ZIFF, Bongo Movies ndani ya Iran
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 5th February 2011 @ 23:50
ZANZIBAR International Film Festival (ZIFF) bado imedhamiria katika kukuza soko la filamu za hapa nyumbani na katika kufanya hivyo iko mjini Tehran, Iran katika tamasha kubwa la Fajr International Film Festival linaloambatana na Iran Film Market.
ZIFF inajaribu kupata wasambazaji, wazalishaji ama wawekezaji wa filamu duniani ambao wangependa kununua, kusambaza, kutengeneza ama kufanya kazi ya pamoja na kiwanda cha filamu hapa Bongo.
"Kwa wakati huu ilikuwa rahisi kupata filamu toka Steps na Pilipili kwa ajili ya kuja kuangalia soko huku Mashariki ya Kati na Asia, natumai mambo yataenda vizuri, napenda kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi nzuri ili zipate kuuzika," alisema Meneja wa ZIFF, Daniel Nyalusi aliyeko Iran.
Pia ZIFF imeenda kuangalia namna ya kupata wawekezaji wa tasnia hii ili kuleta uchangamfu kwa watengenezaji wa ndani na pia kupata filamu toka nchi mbali mbali zitakazooneshwa katika tamasha la mwaka huu Juni 18 - 26, 2011.