mjini Dodoma. Tumepokea msaada huo kwa mikono miwili na ilifanyika hadharani pasipo kificho, wala si kweli kwamba CCM inapokea fedha zilizopatikana kwa njia haramu na wala si ishara ya kukumbatia ufisadi,'' Chiligati alisisitiza.
Wakati huohuo, Chiligati alisema CCM imesikitishwa na namna ambavyo viongozi wa vyama vya upinzani walivyokipaka matope chama hicho kupitia sakata la Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA)
Alisema ukweli ni kwamba, CCM haikuchukua fedha katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kuongeza kuwa iwapo katika orodha ya watuhumiwa wa EPA wapo wana CCM au wakereketwa wake, walifanya hivyo kwa maslahi yao wenyewe na wala hawakutumwa na chama hicho.
Source: Mwananchi.
Hivi kweli kiongozi (Chiligati) tena senior katika chama kutoa maoni, ushauri au maelekezo kama hayo kwa serikali si kuhatarisha amani nchini!! Walimu wanadai haki yao, leo hii kiongozi wa chama kinachoongoza serikali kutoa madai kama hayo ya kuwashughulikia viongozi wa CWT ni ukosefu wa busara na fadhila kwa walimu wetu. Na hii isiangaliwe kwa CWT pekee, kutakuwa na vyama vingine ambavyo vinawaunganisha wafanyakazi wengine nchini ambavyo navyo vitapewa vitisho vya namna hiyo ili visidai haki yao.
Kisieleweke kitu hadi haki itakapopatikana.
Kumshughulikia Mkoba (Rais wa CWT) hakitasaidia lolote bali itaamsha chuki zaidi ya walimu dhidi ya serikali. sasa hapa nani atakuwa auamia.....ni wanafunzi ambao wanapaswa kupewa haki yao ya msingi (ELIMU). Muda wa kutishiana umepitwa na wakati, serikali inawajibu wa kutoa haki kwa hawa walimu, waliokuwa wafanyakazi wa EAC na wengine. Tuache mambo ya kuburuzana na kupeana vitisho, kisa kudai HAKI.