Simba, Yanga zaibana TFF
IMANI MAKONGORO
KLABU kongwe nchini, Yanga na Simba zimetaka wachezaji wao nyota waliochaguliwa kwenye timu ya Taifa ya Tanzania kuondolewa ili washiriki vyema katika maandalizi ya michuano ya Kimataifa ya Afrika.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema kuwa wamekwisha wasilisha barua kwa Shirikisho la Kandanda nchini (TFF) kuhusiana na ombi hilo na wanaamini watakubaliwa.
Mwalusako alisema kuwa hatua hiyo inatokana na kupima umuhimu wa mashindano ya Mto Nile na yale ya kombe la Shirikisho ambapo timu yake itapambana na timu ya Dedebit ya Ethiopia kati ya Januari 28 na 30 mjini Addis Ababa.
Alisema kuwa wanatambua umuhimu wa wachezaji wao katika timu ya Taifa, lakini kwa ubora, Kombe la Shirikisho lipo juu zaidi ukilinganisha na mashindano hayo ya Misri.
�Ni kweli tumewasilisha barua rasmi leo ili kuomba wachezaji wetu wasiende huko Misri kwani watakaborejea, watakuwa wamebakiza siku saba kabla ya kusafiri kwenda Ethiopia, ni muhimu wakishiriki katika mazoezi ya timu yetu,� alisema Mwalusako.
Wachezaji wa Yanga walioko Stars ni Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Nadir �Cannavaro� Haroub, Nurdin Bakari, Jerryson Tegete na Abdi Kassim.
Watani wao wa jadi, Simba SC nao wamewasilisha barua TFF kuomba wachezaji wao waruhusiwe kufanya mazoezi na timu yao na si timu ya Taifa. Makamu wa Mwenyekiti wa Simba, Godfrey �Kaburu� Nyange alisema kuwa wamewasilisha barua hiyo kwa kutambua kuwa ombi lao litakubaliwa.