Michezo magazetini leo...

Michezo magazetini leo...

Status
Not open for further replies.
Soka Mbeya kubuni miradi

Imeandikwa na Joachim Nyambo, Mbeya; Tarehe: 10th January 2011 @ 23:30 Imesomwa na watu: 25; Jumla ya maoni: 0

CHAMA cha soka mkoani Mbeya (MREFA) kimeelezea mikakati kiliyojiwekea katika mwaka 2011, moja kati ya mikakati hiyo ikiwa ni kubuni na kuanzisha mradi utakaokiwezesha kuondokana na adha ya kuwa ombaomba.

Chama hicho kimesema imefika wakati wa chama kusimama kwa miguu yake badala ya kuendelea kutegemea michango ya wadau hali ambayo wakati mwingine imekuwa ikikisababishia kushindwa kuendesha mambo yake kwa wakati ikiwemo mikutano ambayo ili ifanyike ni lazima wapitishe bakuli la kuomba misaada.

Makamu Mwenyekiti wa chama hicho John Mwamwaja aliyasema hayo jana na kubainisha kuwa ukata huo ndiyo chanzo cha kuahirishwa pia kwa mkutano mkuu wa mwaka uliokuwa ufanyike Desemba mwaka jana ambao hadi sasa haijulikani utafanyika lini.

"Tunaandaa andiko la mradi na utakapokamilika tutauweka wazi kwa wadau ili kwa pamoja tuone ni jinsi gani tunaweza kuuendesha.Tumekwama vya kutosha kwa kutegemea mifuko ya wadau, sasa inabidi tuwe wabunifu," alisema Mwamwaja.

Mwamwaja pia alivishauri vyama vya soka katika ngazi za wilaya pamoja na klabu kuangalia uwezekano wa kulifanyia kazi wazo hilo kwakuwa pia vimekuwa vikishindwa kutimiza mikakati vinayojiwekea kutokana na hali ya ukata inayokuwa inavikabili.

Kwa upande wa mikakati ya kuwa na timu katika ligi kuu makamu Mwenyekiti huyo alisema licha ya mikakati inayoendelea kuhakikisha timu ya Prisons inapanda daraja pia MREFA ina mkakati wa kuhakikisha timu nyingine zinapanda daraja na ikiwezekana kufikia ligi kuu ya Tanzania Bara.

Aidha alisema chama pia kinatarajia kukutana na wabunge wote wa mkoa wa Mbeya ili kwa pamoja waweze kujadili mikakati ya kulijenga soka la mkoa ili kuurejeshea heshima yake kimichezo tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo soka limeporomoka kwa kiasi kikubwa.

 
Tukuyu Stars yatembeza bakuli

Imeandikwa na Joachim Nyambo, Rungwe; Tarehe: 10th January 2011 @ 23:25 Imesomwa na watu: 37; Jumla ya maoni: 0

TIMU ya soka ya Tukuyu Stars ya wilayani Rungwe mkoani Mbeya imewaomba wadau na wapenzi wa soka wilayani Rungwe na mkoa kwa ujumla kujitokeza kuichangia timu hiyo ili iweze kukamilisha mikakati yake ya kupanda daraja.

Katika mahojiano na mwandishi wetu, Meneja na Kocha mkuu wa timu hiyo iliyowahi kuwa bingwa wa Tanzania bara miaka ya 1980 Alex Mwambipile alisema baada ya kupotea kwa muda mrefu kwa timu hiyo katika medani ya soka sasa ni wakati wa kuirejesha.

Hata hivyo, Mwambipile alisema nguvu zaidi ya hali na mali inahitajika katika kufanikisha mkakati huo kwa kuwa hali ya ukata ni moja kati ya changamoto kubwa zinazoikabili Tukuyu Stars.

Alisema kwa sasa timu hiyo inayojiandaa na ligi ya taifa ngazi ya mkoa imeshindwa kukaa kambini badala yake wachezaji wake wanatoka majumbani kwao na kukutana uwanjani hali aliyosema inaathiri mazoezi ya timu.

"Ni hali ambayo kwakweli inatupa shida ya kufikia malengo mazuri tuliyojiwekea ya kupandisha daraja timu yetu.

Wachezaji kutoka pamoja na kutoka majumbani wakutane uwanjani ni vigumu kumudu mazoezi wanayopewa na mwalimu kwakuwa baadhi yao wanatoka hawajala makwao," alisema Mwambipile.

Aliongeza kuwa iwapo wadau watajitokeza na kuisaidia timu hiyo, upo uhakika wa kuirejesha katika ligi kuu na hatimaye wadau na wapenzi wa soka mkoani hapa kurejeshewa burudani waliyoikosa kwa miaka mingi kutokana na timu hiyo kushuka daraja.

Katika ligi ya taifa ngazi ya wilaya ya Rungwe,Tukuyu Stars iliibuka mshindi kati ya timu tisa zilizoshiriki ligi hiyo nyingine zikiwa ni Katumba, Ushirika, National Ntaba, Masukuru, Home Boys, Muungano, Kiwira pamoja na Kiwira Magereza.
 
Rwanda yaanza vema fainali za Vijana

Imeandikwa na Finny Muyeshi wa Cecafa, Kigali KIGALI, Rwanda; Tarehe: 10th January 2011 @ 09:48 Imesomwa na watu: 118; Jumla ya maoni: 0


WENYEJI wa michuano ya Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, Rwanda wameanza vema michuano hiyo baada ya kuichapa Burkina Faso mabao 2-1 kwenye uwanja wa Amahoro juzi.

Aidha, Misri nayo iliifunga Senegal idadi hiyohiyo ya mabao katika mechi nyingine ya kundi A.

Hii ni michuano ya pili ya Afrika Rwanda kuandaa ikiwemo ile ya vijana chini ya miaka 20 iliyofanyika miaka miwili iliyopita.

Kwa matokeo hayo, washindi hao sasa wanatarajia kukutana kesho ambapo kila upande unawania kushinda ili kujiweka vizuri.

Kila kundi lina timu nne ambapo washindi wawili katika kila kundi watafuzu kucheza nusu fainali na kukata tiketi ya kushitiki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Mexico Juni.

Rwanda ilianza kupata bao la kuongoza katika dakika ya nne kupitia kwa Faustin Usengimana kabla ya kuongeza bao la pili katika dakika ya pili ya kipindi cha pili kupitia kwa Tibingana Mwesigwe.

Burkina Faso ambayo ilipata medali ya shaba katika michuano iliyofanyika Algeria miaka miwili iliyopita, ilicheza vizuri baada ya kuingia mabao hayo na kufanya kupata bao la kufutia machozi katika dakika ya 55 kupitia kwa Faical Ouedraogo kwa mkwaju wa penati.

"Ni jambo jema kupata ushindi katika mechi ya kwanza," alisema kocha wa Rwanda Mfaransa Richard Tardy.

"Sasa hakuna cha kupoteza zaidi ya kuangalia mbele kushinda mechi mbili zilizosalia," aliongeza.

Katika mechi nyingine, Senegal ilicheza vizuri katika kipindi cha kwanza na kupata bao la kuongoza katika dakika ya 21 likifungwa na Ibrahima Ndiaye.

Lakini Wamisri walibadili matokeo katika dakika ya 61 ambapo walisawazisha bao hilo kupitia kwa Mahmoud Abdelmonen.

Na katika dakika ya 83 mchezaji wa akiba Mohamed Rasham aliifungia Misri bao la ushindi.
"Tumekuja hapa kuchukua ubingwa na hakuna shaka na hilo," alisema kocha wa Misri Mohamed Omar.

"Tutaendelea na moto wetu huu huu wa kushinda kila mechi na wala haijalishi kama mechi ijayo tutacheza na wenyeji," alisema.

Mechi hizo zilitarajiwa kuendelea jana kwa kundi B ambapo kwenye uwanja wa Omuganda, Gisenyi, Gambia ilitarajiwa kucheza na Kongo kabla ya Ivory Coast haijamenyana na Mali.
 
Kongo yatamba kutwaa ubingwa Mto Nile

Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Cairo; Tarehe: 10th January 2011 @ 09:48 Imesomwa na watu: 205; Jumla ya maoni: 0


KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mutubile Santos amesema wao ndiyo wataibuka mabingwa wa michuano ya Nchi za Bonde la Mto Nile inayoendelea mjini hapa.

Santos alitoa kauli hiyo baada ya juzi timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars' mchezo wa Kundi B uliofanyika Uwanja wa Polisi mjini hapa.

"Timu yangu ipo safi kila idara, leo (juzi) hatukucheza vizuri lakini mechi zijazo tutang'ara na sisi ndio mabingwa," alisema Santos.

Kocha huyo aliyeiongoza DRC kutwaa ubingwa wa michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) nchini Ivory Coast mwaka juzi, alisema pia anajivunia wachezaji tisa wa TP Mazembe ambao anao katika kikosi chake.

Wachezaji hao ni kipa mahiri Kidiaba Muteba, Mkulukuta Miala, Mabele Biwaka, Mihayo Kazembe, Kimwaki Joel Kasongo Ngandu, Lofo Bongeli, Kanda Deo na Mvete Luyeye.

Kwa upande wake Kocha wa Harambee Stars, Zedakaya Otieno, alisema DRC si timu ya kutisha sana na kwamba kufungwa kwao kulitokana na makosa ya beki zake.

"DRC ni timu ya kawaida, naamini soka waliloonesha vijana wangu lilikuwa la hali ya juu sana, tutazidi kuimarika mechi za mbele," alisema kocha huyo.

 
Poulsen, wachezaji waapa kufa na Uganda

Imeandikwa na Amir Mhando, Cairo; Tarehe: 10th January 2011 @ 09:48 Imesomwa na watu: 232; Jumla ya maoni: 0


WACHEZAJI wa Taifa Stars na Kocha Mkuu, Jan Poulsen wamesema watakufa na Uganda kesho watakapokutana nayo katika mechi ya mwisho ya makundi ya michuano ya Bonde la Mto Nile.

Watanzania kwa mara nyingine juzi walitoka vichwa chini kwenye Uwanja wa Polisi mjini hapa baada ya dakika 90 kumalizika ikiwa imefungana bao 1-1 na Burundi.

"Nasikitika kwamba tumeshindwa kuifunga Burundi, tumecheza kadri ya uwezo wetu, lakini tumeshindwa kuzitumia nafasi tulizopata.

"Hili ni tatizo na yatupasa kubadilika, naamini vijana wameona na watabadilika," alisema Poulsen jana.

Stars imepata matumaini ya kufuzu nusu fainali baada ya juzi Misri kuifunga Uganda bao 1-0 lililofungwa dakika ya 90 na Haji Gedo kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Arab Contractors.

Matokeo hayo yanaifanya Misri kutinga nusu fainali kwani imefikisha pointi sita, ambapo hata kama itafungwa mchezo wake wa mwisho kesho dhidi ya Burundi haitaathirika.

Ili Stars ifuzu nusu fainali itabidi iifunge Uganda kesho, kisha iombee Misri iifunge Burundi
ama itoke nayo sare, vinginevyo kama Burundi itashinda basi itabidi timu hizo ziangalie uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Mpaka sasa Stars imefungwa mabao sita na imefunga mawili, hivyo ina deni la mabao manne, wakati Burundi imefungwa manne na imefunga mawili huku nayo ikiwa na deni la mabao mawili.

Kundi hilo la A linaongozwa na Misri yenye pointi sita na mabao sita ya kufunga ikiwa imefungwa moja, wakati Uganda ni ya pili ikiwa na pointi tatu na mabao manne ya kufunga, ikiwa imefungwa mawili, huku Burundi ikiwa ya tatu na Stars ya mwisho.

Zote zina pointi moja ila tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

"Najua Uganda nayo itacheza kwa nguvu, lakini tutabadilika sana, haitakuwa kama tulivyocheza na Burundi.

Sijui nini kimetokea, lakini dakika 20 za mwisho ndiyo tulizinduka. "Tunahitaji kubadilika sana, mashindano ni magumu, kila timu inacheza kwa nguvu sana," alisema Poulsen.

Nahodha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa alisema wamepania kuibuka na ushindi na kwamba ama zao Uganda ama Stars.

Pia kipa Juma Kaseja naye alizungumzia mechi hiyo na kusema Waganda wataipata kwani wameshaona uchezaji wao, ingawa wenzao waliibana Misri na kufungwa bao 1-0, wakati Stars ilifungwa mabao 5-1.

Kwa upande wa Kundi B, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), inamaliza kesho na Sudan ambayo mchezo wa kwanza ilifungwa bao 1-0 na Kenya kabla ya DRC kuifunga Kenya bao 1-0.

Kutokana na mazingira hayo, timu za kufuzu nusu fainali kundi hilo bado tata, kwani hata Sudani ikiifunga DRC kesho nayo inaweza kufuzu nusu fainali.

Timu mbili za juu kila kundi zitaingia nusu fainali, ambapo Kundi B lenyewe lina timu tatu wakati A lina timu nne.

Kulingana na ratiba ya michuano hiyo ambayo zawadi kwa bingwa ni kombe na fedha taslimu zaidi ya Sh milioni 200 za Tanzania, washindi wa tatu kila kundi watacheza kuwania nafasi ya tano.
 
Ruvu Shooting, JKT katika fainali za Uhai

Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 10th January 2011 @ 09:46 Imesomwa na watu: 42; Jumla ya maoni: 0

FAINALI za ligi ya vijana chini ya miaka 20, Kombe la Uhai inatarajiwa kufanyika leo kwa kuzikutanisha timu ndugu, JKT Ruvu na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Karume, Ilala Dar es Salaam.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa ya kuvutia kutokana na timu hizo kufanya mashambulizi ya kuvizia, ni kama zinacheza mchezo wa aina moja.

Ruvu Shooting ilitinga fainali baada ya kuifunga AFC mabao 2-0 katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa kwenye uwanja huohuo juzi.

Na JKT Ruvu ilifika hatua hiyo baada ya kuifunga Polisi Dodoma katika mechi nyingine ya nusu fainali juzi.

Kabla ya mechi hiyo itakayochezwa jioni, asubuhi kutakuwa na mechi ya kumtafuta mshindi wa tatu kati ya AFC na Polisi Dodoma.

Mechi hiyo nayo inatarajiwa kuwa kali kutokana na timu hizo zote kuonesha soka ya kuvutia.

Hata hivyo, AFC ndio inayopewa nafasi kubwa ya kupata nafasi ya tatu baada ya kushindwa kufika fainali.

Awali ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufika hatua ya fainali.

Timu hiyo tangu kuanza kwa mashindano imekua ikishiriki kwa tabu kutokana na kukosa fedha ya posho na kujikimu, hali iliyosababisha kituo cha redio cha Clouds kujitolea kugharimia malazi kwa timu hiyo.

 
Ferej anaonewa – Ndolanga

Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 10th January 2011 @ 09:46 Imesomwa na watu: 237; Jumla ya maoni: 1

KIONGOZI wa zamani wa soka nchini, Muhidin Ndolanga, amesema kuna uonevu katika kufutwa kwa uchaguzi uliompa ushindi Rais wa muda mrefu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ali Ferej Tamim.

Katika madai yake, Ndolanga alisema Kamati iliyosimamia uchaguzi huo na baadaye kubatilisha matokeo yake, inapaswa kuvunjiliwa mbali kwa sababu imeshindwa kutenda haki.

Ferej aliye madarakani kwa miaka 22 mfululizo, alishinda uchaguzi huo wa Desemba 31, mwaka jana kisiwani Pemba kwa kuzoa kura 32 kati ya 54 za urais.

Hata hivyo, ushindi wake ulipingwa na wagombea wenzake kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya madai ya kushindwa kuwasilisha cheti cha kumaliza kidato cha nne kama Katiba ya ZFA inavyoelekeza.

Hoja nyingine ni kwamba kulikuwa na wajumbe ambao hawakustahili kupiga kura kwenye uchaguzi huo madai yaliyopata baraka za Kamati ya Uchaguzi na hivyo kufuta matokeo yote ya uchaguzi.

Lakini jana Ndolanga akizungumza na gazeti hili, alisema kuna uonevu katika suala hilo na kuhoji kama Ferej hana elimu ya kidato cha nne, amewezaje kuongoza ZFA kipindi chote hicho na kubeba vikombe.

"Kuna maonevu hapa…ninavyojua mimi mfumo wa elimu wa Zanzibar ulikuwa tofauti na huku Bara huko nyuma. Wenzetu walikuwa wakiishia kidato cha tatu na kwenda vyuoni na kupata elimu nzuri tu.

"Sijui ulibadilika lini, lakini ninachojua Wazanzibari walisoma vizuri na kupata elimu bora sana nje.

Ferej ni msomi mzuri, na ndiyo maana amekuwa akiongoza ZFA kwa muda wote huo, tena vizuri sana," alisema Ndolanga aliyeondoka katika uongozi wa soka mwaka 2004.

Alisema kama hoja ilikuwa ni kumng'oa Ferej, basi lilipaswa kufanywa kwa kufuata haki na demokrasia kwa maana ya kushindwa katika kura na siyo kwa madai ya cheti cha kidato cha nne.

"Hivi wakati akichukua Kombe la Chalenji (mwaka 1995), mbona hawakuuliza cheti cha kidato cha nne?

Mbona Zanzibar iliposhinda mara mbili vikombe vya vijana, tena kwa kuwashinda hata TFF wenye shahada zao, mbona hatukusikia elimu ya kidato cha nne.

"Moja ya sifa za uongozi ni uzoefu. Hapa ni uzoefu katika michezo na hasa soka. Ferej anao.

Watu wanahoji elimu ya kidato cha nne, hivi mbona wenye digrii zao hawana lolote wanalolitenda," alisema Ndolanga, msomi wa Chuo Kikuu cha Nairobi aliyekaa katika uongozi wa juu wa soka kwa zaidi ya miaka 13.

Kiongozi huyo wa zamani anayekumbukwa kwa misimamo yake ikiwamo ya kutetea haki yake anapoona anaonewa, alisema anatoa maoni hayo kama Mtanzania na pia kuepuka masuala kama hayo kujitokeza kwa upande wa Tanzania Bara.

"Haya yakiachwa yafanyike, yataleta vurugu na yatahamia hata huku kwetu (Tanzania Bara)…watu wanataka kutumia vigezo dhaifu kuhalalisha kuingia madarakani.

Ndio maana nashauri na hii Kamati iliyosimamia uchaguzi, ifutiliwe mbali.

Imeshindwa kutenda haki na kusimamia itendeke," alisema. Ndolanga alisisitiza kuwa Ferej alikuwa na sifa za kushiriki uchaguzi huo na ameshinda kwa kuchaguliwa na wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wa ZFA.
 

Kocha Burundi:Ubingwa Chalenji umewazuzua Stars

Imeandikwa na Amir Mhando, Cairo; Tarehe: 10th January 2011 @ 09:20 Imesomwa na watu: 332; Jumla ya maoni: 0
KUFANYA vibaya kwa Taifa Stars katika michuano ya soka kwa Nchi za Bonde la Mto Nile kunatokana na wachezaji wa timu hiyo kuvimba vichwa baada ya kutwaa ubingwa wa Chalenji mwezi uliopita Dar es Salaam.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Kocha wa Burundi, Niyongabo Amas baada ya kumalizika mchezo baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Polisi mjini hapa na matokeo kuwa sare ya bao 1-1.

"Sioni ambacho Tanzania imecheza, si kama ile timu ya Dar es Salaam, naona wamejisahau na ubingwa, wanaona tayari wamepata mafanikio makubwa.

"Wale vijana hatari wote hawaonekani, ni kama timu mpya, hata bao la penati ni zawadi wamepewa haikuwa penati halali," alisema kocha huyo na kuwapongeza vijana wake kwa kucheza vizuri, licha ya kutoibuka na ushindi.

Kocha huyo alikuwa na kikosi cha Burundi katika mashindano hayo Dar es Salaam akiwa Kocha Msaidizi na timu yake ilifungwa mabao 2-0 na timu ya Taifa ya soka ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' hatua ya makundi.

Mwezi uliopita Kilimanjaro Stars ilitwaa ubingwa wa Chalenji mashindano yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) na robo tatu ya wachezaji wa Kilimanjaro Stars ndiyo wanaunda Taifa Stars.

Hata hivyo nahodha wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa alipingana na kauli kwamba wamebweteka na kusema soka ndivyo linavyokuwa kuna kushinda, kufungwa na sare, lakini
pia kutwaa kwao ubingwa wa Chalenji kumezifanya baadhi ya timu ziwakamie.

Wakati huohuo, Misri imekuwa ya kwanza katika michuano ya Nchi za Bonde la Mto Nile inayoendelea mjini hapa kutinga nusu fainali baada ya kuifunga Uganda bao 1-0.

Matokeo hayo yameifanya Misri ifikishe pointi sita baada ya kuifunga Stars mabao 5-1 katika mechi ya kwanza, huku Uganda ikiwa nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu ilizozipata baada ya kuifunga Burundi. Mwisho.


 
Taifa Stars yaingia hukumu leo Monday, 10 January 2011 20:41

kocha%20poulsen2.jpg
Kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen.

Mwandishi Maalum, Cairo
NUSU fainali ya Kombe la Chalenji itarudiwa leo jijini Cairo majira ya 9:45 Alasiri wakati timu ya Tanzania 'Taifa Stars' itapokuwa ikipepetana na Uganda 'The Cranes' kwenye Uwanja wa Polisi mjini hapa.

Mwezi moja tangu Stars iliposhinda kwa mikwaju ya penalti kwenye michuano ya Chalenji iliyofanyika jijini Dar es Salaam, timu hizo zinashuka dimbani zikiwa kwenye viwango tofauti kabisa.

Uganda wanaoneka kuwa bora zaidi kulinganisha na Taifa Stars kwa kuangalia matokeo yao kwenye fainali hizo za Mto Nile. Stars ilifungwa na Misri mabao 5-1, kisha ikatoka 1-1 na Burundi, wakati Uganda iliifunga Burundi 3-1, ikafungwa 1-0 na Misri.

Wachezaji wa Stars wameapa kufa na Uganda, huku wakisisitiza kuwa makosa waliyoyafanya katika mechi mbili zilizopita hayatajirudia na watahakikisha wanaibuka na ushindi mnono.

Ni kawaida ya Stars kuapa kabla ya mechi kwamba watafia uwanjani kuhakikisha wanaibuka na ushindi, lakini inapofika siku ya mechi hakuna hata anayekubali kuzimia.

Jana nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa alisema wanajua matokeo yetu yamewanyong'onyesha Watanzania, lakini hatawaangusha tena kwa kuifunga Uganda na kufuzu nusu fainai.

Kikosi cha Uganda kilichopo mjini hapa hakina nyota wengi waliokuwa Dar es Salaam mwezi uliopita kwenye michuano ya Chalenji, badala yake wachezaji walio wengi ni chipukizi, lakini walio na uwezo mkubwa wa kusakata soka.

Uganda iliwaduwaza mashabiki wa Misri Jumamosi baada ya kuibana vilivyo Misri 'Farao'karibu dakika 89 za mchezo na kufungwa bao pekee dakika ya 90 mfungaji akiwa Ahmed Hassan Gedo.

Hali hiyo imeifanya Uganda sasa kuwa midomoni mwa wadau wa soka mjini hapa kwamba ni timu nzuri na inapewa nafasi kubwa ya kuifunga Stars leo.

Lakini Nsajigwa na wenzake wanasema watawashangaza wengi na hawaoni kwa nini wasiingie nusu fainali, hivyo kazi yao leo ni moja kumpiga Mganda, kwani nia wanayo, uwezo wanao na sababu pia wanayo.

Kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen alisema anatarajia mechi itakuwa ngumu, lakini kwa vile wanaingia wakiwa wanajua makosa halitawasumbua sana.

Naye kocha wa Uganda, Bobby Williamson naye alisema mchi itakuwa ngumu, lakini ameshajua udhaifu wa Stars itakuwa si kazi ngumu kushinda.

Misri inayoongoza Kundi A ikiwa na pointi sita tayari imetinga nusu fainali na leo inamaliza na Burundi mchezo utakaofanyika mjini Ismailia, ambapo hata kama itafungwa haitaathirika.
 
Viongozi Yanga wakiri kumkosea Papic Monday, 10 January 2011 20:39

Calvin Kiwia na Clara Alphonce
UONGOZI wa klabu ya Yanga umekiri kufanya makosa ya kumuogeza kwenye benchi lake la ufundi kocha Felix Minziro bila ya kumhusisha Kostadin Papic anayetishia kuondoka kutokana na kitendo hicho.

Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu Afisa Habari wa klabu hiyo, Luis Sendeu alisema ni kweli timu hiyo ilifanya maamuzi hayo bila ya kumshirikisha Papic.

"Ni kweli hakushirikishwa Papic kwenye uamuzi huu, lakini mambo yote yatakuja kukamilika jijini Dar es Salaam baada ya timu kurejea kutoka visiwani Zanzibar kwenye mashindano ya Mapinduzi," alisema Sendeu.

Alisema kuwa haoni ubaya wowote kwa uongozi wa klabu hiyo kumwongeza kwenye benchi la ufundi Minziro bila ya kumshirikisha Papic.

"Yeye Papic mwenyewe alishawahi kuuomba uongozi wetu kwamba atafutiwe kocha msaidizi ambaye aliwahi kuichezea timu ya Yanga kwa kipindi cha nyuma, hivyo Minziro anasifa hizo zote," alisisitiza.

Aliongeza kuwa Papic hawezi kumkataa kwa sababu siyo yeye anayemlipa mshahara kwenye kibarua chake hivyo kama atamkataa anakuwa na sababu zake mwenyewe na wala sina imani hiyo ya kuwa atamkataa Minziro.

Papic alisema yuko tayari kuacha kuinoa timu hiyo kama viongozi wanaendelea kumlazimisha kwa sababu msaidizi anayemtaka si yule aliyewahi kufundisha timu kubwa.

"Minziro tayari ameshafundisha timu kazaa katika Ligi Kuu Tanzania bara hivyo hawezi kuwa msaidizi wake kwa kufanya hivyo ni kutaka kumchanganya na kuvuruga timu.

''Nataka msaidizi, lakini hawe alishakuwa mchezaji wa zamani na hajawahi kufundisha timu za ligi kuu au kuwa kocha mkuu wa timu yoyote,''alisisitiza Papic.

Wakati huo huo; Jackson Odoyo kutoka Zanzibar kuwa wadhamini wa Yanga wakiongozwa na mfadhiri wao Yusufu Manji wametoa shs 5milioni kwa wachezaji ili kuwatia moyo.

Fedha hizo ilizotoa kamati hiyo chini ni zaidi ya zile ambazo bingwa wa Kombe la Mapinduzi atapewa sh3milioni.

Mdhamini huyo aliyekutana na wachezaji wa Yanga kwenye kambi yao iliyopo hoteli ya All Anoor aliwataka wafuzu kwa fainali na kuivaa Simba.

"Mimi nimekuja hapa ili kukutana na wachezaji kwa ajili ya suala moja tu la kuwatia moyo ili washinde mechi ya leo na hatimaye waingie katika hatua ya fainali," alisema Manji
 
JKT Ruvu mabingwa wapya
Monday, 10 January 2011 20:37

Salome Millinga na Neema Kimaro
BAO la dakika 119, lililofungwa na Prosper Mkwama lilitosha kuipa ubingwa Kombe la Uhai, JKT Ruvu dhidi ya ndugu zao wa Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Mabingwa hao wapya wa Kombe la Uhai walilazimika kutumia nguvu ya ziada kabla ya kusawazisha bao la mapema la Shooting lililofungwa naNjaidi Njaidi dakika 17, kabla ya Ibrahim Kombo kuisawazishia JKT dakika 83 kufanya mchezo huo kwenda dakika 120.

Wakati mashabiki waliofurika uwanjani hapo wakisubili mikwaju ya penalti Mkwama aliwainua mashabiki wa JKT kwa kufunga bao la ushindi dakika moja kabla ya filimbi ya mwisho.
Awali vijana AFC Arusha walifanikiwa kuchukua nafasi ya tatu baada ya kuinyuka Polisi Dodoma kwa mabao 2-0 kwenye uwanja huo.

Mabao ya AFC yalifungwa na Paulo Msafiri dakika ya 17 na Zakayo Joseph la pili mchezo ulionekana kuwa na kasi kubwa, lakini wingi wa majeruhi kwenye kikosi cha Polisi ulitoa mwanya kwa vijana wa Arusha kutawala mchezo huo.

Bingwa wa michuano hiyo JKT Ruvu walijinyakulia shs 1.5m, huku Shooting wao waliondoka na shs 1m na AFC walikabidhiwa 500,000/= kama washindi wa tatu.

Tuzo ya kipa bora ilichukuliwa na Edson John wa JKT Ruvu, mfungaji boraMichael Mgimwa wa Mtibwa na mchezaji bora wa mashindano Ayoub Kitala kila moja alikabidhiwa shs 300,000/=, wakati tuzo ya timu wenye nidhamu ilikwenda kwa Toto African waliokabidhiwa Shs 400,000/= na mwamuzi bora Listone Iyali alipata laki tatu.

Akizungumza na Mwananchi kocha AFC, Rashidi Chama alisema ''Namshukuu Mungu kwani hii ni mara yetu ya kwanza kushiriki michuano hii na pamoja na matatizo yote tuliyoyapata bado tumefanikiwa kushika nafasi ya tatu."

''Tunaomba wadhamini waangalie sana timu zinashiriki kutoka mikoani kuongeza kiwango cha fedha ili kukidhi mahitaji ya timu katika michuano ijayo pia wapenzi wa AFC tunaomba mtuchangie ilituweze kununua vifaa vya wachezaji,'' alisema chama.

Naye kocha wa Polisi Dodoma, Charles Kates ''Tunamshukuru kwa hapa tulipofikia mashindano yalikuwa mazuri kwa kweli sijaona mapungufu yoyote ili wadhamini waongeze fedha kidogo ili wachezaji waweze kujikimu hususani wa mikoani''.

Timu yangu leo haikucheza vizuri sababu majeruhi walikuwa wengi nitajipanga vizuri katika michuano ijayo nita imarisha kwenye mapuungufu yaliyo jitokeza kwa wa chezaji wangu'' alisema Kates.
 
Makocha wa kigeni wazua jambo Monday, 10 January 2011 20:36

Sosthenes Nyoni
BAADHI ya viongozi na makocha wa soka wametupiana lawama ambapo kila upande ukiutuhumu mwingine kuwa ndio chanzo cha makocha wa kigeni kupewa kipaumbele tofauti na wazalendo.

Wakizungumza mwishoni mwa wiki kupitia kipindi cha 'Sport Kizaazaa' kinachowakutanisha wadau mbalimbali wa mchezo huo na kurushwa hewani kupitia kituo cha televisheni cha ITV, viongozi na makocha hao kila mmoja uliutaka upande mwingine ubadilike.

"Ukweli ni kwamba sio kama sisi tunapenda kuajiri makocha wa kigeni isipokuwa wazawa wana matatizo mengi kwanza hawajiamini katika kazi zao, lakini pia wanagawa wachezaji kwa mfano mimi nilishawahi kuletewa kesi za namna hiyo mara kadha," alisema Hassan Dalali aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba.

Naye makamu mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' akichangia mada hiyo alisema kinachowafanya makocha wazalendo wasipewe kipaumbele ni tabia ya kutopenda kujiendeleza.

"Ifike wakati makocha wawe na utamaduni wa kujiendeza kielimu zaidi na kujiamini vinginevyo tutakuwa tunalaumiana tu, angalau tuifahamu elimu ya michezo, utakuta mchezaji anaumia, lakini kocha hajui chochote wakati yeye ndiye mtu wa kwanza," alisema Kaburu.

Akijibu hoja hizo kocha Joseph Kanakamfumu alisema fikra hizo ni potofu na kuongeza kuwa kudharaulika kwa walimu wazalendo ni matokeo ya dhana ya viongozi wa klabu kuthamini ngozi nyeupe.

"Hatupewi kipaumbele kabisa, ukiwa na ngozi nyeupe utapewa kila kitu kama unataka mipira 20 haraka utapata ikiwemo mshahara mkubwa, lakini mzalendo hiyo laki tatu yenyewe mpaka ulipwe balaa, isitoshe ikitokea wamekupa timu watakupangia kikosi wao," alisema Kanakamfumu
 
Wapinga kamati ya ZFA Monday, 10 January 2011 20:35

Vicky Kimaro
WADAU wa soka visiwani Zanzibar wamepinga kamati ya muda iliyoteuliwa kuongoza Chama cha Soka, ZFA, hadi hapo uchaguzi mkuu utakaporudiwa.

Kamati hiyo ya muda iliyoteuliwa itaongozwa na Katibu Mzee Zam Ali na Masoud Atai ni mjumbe kutoka Wilaya ya Kusini Unguja, Musa Soraga na Ravia Idarus ni wajumbe ZFA taifa.

Akizungumza na Mwananchi jana mjumbe wa ZFA Mjini Unguja, Uledi Said alisema anashangazwa na kamati ya uchaguzi chini ya Mwenyekiti Ali Suleiman 'Shihata' kuwateua viongozi hao kuiongoza ZFA wakati wamekuwa wakishutumiwa kutumia vibaya mali za chama.

"Wao wanashutumiwa kwa utendaji mbovu pamoja na viongozi waliopita ndio maana ulishinikizwa ufanyike uchaguzi halafu leo tena hao hao wanachaguliwa kuunda kamati ya muda, serikali ingilie kati suala hili itusaidie kuchangia gharama za uchaguzi ili ufanyike kama ulivyoagizwa na kamati ya uchaguzi tukomboe soka letu la Zanzibar," alisema Said.

ZFA walisema hawawezi kurudia uchaguzi huo kama ulivyoagizwa na kamati ya uchaguzi chini ya Shehata kwa madai kuwa chama hicho hakina fedha kwani hata uchaguzi wa kwanza uliomuingiza madarakani rais Ally Ferej Tamim uligharimu zaidi ya shilingi milioni 30.

Mwenyekiti wa kamati Ally Shehata aliiambia Mwananchi kuwa kamati yake itakaa leo kujadili masuala mbali mbali na kutoa msimamo wake kuhusu uchaguzi huo.
 
Gambia yaloa, Rwanda yaiva Misri leo Monday, 10 January 2011 20:34

KIGALI, Rwanda
MABINGWA watetezi Gambia walipokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Congo Brazzaville kwenye fainali hizo za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 inayoendelea nchini Rwanda.

Michuano hiyo inaendelea leo kwa katika Kundi A, kwa kuwakutanisha wenyeji Rwanda dhidi ya Misri, huku Burkina Faso wataonyeshana kazi na majirani zao Senegal.

Timu mbili kutoka kila kundi zitafuzu kwa nusu fainali na timu hizo nne ndizo zitakazoiwakilisha Afrika kwenye Kombe la Dunia fifa kwa vijana baadaye mwaka huu.

Mchezo huo baina ya mabingwa ho wa zamani Gambia na Congo ilichezwa kwenye uwanja mpya wa Umuganda uliopo kwenye mji wa tatu kwa ukubwa nchini Rwanda wa Rubavu.

Congo walipata mabao yao mawili katika dakika saba za mwanzo kupitia kwa Samarange Binguila (4) na Stevy Epako (7) na kwenda mapumziko wakiwa kifua mbele kwa ushindi huo. Binguila alihitimisha kalamu hiyo kwa kufunga bao la tatu zikiwa zimebaki dakika 15 mpira kumalizika.

Mabingwa hao Gambia waliowasili Rwanda ikiwa ni moja ya timu inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo, lakini baada ya kipigo hicho cha mabao3-0 sasa watalazimika kushinda mechi zao mbili za mwisho kutafuta nafasi ya kucheza nusu fainali.

Katika mchezo mwingine wa kundi hilo Tembo watoto wa Ivory Coast wameanza vizuri kampeni zake kwa ushindi mnono wa mabao 2-1 dhidi ya majirani zao Mali.

Mali iliyokuwa timu ya kwanza kuwasili Kigali kwa ajil ya fainali hizi za CAF U-17, walipata bao lao la kwanza dakika ya 24 kupitia Tiecoro Keita, lakini Drissa Diarassouba alisawazisha kwa tembo hao watoto kabla ya mapumziko.

Katika kipindi cha pili Guy Stephane Bedi alifunga bao la pili kwa Tembo hao na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele.

Congo na Ivory Coast zinaongoza Kundi B kwa kufikisha pointi tatu kila moja lakini wanatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
 
Ronaldo apiga tatu, Milan yashikwa
Monday, 10 January 2011 20:35

MADRID, Hispania
MABAO tatu ya Cristiano Ronaldo na moja la Kaka yalitosha kuipa Real Madrid ushindi mnono dhidi ya Villarreal 4-2 na kuisogelea Barcelona kileleni mwa La Liga.

Mreno huyo alisawazisha mara mbili katika kipindi cha kwanza kwa wenyeji hao na kuwafungia bao la tatu dakika ya 79, likiwa ni goli kale la 22 msimu huu kabla ya kutegeneza bao la nne kwa Kaka aliyeingia akitokea benchi.

Kocha Jose Mourinho na Real wamefikisha pointi 47katika michezo 18, wakiwa nyuma ya Barcelona yenye pointi 49 baada ya kuifunga Deportivo Coruna 4-0 hape Jumamosi.

"Cristiano amenifanya nikose la kusema. Amekuwa akibadilika kila baada ya mchezo, kila baada ya wiki. Hata sijui nitafananisha na nini uchezaji wake," Mourinho aliwaambia wanahabari wakati Real wakipaa juu kwa pointi 11 zaidi kwa Villarreal inayoshika nafasi ya tatu.

Valencia ya nne na pointi zake 34, baada ya Juan Mata, ambaye awali alikosa penalti, lakini alijirekebisha na kufunga bao pekee kwa 1-0 dhidi ya mahasimu wao Levante.
Nayo Espanyol iliwasambaratisha Real Zaragoza 4-0 na kuendelea kusaka ndoto yake ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Pablo Osvaldo, Luis Garcia (penalti) na Alvaro Vazquez ilifanya timu hiyo ya jiji la Barcelona kuwa mbele kwa mabao 3-0 hadi mapumziko kwenye Uwanja wa Cornella-El Prat kabla ya Sergio Garcia kumalizia kalamu hiyo ya mabao dakika ya 87 na kuipandisha Espanyol hadi nafasi ya tano kwa pointi 31.

Real Mallorca ilishinda 4-1 nyumbani dhidi ya Almeria, Osasuna walilazimishwa suluhu na Getafe nayo Sporting Gijon iligawana pointi na Racing Santander kwa sare ya bao 1-1.

MILAN, Vinara AC Milan walipunguzwa kasi yao baada ya kutoka sare ya 4-4 na Udinese, lakini bado wanaendelea kuongoza Serie A kwa pointi nne baada ya Edinson Cavani kufunga mabao matatu kwa Napoli iliposhinda 3-0 dhidi ya Juventus.

Lazio iliyokuwa nafasi ya tatu ilipokea kipigo cha mabao 2-1kutoka kwa Lecce nao mabingwa watetezi Inter Milan, sasa wako nyuma kwa pointi11 kwa Milan, baada ya kushinda 2-1 dhidi ya Catania shukrani kwa mabao mawili ya Esteban Cambiasso.

Wageni Udinese walifunga bao la kwanza dakika ya 35, wakati shuti la Gokhan Inler lilipogonga mwamba na kumkuta Antonio Di Natale, aliyeingia kwenye orodha ya wafungaji wa Serie A sawa na Cavani.

Milan walisawazisha kabla ya mapumziko wakati Zlatan Ibrahimovic alipompitishia krosi safi Alexandre Pato aliyefunga bao hilo.

Sampdoria walitoa zawadi kwa AS Roma walipokubalia kufungwa mabao 2-1 wakati beki Juan akitoa mchango katika kupatikana kwa mabao yote ya mchezo huo, lakini Palermo wameendelea kusuasua baada ya kulazimisha suluhu na Chievo.

Hali imezidi kuwa mbaya kwa kocha Fiorentina, Sinisa Mihajlovic baada ya kushudia vijana wake wakipokea kipigo cha mabao 3-2 nyumbani kutoka kwa Brescia.
Vibonde wa ligi hiyo Bari walipokea kipigo cha mabao 2-0 nyumbani kutoka kwa Bologna.
 
Yanga lipeni madeni
Sunday, 09 January 2011 20:46

nchunga%20yanga.jpg
Mwenyekiti wa Yanga,Lloyd Nchunga.

MWISHONI mwa mwaka jana klabu ya Yanga ilisema inatarajia kutumia shilingi 4.5 bilioni kwa ajili kukarabati wa Uwanja wao wa Kaunda na kukarabati jengo lao la mtaa wa Mafia Jijini Dar es Salaam ili liwe la kisasa zaidi, ukarabati ambao utachukua miaka miwili.

Uongozi wa Yanga ulisema umeshaingia mkataba na Kampuni ya Nedco ambayo imeshaanza uchoraji wa ramani wa Jengo hilo ambalo litakuwa na gorofa 10 pamoja na ukaguzi wa uwanja kabla hawajaanza kazi rasmi ya ujenzi.

Pia uongozi huo ulisema kwa sasa klabu yao haina fedha, ila kampuni ya uchoraji itakapokamilisha uchoraji wa ramani, klabu ya Yanga itakuwa ikifanya tafrija mbali mbali kama kuandaa chakula na kuwaalika waheshimiwa na makampuni mbali mbali kwa ajili ya kuchangia na kufanya matamasha ambayo yataiingizia Yanga fedha za kukamilisha ujenzi huo.

Ukiacha masuala hayo ya maendeleo yanayotaka kufanywa na viongozi wa Yanga, klabu hiyo imekuwa ikielezwa kudaiwa fedha na wachezaji wake, wachezaji iliyovunja nao mkataba, makocha wake na hoteli ya Holiday Inn.

Tunaamini Yanga ni kati ya klabu kubwa barani Afrika ambayo inatakiwa kujiendesha kibiashara zaidi na kuacha utaratibu wa kujiendesha bila utaratibu kiasi kwamba inakuwa inadaiwa madeni madogo lakini inazungusha kulipa.

Tunatarajia uongozi wa Yanga utahakikisha unalipa madeni yote wanayodaiwa ili waweze kuendelea vizuri na utaratibu wao mzuri wa kutaka kuiboresha klabu yao kwa kukarabati Uwanja wao wa Kaunda na kukarabati jengo lao la mtaa wa Mafia.

Tunasema hivyo kwa kuamini Yanga ina mtandao mkubwa wa wanachama, mashabiki, udhamini na vyanzo mbalimbali vya mapato pamoja na rasilimali ilizonazo ambazo zinatosha kuhakikisha wanapata fedha na kulipa madeni yao, badala ya kukaa na kumtegemea mfadhili wao.
 
Udhamini uongezwe mashindano ya vijana
Sunday, 09 January 2011 20:39

MASHINDANO ya Vijana chini ya umri wa miaka 20, yanayojulikana kama Kombe la Uhai yatafikia tamati leo kwa kuzikutanisha Ruvu Shooting dhidi ya JKT Ruvu huku ubingwa akitarajiwa kujinyakulia kiasi cha shilingi 1.5 milioni na medali za dhahabu.

Washindi wa pili katika mashindano hayo watajitwalia medali ya fedha na Shs 1 milioni, washindi watatu watapewa shs 500,000 na timu yenye nidhamu shs 400,000.

Mfungaji bora atapata sh 300,000, mchezaji bora wa mashindano yote atapata Sh 400,000 wakati kipa bora atapata kiasi cha sh 300,000.

Mashindano ya mwaka huu kwa kiasi fulani yamefanikiwa kulinganisha na mashindano ya mwaka jana, ambapo mwaka huu zipo zawadi nyingi tofauti na zilizotolewa mwaka jana.

Pamoja na kufanikiwa kwa kiasi fulani kwa mashindano hayo ya vijana ambayo tunaamini ndio msingi sahihi wa maendeleo ya soka hapa nchini,bado kumekuwa na mapungufu mengi yanayohitaji kuangaliwa kwa umakini zaidi.

Tunaamini udhamini unaotolewa katika mashindano haya ya vijana bado hautoshi kwa sehemu kubwa ndio maana baadhi ya timu kama AFC Arusha walikuwa wakilalamikia kufukuzwa kwenye hoteli waliyofikia pamoja na timu ya Majimaji kuthubutu kucheza pekupeku.

Kama tunavyosema kila siku udhamini wa michezo yoyote hauwezi kuchukuliwa na kampuni au mtu moja, TFF wanapaswa kutafuta wadhamini wengi zaidi ikiwa ni pamoja na mahoteli ili kutoa uhakika wa malazi na chakula kwa vijana hawa, udhamini wa vifaa, udhamini wa maandalizi na usafiri.

Pia tunaamini udhamini wa kutosha wa zawadi unahitajika ili kuwapa motisha vijana hao waweze kuongeza juhudi ya kuupenda mchezo wa soka ili wawe tegemeo katika klabu zao siku za baadaye pamoja na kuwa wachezaji bora katika timu ya taifa.

Tunakishauri kitengo cha masoko cha shirikisho la soka Tanzania kuchukua mapungufu yaliyojitokeza kwenye mashindano haya ya vijana kama changamoto kwao kwa ajili ya kuboresha mashindano yajayo.

Tunatarajia pia klabu zitaziendeleza timu zao za vijana baada ya mashindano haya kumalizika na kuepuka kasoro za kuwachezesha wachezaji wenye umri mkubwa katika mashindano yajayo, huku tukitarajia TFF itakuwa imewaona wachezaji waliofanya vizuri katika mashindano haya na kuwapa nafasi ya kuwaendeleza.
 
Waliojitokeza kumsaidi Mtagwa tunawapongeza
Friday, 07 January 2011 19:37

afyamtagwa.jpg
UONGOZI wa Chama cha Wachezaji wa Soka Tanzania (Sputanza) wanatarajia kumpeleka nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Jellah Mtagwa mkoani Iringa kwa ajili ya kupatiwa matitabu ya ugonjwa wa Kiharusi unaomsumbua tangu mwaka 2006.

Hatua hiyo imechukuliwa siku chache baada ya gazeti hili kuandika habari kuhusu matatizo ya kiafya yanayomkabili kiungo huyo wa zamani wa Stars kiasi cha kumsababishia kushindwa kumudu gharama za matibabu ikiwa ni pamoja na kujikimu kimaisha na familia yake.

Baada ya gazeti hili kuandika habari za Mtagwa, alitokea msamaria mmoja ambaye amejitolea kumchukua mchezaji huyo wa zamani kwa ajili ya kwenda kupata matibabu mkoani humo, pia wapo waliojitokeza kumsaidia kwa kutoa fedha.

Kitendo cha wadau mbalimbali kujitokeza kumsaidia mchezaji huyu ni kitendo cha kizalendo na kinapaswa kuungwa mkono na wanamichezo wote nchini kutokana na mfumo wa michezo ulivyo nchini unaosababisha wachezaji wengi kuishi maisha magumu wakishastaafu katika michezo mbalimbali.

Tunaamini utamaduni wa kuchangia matibabu kwa wanamichezo wetu ndio tija kwa maendeleo ya taifa na michezo kuliko ule wa kusubili msiba ndipo tunajitokeza kugharamia gharama za mazishi.

Sasa wakati umefika kwa Sputanza kwa kushirikiana na TFF, klabu kuandaa utaratibu wa kukusanya fedha kwa ajili ya kuwasaidia wachezaji wakongwe nchini na kuhakikisha unakuwepo mfumo wa kuwasaidia wachezaji wanapostaafu.

Vyama hivi kwa kushirikiana na klabu kwa kuanzia vinaweza kuandaa mechi za kirafiki hapa jijini Dar es Salaam na mikoani na fedha za viingilio zikatumika kwa ajili ya kugharamia matibabu ya wachezaji.

 
ZESCO kuzinoa Simba, Yanga


Na Zahoro Mlanzi

MABINGWA wa Ligi Kuu ya soka ya Zambia, ZESCO United inatarajia kujipima na wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, Simba na Yanga katika michezo itakayopigwa Jumamosi na Jumapili Uwanja wa
Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa michezo hiyo, George Wakuganda alisema timu hiyo itawasili nchini kesho na ndege ya Shirika la Ndege la nchini humo ikiwa na kikosi kamili.

Alisema wachezaji 20 pamoja na viongozi saba, ndiyo watakaounda kikosi hicho ambapo kwa sasa timu hiyo ndiyo mabingwa wapya katika ligi ya nchini humo.

"Mabingwa hao wa Zambia, watacheza na mabingwa wa Tanzania Bara, Simba siku ya Jumamosi na Jumapili watacheza na Yanga, katika michezo ambayo ninaamini itakuwa ni kipimo tosha kwa timu hizo katika maandalizi yao ya michuano ya kimataifa," alisema Wakuganda.

Mbali na mchezo huo, Wakuganda alisema Jumatatu Simba itashuka tena uwanjani kuumana na SOFAPAKA kutoka Kenya, ambayo inatarajia kutua nchini Ijumaa ikiwa na kikosi kamili.

Alisema michezo yote hiyo itakuwa na kiingilio kimoja ambapo Viti Maalum (VIP) sh. 15,000, Jukwaa Kuu sh. 10,000, Jukwaa la Kijani sh. 5,000 na mzunguko ni sh. 3,000.

ZESCO imetwaa ubingwa ikiwa na pointi 60 na michezo miwili mkononi ambapo timu inayofuata, Nchanga Rangers ina pointi 53 na kwa upande wa SOFAPAKA wao wamemaliza ligi wakiwa katika nafasi ya nne nyuma ya mabingwa Ulinzi.
 
Congo, Ivory Coast zatesa U-17 Afrika


KIGALI, Rwanda

TIMU ya taifa ya Gambia imepata kichapo cha nguvu katika michuano ya Afrika kwa vijana wenye miaka chini ya 17, baada ya kufungwa mabao 3-0 na Congo juzi.Ikiwa ni siku ya pili tangu kuanza kwa mashindano hayo nchini
Rwanda, mechi hiyo ilipigwa kwenye Uwanja mpya wa Umuganda mjini Gisenyi uliopo mpakani mwa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Gambia watatakiwa kushinda mechi dhidi ya Mali na Ivory Coast, ili iweze kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

Congo ilipata bao la kwanza dakika ya saba kupitia kwa Samarange Binguila na bao la pili lilitumbukizwa kimiani dakika tatu baadaye na Stevy Epako.
Binguila alimalizia shangwe kwa kufunga bao la tatu dakika ya 51 na kuwamaliza nguvu wapinzani wao.

Uwanja huo mpya wenye uwezo wa kuingiza mashabiki waliokaa kwenye viti 6000, ulizidiwa na mashabiki, Ivory Coast ilitoka nyuma na kuichapa Mali mabao 2-1.

Ivory Coast walichapwa bao dakika ya 25, lililofungwa na Tiecoro Keita. Lakini walitulia na kufanya mashambulizi yaliyozaa bao la kusawazisha dakika ya 47, kupitia kwa Drissa Diarrassouba.Ushindi wa Ivory Coast, ulipatikana dakika ya 70, kwa njia ya penalti iliyopigwa na Stephane Bedi.

Kesho katika Kundi A, litakuwa na mechi kati ya wenyeji Rwanda na Misri, wakati Burkina Faso wataumana na Senegal, mshindi atajiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele, wakati atakayefungwa atakuwa katika nafasi ya kutoka.

Timu mbili katika kila kundi, zitakazofuzu kucheza nusu fainali, zitakata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wenye miaka chini ya 17 nchini Mexico, Juni mwaka huu.Hii ni mara ya pili katika miaka miwili, Rwanda kuandaa fainali za Afrika, mwaka juzi iliandaa fainali za vijana wenye miaka chini ya 20.

 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom