Rutashubanyuma
JF-Expert Member
- Sep 24, 2010
- 219,468
- 911,184
- Thread starter
- #2,081
Mwanahabari ajitosa kuongoza soka Morogoro
Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Morogoro; Tarehe: 29th December 2010 @ 23:35
MWANDISHI wa habari za michezo wa Radio Free Africa na Star tv Nickson Mkilanya ni miongoni mwa wanamichezo 21 waliojitokeza kuwania uongozi katika uchaguzi mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Morogoro (MRFA) uliopangwa kufanyika Januari 15 mkoani hapa.
Akizungumza na HABARILEO kwa njia ya simu jana, Mkilanya aliyepata kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (Taswa) na msemaji wa timu ya Mkoa wa Morogoro "Moro Star" mwaka 2007/8 alisema anawania nafasi ya ujumbe anayewakilisha klabu za Ligi Kuu na kwamba ameamua kugombea nafasi hiyo ili kusaidiana na uongozi utakaochaguliwa kuinua soka mkoani Morogoro na kuirejesha Morogoro katika ulimwengu wa soka kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Mkilanya alisema kuwa kama wajumbe watamchagua katika wadhifa huo atahakikisha anashirikiana na viongozi wenzake kuelekeza nguvu zao zaidi katika soka ya vijana ili kuibua vipaji zaidi na kuviendeleza sanjari na kuwatafutia wachezaji hao nafasi za kucheza katika timu za Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Kuu na baadaye nje ya nchi.
"Wajua Morogoro kuna vipaji vingi sana vya soka na si kweli kwamba Morogoro imechoka, lakini tatizo letu ni namna ya kuibua vipaji na kuviendeleza, tunataka wachezaji wenye vipaji ambao wapo huko wilayani waje mkoani wacheze wakitoka hapa wacheze timu kubwa na wasaidie kupandisha timu zetu,"alisema Mkilanya ambaye amepata kucheza timu mbalimbali za ligi daraja la tatu hadi ngazi ya Kanda.
Aidha alisema anataka kuwaunganisha wadau wa soka Mkoa wa Morogoro kuzisaidia timu zao katika madaraja mbalimbali na kwamba hilo linawezekana kwa kutafuta wafadhili ikiwemo taasisi za fedha zilizotapakaa mkoani hapa kusaidia soka la Mkoa wa Morogoro kwa kutoa udhamini ili soka iweze kusonga mbele.
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya MRFA Stephen Mdachi katika siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu aliwatangaza wanamichezo 21 kuwa wamejitokeza kuwania nafasi hizo akiwemo Athuman Kambi anayetetea nafasi ya Uenyekiti na Pascal Kihanga anayewania nafasi hiyo kwa mara ya kwanza.
Wengine ni Khamis Semka na Aristotle Nikitas wanaowania ukatibu mkuu, Msafiri Mkelemi na Athuman Ujuo wanaowania umakamu Mwenyekiti, Emanuel Kimbawala na Ramadhan Wagala wakichuana katika nafasi ya Katibu Msaidizi na Hasan Bantu anayewania ujumbe wa mkutano mkuu wa TFF.
Katika uchaguzi huo Mkilanya anachuana na Farid Nahad, wakati Abdallah Mkali akiwania uhazini, na wajumbe 10 wamejitokeza kuwania nafasi tatu za ujumbe wa Kamati ya Utendaji.