Rutashubanyuma
JF-Expert Member
- Sep 24, 2010
- 219,468
- 911,184
- Thread starter
- #2,801
Simba, Yanga fainali Mapinduzi leo
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 11th January 2011 @ 23:59
MIAMBA ya soka nchini Simba na Yanga leo itamenyana kuwania fainali za Kombe la mapinduzi katika uwanja wa Amaan Zanzibar.
Timu hizo zimeshakutana mara nyingi tangu kuanzishwa kwake lakini mechi ya leo ni ya
kipekee kutokana na timu hizo kukutana Zanzibar kwenye uwanja huo baada ya kupita miaka 19.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Zanzibar mwaka 1992 kwenye michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame) na Simba kuifunga Yanga mabao 5-4 kwa mikwaju ya penati baada ya kutoka bao 1-1 kwa dakika 120.
Aidha timu hizo zinakutana zikiwa zimebakiwa na takriban miezi miwili kukutana kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara Machi 5.
Inawezekana kabisa mechi ya leo, Simba ndio yenye mcheche zaidi kwani itataka kuitumia mechi hiyo kulipa kisasi cha kupigwa mara mbili mfululizo na mtani wake Yanga mwaka jana.
Kabla ya kuanza kwa ligi Agosti mwaka jana, timu hizo zilikutana katika mechi ya ngao ya hisani na Simba kufungwa na Yanga.
Lakini pia baada ya miezi miwili tangu kupata kipigo hicho, Simba ilichapwa tena bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi, Oktoba.
Hata hivyo, timu hizo leo zinakutana zikiwa hazina nyota wake kama Juma Kaseja, Kelvin Yondani, Juma Nyoso, kwa upande wa Simba na kwa Yanga itawakosa Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub, na Jerryson Tegete ambao wapo kwenye timu ya Taifa inayoshiriki michuano ya Bonde la Mto Nile, Misri.
Tegete ndiye aliyefunga bao la ushindi walipokutana Oktoba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba
Mwanza na aliapa atakuwa akiifunga Simba kila atakapokutana nayo.
Lakini mechi ya leo inatarajiwa kuwa na msisimko wa hali ya juu na matokeo hayatabiriki kwani kila upande utakuwa na wachezaji wake wapya iliowasajili kwenye dirisha dogo na wanaonekana ni wazuri hasa Davis Mwape wa Yanga ambaye karibu kila mechi anazochezea timu hiyo hakosi kufunga.
Timu hizo hazijaachana sana kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwani zimepishana kwa pointi mbili. Simba inaongoza ikiwa na pointi 27 na Yanga inashika nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 25.
Katika michuano hiyo ya kuadhimisha kilele cha Mapinduzi ya Zanzibar, sherehe zitafanyika
leo kwenye uwanja huo.
Yanga haikuanza vizuri sana kwani ilitoka sare mara mbili, dhidi ya Zanzibar Ocean View, Chuoni na kuifunga Azam huku Simba ikiifunga Jamhuri, KMKM na kutoka sare dhidi ya Mtibwa Sugar.
Katika mechi ya nusu fainali, Simba iliifunga Zanzibar Ocean View na Yanga kuifunga Mtibwa Sugar.
Akiizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Simba Patrick Phiri alisema anajua itakuwa ngumu lakini amejiandaa vizuri kuibuka na ushindi.
"Yanga wameshanifunga mara mbili mwaka jana, safari hii vijana wangu hawatakubali tumeajindaa kushinda mechi na tuna imani tutashinda," alisema Phiri ambaye aliipa Simba ubingwa wa ligi mwaka jana bila kupoteza mechi.
Naye kocha wa Yanga, Kostadin Papic alisema anajua atashinda mechi kwani Simba ameshaisoma na ndio maana aliweza kuifunga mara mbili mfululizo, haimpi tabu.